Akizungumza jana, mumewe huyo, Charles Gibore, pamoja na mambo mengine
alimtaka Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hoseah(pichani) na Jeshi
la Polisi kufanya uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo kubaini ukweli.
“Mke wangu aliuawa na mfanyakazi mwenzake na tukio hilo limegubikwa na
utata ambao Takukuru na Polisi ndiyo pekee wanaoweza kutupa ukweli,”
alisema Gibore nje ya chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya
Taifa ya Muhimbili (MNH), Dar es Salaam.
Gibore alieleza kuwa mkewe huyo aliuawa usiku wa kuamkia Jumapili katika
tafrija ya kuagana na kupongezana na baadhi ya wafanyakazi wenzake wa
Takukuru waliokuwa wamepandishwa vyeo, tafrija ambayo Bhoke alipewa
zabuni ya kupika chakula.
Alisema pia mkewe aliombwa pia awapatie wenye sherehe hiyo, vijana
wawili wa kuwachomea nyama... “Vijana hao walikwenda asubuhi ukumbini
ili kuandaa eneo la kuchomea nyama, huku Bhoke akiwa bado nyumbani
akiandaa chakula,” alisema Gibore na kuongeza:
“Wale vijana walinieleza kwamba baadaye saa 8:30 mchana, Bhoke na
wenzake walifika ukumbini na kuwakuta vijana wawili wanaofanya nao kazi
wakinywa pombe, huku wakichezea silaha aina ya bastola kujaribu
shabaha.”
“Vijana hao walifyatua risasi juu na ndipo muuaji alipompiga kichwani
marehemu katika jicho na mauti yalimfika muda mfupi,” alisema.
Alisema baada ya hapo muuaji huyo alitoweka kisha kujisalimisha mwenyewe
katika Kituo Kikuu cha Polisi Mkoa wa Temeke, Chang’ombe.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Engelbert Kiondo
alithibitisha mtuhumiwa huyo kujisalimisha na kisha kushikiliwa kituoni
hapo na kueleza kuwa amekuwapo hapo Jumamosi iliyopita.
Kamanda Kiondo alisema pamoja na mtuhumiwa huyo kujitambulisha kuwa ni
mfanyakazi wa Takukuru, polisi wanaendelea kuchunguza ili kubaini ukweli
wa taarifa hizo.
“Tunaendelea kumshikilia hapa na uchunguzi utakapokamilika tutamfikisha
mahakamani kwa taratibu nyingine za kisheria,” alisema Kiondo.
Marehemu Bhoke
Ryoba alizaliwa Juni 18, 1978 katika Kijiji cha Kiterere, Wilaya ya
Tarime mkoani Mara na anatarajiwa kuzikwa kesho kijijini kwao.
Ameacha watoto watatu; Doloresy (10), Dolrisy (4) na Dolrick Gibore ambaye ana mwaka mmoja. SOURCE: MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment