Balozi Joel M Nheleko wa Swaziland nchini
Ubeligiji, ambaye alikuwa Rais wa Mabalozi wa Afrika nchini Ubeligiji
aliyemaliza muda wake, akimkabidhi Balozi wa Tanzania Dk. Diodorus Kamala mfuko
wenye vitendea kazi kama ishara ya kumkabidhi Urais wa Mabalozi wa Afrika
Ubeligiji jijini Brussels juzi.
**** ****
Balozi wa Tanzania nchini Ubeligiji, Dk.
Diodorus Kamala ameteuliwa na mabalozi wa nchi za Africa wanaoziwakilisha nchi
zao nchini humo kuwa Mwenyekiti wao.
Balozi Kamala amepokea uenyekiti huo kutoka kwa
Balozi wa Swaziland nchini Ubeligiji, Joel Nheleko aliyemaliza muda wake.
Tanzania itashikilia kiti hicho kwa muda wa miezi sita hadi Julai 1, 2013.
“Nimefurahi kupewa heshima hii, na naamini
nitaitumia fursa hii kufahamiana vizuri na mabalozi wenzangu na kuvutia fursa
za kiuchumi kwa nchi yetu,” alisema Balozi Kamala.
Wakati huo huo, juzi mabalozi wa nchi tano
zinazozunguka Bonde la Ziwa Tanganyika, walimchagua Balozi Kamala kuwa
mwenyekiti wao.
Nchi wanachama wa Bonde la Ziwa Tanganyika ni
Burundi, Rwanda, Tanzania, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Zambia.
Nchi hizi zimeunganisha nguvu kutafuta wafadhili
kwa ajili ya maendeleo ya Bonde la Ziwa Tanganyika, ambapo eneo la bonde hili
lenye wakazi wastani wa milioni 40 wanalenga kuliendeleza kwa ajili ya kujenga
miundombinu, kurahisisha usafiri na usafirishaji, kujenga reli mpya na
kuendeleza utalii.
Chini ya mpango huu wanalenga pia kuboresha
viwanja vya ndege vya nchi wanachama vya Mbala, Kalemie, Bujumbura, Kigoma na
Kasanga kwa nia ya kurahisisha usafiri wa anga katika ukanda huu.
Dk. Kamala amekabidhiwa jukumu la kuratibu
mpango huu na kwa pamoja watatafuta fedha kutoka kwa wafadhili kwa ajili ya
mradi huu.
0 comments:
Post a Comment