Na Benedict Liwenga-Maelezo, Dodoma
Fedha zote zinazokusanywa kutokana na Michezo kupitia Wizara
ya Habari, Vijana, Tamaduni na Michezo zinatumiwa kwa watanzania wote kutokana
na kuchangia kwenye mfuko Mkuu wa Serikali.
Akijibu swali bungeni kwa niaba ya Waziri wa Habari, Vijana,
Tamaduni na Michezo, Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Amos Gabriel Makalla
amesema kuwa mapato yanayokusanywa kutokana na shughuli mbalimbali zizazofanywa
na Wizara hiyo ikiwemo za Uwanja wa Taifa hutumiwa na serikali katika huduma
mbalimbali kwa wananchi wa Tanzania.
Mhe. Makalla alikuwa akijibu swali lililoulizwa na Mhe.
Philipa Geofrey Mturano (Viti Maalumu) ambaye alitaka kujua wilaya ya Temeke
ambayo ndiyo mwenyeji wa Uwanja wa Taifa inanufaikaje na mapato yatokanayo na
uwanja huo.
Amesema wilaya ya Temeke hunufaika na mapato yatokanayo na matumizi
ya Uwanja wa Taifa ambayo huingia kwenye mfuko Mkuu wa Serikali. Mapato hayo
yanatokana na asilimia kumi na nane (18%) ambayo ni kodi ya ongezeko la thamani
(VAT) inayokatwa kwa kila mchezo unaochezwa na kupelekwa TRA na pia gawio la
asilimia kumi na tano (15%) ambazo hukatwa kama ada ya matumizi ya uwanja.
“Mapato yote hayo hutumiwa na serikali katika kutoa huduma
mbalimbali kwa wananchi wa Tanzania ikiwa ni pamoja na Manispaa ya Temeke”.
Alisema Naibu Waziri.
Makalla amebainisha kuwa tangu Uwanja wa Taifa uanze kutumika
mwezi Agosti, 2007 hadi kufikia mwezi Februari mwaka huu, ulikuwa umeingiza
shilingi 1,533,697,666 kwa makusanyo yanayopitia Wizara ya Habari, Vijana,
Tamaduni na Michezo ambazo hizo ni nje ya mapato yanayokusanywa kupitia kodi ya
ongezeko la thamani (VAT) yanayowasilishwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF).
Kuhusu kuwepo na mianya ya rushwa, ufisadi na upotevu katika
makusanyo ya mapato, Naibu Waziri Makalla amesema Wizara yake itafuatilia
lakini pia serikali itaunda mbinu mpya za kukagua tiketi wakati wa michezo.
Licha za serikali kukabiliana na changamoto nyingi katika
sekta ya michezo kama vile uchakavu wa miundo mbinu ikiwemo viwanja mbalimbali
vya michezo hapa nchini, serikali imejipanga vema katika kuhakikisha kuwa
changamoto hizo zinapungua ama kwisha kabisa na pia inaandaa mbinu mbalimbali
za kuepusha mianya ya rushwa kujitokeza katika sekta ya michezo.
0 comments:
Post a Comment