Nafasi Ya Matangazo

January 25, 2013

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka ameanzisha Wakala wa Kuendeleza Mji wa Kigamboni (KDA). Kwa maana hiyo, mji huo hautakuwa tena chini ya mamlaka ya Manispaa ya Temeke.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Profesa Tibaijuka alisema Serikali imeamua kuanzisha wakala huo ili pamoja na mambo mengine, upange na kusimamia ujenzi wa mji wa kisasa katika eneo hilo.
“KDA imeanzishwa chini ya Sheria ya Wakala wa Serikali ya 1997 ili iweze kuhakikisha mji unajengwa na unakuwa bora,” alisema Profesa Tibaijuka.
Alisema kutokana na kuanzishwa kwa KDA, kata zote za Kigamboni, zitaungana na madiwani wake pamoja na mbunge wao watakuwa wakikutana katika Baraza la Ushauri la KDA.

“Kutakuwa na Baraza la Kigamboni ambalo madiwani na mbunge wao wataingia humo kujadili maendeleo ya mji huo na leo (jana), kutakuwa na kikao cha kwanza,” alisema Profesa Tibaijuka.

Alizitaja kata hizo kuwa ni Kigamboni, Tungi, Mjimwema, Vijibweni, Kibada, Pemba Mnazi, Kimbiji, Kisarawe II, Somangila, Kendwa, Sinda Chini na Sinda Juu.

Profesa Tibaijuka alisema eneo lote la Kigamboni lenye hekta 50,935, litaendelezwa na wananchi 80,000 wa eneo hilo watanufaika.

Profesa Tibaijuka alisema wananchi wa Kigamboni ambao wako kwenye maeneo ambayo yatahitajika kwa ajili ya ujenzi huo watashirikishwa ipasavyo katika mchakato mzima ikiwa ni pamoja na kulipwa fidia zao kwa wakati.
Alisema fidia itatolewa kwa kila mwananchi na wahusika watahamishiwa katika maeneo mengine ndani ya mji huohuo wa Kigamboni, ili kupisha ujenzi.
“Mwananchi yeyote ambaye hatajisikia kubaki Kigamboni atalipwa fedha zake na kwenda kuishi kokote anakotaka iwe ni Kimara au Kibaha ataamua mwenyewe na tayari majengo ya kuwahamishia yameshaanza kujengwa,” alisema.
Profesa Tibaijuka alisema ni wakati wa Watanzania wanaoweza kuendeleza eneo la Kigamboni kujitokeza ili wapewe ‘blocks’ na kuondokana na suala la viwanja.

Alisema zaidi ya Sh11 trilioni zitatumika kujenga mji huo mpya ambao unatarajiwa kukamilika ifikapo 2032.

“Bajeti ya mwaka huu tulihitaji Sh600 bilioni, lakini tukapewa asilimia 10 ya fedha hizo ambayo ni Sh60 bilioni. Tunajipanga na hii ni moja ya mipango yetu kufanikisha ujenzi huo. Katika awamu ya kwanza tutahitaji kiasi cha Sh3 trilioni ili kuifanikisha.”

Mbunge hataki
Mbunge wa Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile amepinga kuanzishwa kwa KDA na kueleza ni kuongeza gharama kwa Serikali akataka Manispaa ya Temeke iwezeshwe ili isimamie mji huo.

“Walishakuja na kutueleza hilo suala hata hivyo, sisi na manispaa tulikataa kwa kuwa uwezo wa kufanya kazi hiyo manispaa inayo hivyo hatuikubali mamlaka hiyo,” alisema Dk Ndugulile.
Aidha, alikanusha taarifa ya Profesa Tibaijuka kuwa angekutana nao katika mkutano wa Baraza jana akieleza kuwa hakuna mkutano kama huo kwa kuwa yeye na madiwani wenzake hawajataarifiwa. Source: Mwananchi.
Posted by MROKI On Friday, January 25, 2013 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo