Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Mama Salma Kikwete,
akiwahoji kwa nini walikuwa hawakwenda shule, wanafunzi wa shule ya
msingi Kikwetu, wilaya ya Lindi mjini, walipokuwa kwenye mkutano wake wa
hadhara uliofanyika, leo katika kijiji hicho. Kutoka kulia ni Said
Martin (darasa la saba), Regina Fred na Rahma Mandunda wote wa darasa la
sita. (Picha na Bashir Nkoromo).
*** ***
Na
Anna Nkinda – Maelezo , Lindi
Wanafunzi
wametakiwa kuachana na tabia zisizoendana
na maadili ya kiuanafunzi ikiwemo utoro
na mashindano ya mavazi bali wasome kwa bidii na kutengeneza mazingira ya
kujisomea ili waweze kufanya vizuri katika mitihani yao kwani elimu inaweza kuwatoa
katika hali duni ya maisha na kuwaweka
katika hali nzuri.
Wito
huo umetolewa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete alipokuwa akiongea kwa nyakati tofauti na wananchi wa kata za Jamhuri, Makonde na Ndoro
zilizopo katika wilaya ya Lindi mjini
wakati wa ziara yake ya kuwashukuru wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa
kumchagua kuwa mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM kutoka wilaya hiyo.
Mama
Kikwete ambaye pia ni MNEC alisema kuwa licha ya kuwa na tatizo la upungufu wa
walimu na vifaa vya kufundishia lakini wanafunzi wengi wa siku hizi ni watoro,
hawapendi kusoma, hawawatii wazazi na walimu wao, siyo wasikivu wawapo darasani
jambo linalosababisha kutofanya vizuri katika mitihani yao.
“Wanafunzi
lazima mtambue kuwa elimu haina mwisho na elimu ndiyo msingi wa maendeleo,
someni acheni tabia ya utoro na mkimaliza darasa la saba jiungeni na elimu ya
sekondari, baada ya hapo msome hadi chuo
kikuu hali hii itasaidia kupata
wataalamu wengi zaidi na hivyo kupunguza tatizo la watumishi”, alisema Mama
Kikwete.
Kwa
upande wa wazazi aliwataka kusimamia maendeleo ya elimu ya watoto wao na
kuhakikisha kuwa wanakwenda shule na kuhudhuria madarasani na kutowaachia
jukumu hilo walimu peke yao kwani kama watoto wao hawatasoma ni vigumu kwa mkoa
huo kusonga mbele kimaendeleo kwa kuwa maendeleo hayapatikani bila ya kuwa na
elimu.
“Maendeleo
ya elimu katika mkoa wa Lindi ni mabaya ukilinganisha na mikoa mingine tatizo
hili likiachwa kwa muda wa miaka 10 hali itakuwa mbaya zaidi. Suala la ufaulu
mdogo wa wanafunzi lisiwakatishe tamaa na kuwarudisha nyuma bali nyote kwa
pamoja wanafunzi, walimu, wazazi na viongozi wa Vyama vya siasa na Serikali mchukue
hatua za makusudi ili muweze kuinusuru hali hii”, alisema Mama Kikwete.
Tatizo
la utoro lilijidhihirisha pale ambapo zaidi ya wananafunzi 33 kutoka shule ya
msingi Tulieni na juzi wanafunzi zaidi ya 40 wa shule ya msingi Kikwetu walihudhuria
katika mikutano ya hadhara muda wa masomo wakiwa pamoja na wazazi au ndugu zao na Mama
Kikwete alipowauliza kwanini hawakwenda shule hawakutoa sababu za msingi.
Aidha
Mama Kikwete pia aliwasihi wananchi hao kulima
mashamba yao, kupanda , kupalilia na kuvuna kwa ushirikiano kama walivyokuwa
wakifanya miaka ya nyuma na kuachana na tabia ya
kila mtu kulima shamba lake peke yake kwani kwa kulima kwa ushirika kwa muda mfupi wanalima hekari nyingi tofauti na kulima mtu mmoja
mmoja.
Pia
aliwataka viongozi wa vyama vya Siasa na
Serikali kuacha tabia ya kuchanganya lugha ya Kiswahili na kiingereza wakati
wanajibu maswali au kuongea na wananchi kwa kuwa wananchi wengi hawafahamu lugha hiyo zaidi ya
lugha ya Kiswahili na hivyo kuwafanya wasielewe mambo mbalimbali ya maendeleo
yao.
Kwa
upande wake Diwani wa kata ya Jamuhuri Nelson Bebo alisema kuwa wakazi wa kata
hiyo wamenufaika na miradi ya kopa
ng’ombe lipa ng’ombe, ufugaji wa kuku wa kienyeji na mayai na ufugaji wa mbuzi
na kujipatia kipato cha ziada ambacho kimeongeza pato la familia.
Akiwa
katika kata za Jamhuri, Makonde na Ndoro Mjumbe huyo wa NEC alikabidhi kadi
kwa wanachama wapya wa CCM 47, Umoja wa vijana 32, Umoja wa
Wanawake 52 na Jumuia ya Wazazi 39.
0 comments:
Post a Comment