Rais Kikwete akizindua rasmi mradi mkubwa wa kuboresha na kuendeleza miji ya Tanzania jijini Arusha.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
leo, Alhamisi, Novemba Mosi, 2012, amezindua rasmi mradi mkubwa wa
kuboresha na kuendeleza miji ya Tanzania unaojulikana kama Mradi wa
Uboreshaji Miji ya Tanzania (Tanzania Strategic Cities project – TSCP)
utakaogharimu mabilioni ya fedha.
Aidha,
Rais Kikwete amezidua rasmi Jiji la Arusha katika sherehe ya kufana
iliyofanyika kwenye Mnara wa Azimio la Arusha katikati ya jiji hilo.
Mradi wa TSCP unalenga kuboresha huduma za msingi katika miji saba na
Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) kwa kujenga upya,
kukarabati na kupanua miundombinu pamoja na kuijengea uwezo wa kukusanya
na kusimamia mapato ya miji husika.
Mradi
huo ni mmoja ya miradi mitatu inayogharimiwa na Benki ya Dunia kwa nia
ya kuboresha miji ya Tanzania. Mbali na TSCP, miradi mingine ni Mradi wa
Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam (Dar es Salaam Metropolitan
Development Project - DMDP) na Urban Local Government Strengthening
Programme (ULGSP). Mpaka sasa Benki hiyo imekwishakutoa sh bilioni 8.76
kati ya sh bilioni 34.7 za TSCP.
Chini
ya TSCP ambao unagharimu kiasi cha sh bilioni 191.3 miji itakayonufaika
ni Tanga, Arusha, Mwanza, Kigoma, Dodoma, Mbeya, Mtwara na CDA ambayo
ndiyo itakayopata pesa kubwa zaidi kuliko mjini mingine.
Aidha, chini ya TSCP, miji hiyo itajengewa miundombinu ya barabara zenye
jumla ya kilomita 141.2, ujenzi wa madampo matano, ununuzi wa vifaa vya
kusimamia taka ngumu, vituo vya mabasi sita, vituo viwili vya kuegesha
malori na kilomita 15.9 za mitaro ya maji ya mvua.
Katika mji wa Arusha, kiasi cha barabara za lami zenye urefu wa kilomita
7.23 zitajengwa, mtaro mkubwa wa maji ya mvua wa mita 800 utajengwa,
zitafungwa taa za kuongoza magari kwenye makutano ya barabara tatu
ambazo ni Sokoine na Viwandani, Sokoine na Esso na Kanali Middleton na
Makongoro. Katika awamu ya pili, kiasi cha barabara zenye urefu wa
kilomita 7.8 zitajengwa katika Jiji la Arusha.
Miji
itakayonufaika na ULGSP ambako Benki ya Dunia inatoa mkopo wa dola za
Marekani milioni 255 na unatarajiwa kuanza katika mwaka ujao wa fedha ni
Morogoro, Tabora, Moshi, Sumbawanga, Shinyanga, Songea, Singida,
Musoma, Iringa, Bukoba, Lindi, Njombe, babati, Kibaha, Mpanda, Geita,
Korogwe na Bariadi.
DMDP kwa ajili ya Jiji la Dar Es Salaam, itahusika wilaya zote tatu za
Kinondoni, Ilala na Temeke na utagharimu kiasi cha dola za Marekani
milioni 75.
Baada
ya kuzindua mradi huo wa TSCP, Rais Kikwete amezindua Jiji la Arusha
ambalo linapanda hadhi kutoka Manispaa. Katika uzinduzi huo, Rais
amezindua nembo ya Jiji pamoja na kukabidhi cheti cha kulipandisha hadhi
Jiji hilo.
Rais Kikwete amezindua miradi hiyo ikiwa ni shughuli zake katika siku ya
kwanza ya ziara yake ya siku mbili kukagua na kuzindua miradi ya
maendeleo katika Mkoa wa Arusha. Rais amewasili Arusha mchana wa leo
kutoka Dodoma.
bango la mradi mkubwa wa kuboresha na kuendeleza miji ya Tanzania
Rais Kikwete akisalimiana na Mbunge wa Arumeru Mashariki Mhe. Joshua Nassari katika sherehe za uzinduzi rasmi wa mradi mkubwa wa kuboresha na kuendeleza miji ya Tanzania jijini Arusha
Wakaazi wa Arusha wakimshangilia Rais Kikwete alipowasili katika sherehe za uzinduzi rasmi wa mradi mkubwa wa kuboresha na kuendeleza miji ya Tanzania
0 comments:
Post a Comment