Nafasi Ya Matangazo

March 09, 2013



Jeshi la Polisi limeanza kuwashughulikia waliotuma ujumbe wa matusi kwa simu ya mkononi kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda na Naibu wake, Job Ndugai.

Hali hiyo imedhihirika baada ya mkazi wa  Ihumwa mjini hapa, Noel Mulingwa (26) jana kufikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Dodoma Mjini kujibu mashitaka ya kutumia lugha ya matusi kupitia ujumbe mfupi wa simu ya mkononi.

Akimsomea mashitaka, Wakili wa Serikali Farhat Seif, alidai mbele ya Hakimu Rebeca Mbilu kuwa Februari 16 Ihumwa, mshitakiwa alituma ujumbe wa matusi kupitia namba 0754 46..26 iliyosajiliwa kwa jina la Anne Makinda kwa kutumia simu namba 0763 44..56 huku akijua kufanya hivyo ni makosa.

Katika mashitaka ya pili, ilidaiwa kuwa Februari 10 Ihumwa, mshitakiwa pia alituma ujumbe wa matusi kwenye namba 0762 60..61 iliyosajiliwa kwa jina la Job Ndugai kwa simu namba 0763 44..56.


Mshitakiwa alikana mashitaka na kurudishwa rumande hadi Machi 21, kesi yake itakapotajwa ambapo pia Mahakama itafikiria dhamana yake.

Awali Jeshi la Polisi lilidai kuwa, Mlingwa alikamatwa Februari 12 katika eneo la sekondari ya City mjini hapa kwa tuhuma za kutuma ujumbe wa maandishi wenye vitisho na matusi kwa Spika wa Bunge la Tanzania na Naibu wake.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, David Misime alitoa mwito kwa wananchi wote wa mkoa wa Dodoma kuacha kutumia simu zao za mkononi kwa kutuma ujumbe wa matusi na vitisho kwa watu wengine; yeyote atakayefanya hivyo atakamatwa na atafikishwa katika vyombo vya sheria.

Februari 10 viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), walitoa namba za simu za Makinda na Ndugai ili wananchi wawashinikize viongozi hao kujiuzulu kwa madai kuwa walikuwa wakikandamiza upinzani bungeni.

Ofisi ya Bunge kupitia kwa Katibu wake, Thomas Kashilillah ikalitaka Jeshi la Polisi kuchukua hatua kali dhidi ya waliotumia lugha ya matusi kwa njia ya ujumbe mfupi au kwa kupiga simu kwa Spika na Naibu wake.

Hata hivyo, Spika Makinda alipata kukaririwa akisema alitumiwa ujumbe mfupi zaidi ya 400 na kupigiwa simu zisizopungua 200, zilizokuwa zikimkashifu na nyingine zikimtisha, huku Naibu Spika akipokea ujumbe na simu kadhaa zenye matusi.
Posted by MROKI On Saturday, March 09, 2013 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo