Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akimjulia
hali Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, ambaye pia ni Mhariri Mtendaji
Mkuu wa Kampuni ya New Habari 2006 Ltd, Absolom Kibanda, aliyelazwa
katika Wodi ya Moi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, baada ya
kujeruhiwa na watu
wasiojulikana usiku wa kuamkia leo wakati akiingia nyumbani kwake
maeneo ya Mbezi Beach jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mwenyekiti Mtendaji
wa Kampuni ya IPP Regnard Mengi
******
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri na Mhariri Mkuu wa Mtendaji
wa Kampuni ya New Habari 2006, wachapishaji wa magazeti ya Mtanzania, Dimba,
Bingwa na Dimba, Absalom Kibanda, amevamiwa na watu wasiojulikana usiku wa
kuamkia leo akiwa ndani ya gari lake wakati akiingia nyumbani kwake maeneo ya
Mbezi-Beach, jijini Dar es Salaam.
Akielezea tukio hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya New
Habari, Hussein Bashe amesema Kibanda alivamiwa majira ya saa sita usiku wa
jana, akitokea kwenye majukumu yake ya kila siku. Inadaiwa kuwa alitolewa
kwenye gari, akapigwa kichwani, akajeruhiwa jichoni na kisha kutelekezwa mbali
kidogo ya nyumbani kwake.
Baada
ya tukio hilo, wasamaria wema waliomwona walimpeleka katika Hospitali ya Taifa
ya Muhimbili, ambako alipokelewa vizuri na madaktari na kumpatia tiba ya awali
na baadaye kumhamishia kwenye Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI) ambako mpaka sasa
anaendelea na matibabu.
Watu
waliotenda ukatili huo hawakuchukua kitu chochote kwenye gari.
Kwa mujibu wa maelezo ya mgonjwa aliyekaririwa akizungumza
kwa shida, ameeleza kuwa, majira ya usiku wakati akiingia nyumbani kwake
alivamiwa na watu watatu --mmoja akiwa ameshika bastola na wawili wakiwa
wameshika nondo-- ambapo alipofika nje ya nyumba yake, watu hao walilivamia
gari lake na kuvunja mlango wa gari lake, wakamtoa nje, wakaanza kumshambulia,
wakamtoa meno mawili, wakamng'oa kucha katika moja ya vidole vyake na kumtoboa
jicho lake kwa nondo.
Mwenyekiti wa TASWA, Juma Pinto, alisema kuwa watu hao waliohusika wakamatwe ili sheria ichukue mkondo wake.
''Tusingependa
kama waandishi kuamini yanayosemwa lakini kutokana na uadilifu mkubwa wa vyombo
vyetu vya ulinzi na Usalama kuwapata watu ambao wamehusika na tukio hilo.
Sisi
tunaamini tukio hili la mwenzetu kuvamiwa na watu hao halikuwa kwa bahati mbaya
ni Jambo ambalo linaonekana Kama limepangwa na Kama ni hivyo lengo na madhumuni
yake ni nini kwa waandishi wa Tanzania? Uhuru na Usalama wa waandishi upo wapi?
Kutakana
na tukio hili la mpiganaji na Kiongozi wetu kuvamiwa ,ipo haja ya sisi
waandishi kuungana pamoja katika kutafuta Usalama wetu. Kuna matukio mengi ya
waandishi yametokea na tumekuwa tukipiga kelele lakini matokeo yake hakuna
hatua ambazo serikali inayafanyia kazi.
Kutokana
na majeraha makubwa aliyopata mwenzetu, tunaiomba serikali na
hasa Mheshimiwa Rais, Dr. Jakaya Kikwete kutoa Msaada wa mwenzetu kwenda
kutibiwa nje,tunaamini serikali ni sikivu na Rais wetu ni mwenye kusikia kilio
cha watu wake'' alisema Pinto.
Kibanda
na wenzake ndani ya Jukwaa la wahariri wamekuwa mstari wa mbele katika
kurudisha hadhi ya tasnia ya habari na kujenga umoja miongoni mwa waandishi wa
habari na kuifanya tasnia ya habari kuheshimika tofauti na ilivyokuwa nyuma.
Tunaungana
na kampuni ya habari, wafanayakazi wenzake, familia yake na waandishi wote kwa
jumla na kumuomba Mungu amponye ili tuweze kuungana nae katika kusaidia kupasha
habari Watanzania lakini ili aweze kuwaongoza waandishi wenzake.
0 comments:
Post a Comment