Mwenyekiti
wa CCM, Rais Jakaya Kikwete na viongozi wa juu baada ya kuwasili
katika ukumbi wa Kizota mjini Dodoma kufungua Mkutano mkuu wa nane wa
CCM, leo.
Makamu
Mwenyekiti Mteule wa CCM (Bara), Phili Mangula (kulia) akiungana na
wanachama wengine kushangilia Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete alipoingia
ukumbini wakati wa mkutano huo.
Baadhi ya wajumbe ukumbini.
wake wa viongozi.
Waaliwa kutoka kutoka nchi za nje.
Waalikwa kutoka vyama vya siasa hapa nchini
Wajumbe wakiwa wamesimama wakati wa wimbo wa Taifa kabla ya kuanza mkutano huo.
Watu waliokuwa nje ya ukumbi wakifuatilia kwenye banda maalum
Kusoma hotuba kamili ya Mwenyekiti wa CCM Rais Kikwete
*********
Mheshimiwa Dkt. Amani Abeid Karume, Makamu Mwenyekiti
wa CCM na Rais Mstaafu wa Zanzibar;
Ndugu Pius Msekwa, Makamu Mwenykiti wa CCM wa Bara;
Mwenyekiti Mstaafu wa CCM, Ndugu Benjamin William Mkapa;
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Waziri Mkuu;
Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ;
Viongozi Wakuu Wastaafu;
Katibu Mkuu wa CCM, Ndugu Wilson Mukama;
Ndugu Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM;
Wageni wetu waalikwa kutoka vyama rafiki,
Ndugu zetu wa Vyama vya Siasa Nchini;
Waheshimiwa Mabalozi,
Viongozi wa Dini,
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana;
Kama ilivyo ada, naomba tuanze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa
rehema kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kukutana hapa Dodoma, siku
ya leo, kwenye Mkutano Mkuu wa Nane wa Chama cha Mapinduzi.
Ndugu Wajumbe;
Karibuni
Dodoma. Karibuni Mkutanoni. Nawapeni pole kwa safari. Tunamshukuru
Mungu kwa kutuwezesha kufika salama na tuombe turejee makwetu salama.
Kwa niaba yenu, niruhusuni niwashukuru wenyeji wetu, yaani wana-CCM na
wananchi wote wa Dodoma, wakiongozwa na Alhaji Adam Kimbisa, Mwenyekiti
wa CCM, Mkoa wa Dodoma na Mkuu wa Mkoa Dkt. Rehema Nchimbi, Mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya Taifa. Tunawashukuru kwa kutupokea vizuri na kwa
ukarimu wao unaotufanya tujisikie tuko nyumbani katika huu mji ambao
ndiyo Makao Makuu ya nchi yetu na Chama chetu.
Ndugu Wajumbe;
Napenda kuchukua nafasi hii kutoa pongezi nyingi kwa
Halmashauri Kuu ya Taifa kwa matayarisho mazuri ya Mkutano huu wa Nane
wa Taifa wa CCM. Natoa pongezi maalum kwa Sekretarieti ya Halmashauri
Kuu ya Taifa chini ya uongozi mahiri wa Katibu Mkuu Ndugu Wilson Mukama
na Kamati zote za Maandalizi ya Mkutano kwa kazi kubwa na nzuri
waliyofanya ya kuwezesha Mkutano huu kufanyika. Kwenu nyote nasema
hongereni na asanteni sana.
Ndugu Wajumbe;
Karibuni tena Kizota. Nasikitika kwamba matumaini yangu ya kufanya
Mkutano Mkuu katika ukumbi wetu wenyewe hayakutimia. Hii ni kwa sababu
kazi ya matayarisho imechukua muda mrefu kuliko nilivyotazamia.
Tumechelewa kupata kiwanja kilichokidhi mahitaji yetu na matazamio
yetu. Kwanza tulipata kiwanja nyuma ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Lakini tukaona ni mbali mno na walipo wananchi.
Tukaja kupata kiwanja kingine juu ya Kilimani Club ambacho hakikuwa kikubwa cha kutosha. Mapema mwaka huu ndipo tulipopata kiwanja eneo la Makulu ambacho kinakidhi sifa za kuwa kikubwa cha kutosha na kuwa karibu na katikati ya mji wa Dodoma. Tumekiafiki na matayarisho ya kuanza ujenzi yamekamilika. Leo asubuhi tumeweka jiwe la msingi kuzindua ujenzi wa Ukumbi wa Mkutano (Dodoma Convention Centre). Baadae utafuta ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya CCM na jengo la Hoteli ya Kisasa.
Tukaja kupata kiwanja kingine juu ya Kilimani Club ambacho hakikuwa kikubwa cha kutosha. Mapema mwaka huu ndipo tulipopata kiwanja eneo la Makulu ambacho kinakidhi sifa za kuwa kikubwa cha kutosha na kuwa karibu na katikati ya mji wa Dodoma. Tumekiafiki na matayarisho ya kuanza ujenzi yamekamilika. Leo asubuhi tumeweka jiwe la msingi kuzindua ujenzi wa Ukumbi wa Mkutano (Dodoma Convention Centre). Baadae utafuta ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya CCM na jengo la Hoteli ya Kisasa.
Wageni Karibuni
Ndugu Wajumbe;
Kama
mjuavyo Chama cha Mapinduzi kina marafiki wengi Afrika na kwingineko
duniani. Tumekuwa na mazoea ya kualikana katika mikutano mikuu yetu.
Safari hii tumefanya hivyo tena. Kwa niaba yenu niruhusuni niwashukuru
sana wageni wetu wote wa kutoka vyama rafiki Afrika na duniani kwa
kukubali mwaliko wetu na kuja kujumuika nasi siku ya leo.
Kuwepo kwao ni kielelezo tosha cha udugu na urafiki uliopo baina ya vyama vyetu na nchi zetu ambao hatuna budi kuudumisha, kuuendeleza na kuukuza. Hali kadhalika, nawashukuru Mabalozi wa Nchi za Nje na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa walioweza kuja kushiriki nasi katika sherehe za ufunguzi wa Mkutano wetu.
Kuwepo kwao ni kielelezo tosha cha udugu na urafiki uliopo baina ya vyama vyetu na nchi zetu ambao hatuna budi kuudumisha, kuuendeleza na kuukuza. Hali kadhalika, nawashukuru Mabalozi wa Nchi za Nje na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa walioweza kuja kushiriki nasi katika sherehe za ufunguzi wa Mkutano wetu.
Ndugu Wajumbe;
Tunawakaribisha
kwa furaha na upendo mkubwa viongozi na wawakilishi wa vyama vya siasa
vya hapa nchini kwa kukubali mwaliko wetu na kuja kuhudhuria Mkutano
Mkuu wa Taifa wa CCM siku ya leo. Tunawashukuru kwa moyo wao wa
uungwana kwani tofauti za vyama si uadui. Wamethibitisha jinsi
demokrasia ya vyama vingi inavyozidi kustawi na kukomaa hapa nchini.
Nawashukuru
sana pia, viongozi wetu wa dini na wananchi mbalimbali waliojumuika
nasi. Kuwepo kwao ni jambo la faraja kubwa. Dua za viongozi wa dini
zitasaidia kuponya na kuupa baraka mkutano wetu uende salama, uwe wa
mafanikio na kuwafanya wale wote wasiokiombea mema Chama chetu
watahayari na kufadhaika.
Karibuni Diaspora
Napenda
kuwatambua na kuwakaribisha viongozi na wananchama wa Chama chetu
waliopo nje, Marekani, Italia, India na Uingereza. Ndugu zetu hawa kwa
upenzi wao kwa Chama wamesafiri masafa marefu kuja kushiriki nasi. Hawa
wanastahili pongezi maalum kwa jinsi wanavyopeperusha bendera ya CCM na
kueneza sera zake. Naomba tuwape makofi ya nguvu.
Agenda ya Mkutano
Ndugu Wajumbe;
Agenda ya Mkutano Mkuu wa Taifa wa Nane wa Chama cha Mapinduzi ina
mambo makuu manne. Kwanza kufanya marekebisho ya Katiba ya Chama cha
Mapinduzi. Mengi ya marekebisho hayo yanatokana na uamuzi wa
Halmashauri Kuu ya Taifa katika kikao chake cha trehe 11 – 12 Aprili
2011 wa kufanya mageuzi ndani ya Chama. Miongoni mwa matunda ya mageuzi
hayo ni kuundwa kwa Baraza la Ushauri na Wajumbe wa NEC kuchaguliwa
Wilayani badala ya Mikoani.
Kwa
mujibu wa Katiba ya CCM, Halmashauri Kuu ya Taifa ina mamlaka ya
kufanya marekebisho ya Katiba na marekebisho hayo kutumika. Hata hivyo,
marekebisho hayo hayana budi kuletwa katika Mkutano Mkuu wa Taifa ili
yaingizwe rasmi kwenye Katiba.
Ndugu Wajumbe;
Jambo la pili litakuwa ni kwa Serikali zetu mbili kutoa taarifa za
maendeleo ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya 2010 – 2015 tangu baada
ya uchaguzi mkuu hadi sasa. Vile vile, tutapokea Taarifa ya
Halmashauri Kuu ya Chama kuhusu kazi za Chama kwa miaka mitano
iliyopita. Jambo la nne na la mwisho ni kufanya uchaguzi wa Mwenyekiti,
Makamu wake wawili na Wajumbe wa NEC wa Kundi la Zanzibar na Tanzania
Bara.
Ndugu Wajumbe;
Tofauti na mikutano iliyopita, Halmashauri Kuu ya Taifa inapendekeza kuwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wajigawe katika makundi matano kujadili
taarifa ya kazi za Chama na zile za utekelezaji wa Ilani. Kisha kila
kikundi kitatoa taarifa ya maoni na mapendekezo yake. NEC ilifikiria
iwe hivyo ili kutoa muda wa kutosha kwa wajumbe kujadili taarifa hizo
muhimu katika utaratibu wa zamani wa mtu mmoja kila mkoa kuitwa kusoma,
wajumbe hawapati fursa ya kutosha ya kuzijadili taarifa zinazotolewa.
Kuimarisha Chama Kazi Endelevu
Ndugu Wajumbe;
Katika hotuba yangu ya kushukuru baada ya kuchaguliwa kwa mara ya
kwanza kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi kwenye Mkutano Mkuu wa
Taifa Maalum wa tarehe 25 Juni, 2006, pamoja na kuzungumzia mambo
mengine, nilisisitiza umuhimu wa kuimarisha Chama chetu. Nilitoa maoni
yangu kwa upana kiasi kuhusu mambo ya kuzingatia. Leo tena, katika
ufunguzi wa Mkutano Mkuu huu narudia kusisitiza jambo hili. Nafanya
hivyo kwa sababu hilo ndiyo jukumu la kudumu na jukumu la kwanza na la
msingi kwa kila kiongozi na kila mwanachamawa CCM. Isitoshe, kwa hali
ilivyo sasa, kuimarisha Chama cha Mapinduzi lazima iwe agenda kuu ya
kila mmoja wetu. Ni ukweli ulio wazi kuwa ustawi na uhai wa Chama
unategemea viongozi na wanachama kufanya kazi ya ziada kuimarisha Chama
chao.
Ndugu Wajumbe;
Bahati
nzuri, chini ya uongozi wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Ndugu Lt.
Yusuf Rajab Makamba tarehe 19 Desemba, 2006 ulianzishwa Mradi wa
Kuimarisha Chama. Mradi huo ndiyo uliokuwa dira na mwongozo wetu wa
kufanya kazi za Chama tangu wakati huo mpaka leo. Wajibu wa kila
kiongozi na kila mwanachama na kila kikao cha kila ngazi vimeainishwa
vizuri. Pia, uliwekwa utaratibu mzuri wa kufuatilia utekelezaji wake.
Bila ya shaka mtakumbuka kuwa utaratibu maalum uliwekwa wa kutoa tuzo
kwa Mikoa iliyofanya vizuri katika utekelezaji wa vipengele mbalimbali
vya uimarishaji wa Chama kwa mujibu wa Mradi huo.
Ndugu Wajumbe;
Kazi
ya kuimarisha Chama chetu ni jukumu endelevu kwa kila mwanachama wa
CCM, kila kiongozi wa CCM na kila mtumishi wa CCM. Kwa sababu hiyo,
Mradi wa Kuimarisha Chama ni mchakato usiokuwa na ukomo. Ni kazi ya
kudumu na wala siyo tukio lililoanzishwa na Katibu Mkuu Lt. Yusufu
Rajabu Makamba na kukoma siku alipostaafu.
Tuongeze Wanachama
Kazi ya kuingiza wanachama wapya ni ya kudumu katika uhai wa Chama cha
Mapinduzi. Hii siyo kazi ya msimu wa uchaguzi wa ndani ya Chama au
wakati wa kura za maoni na hivyo kugeuzwa kuwa ni kwa ajili ya kuwapigia
debe watu wanaotafuta vyeo. Lazima wakati wote tuwe tunaingiza
wanachama wapya lakini pia lazima tuzingatie utaratibu ulioelekezwa na
Katiba ya CCM. Hatuna budi kuhakikisha kuwa tuna wanachama walio
waumini wa kweli na wapenzi wa dhati wa CCM, itikadi yake na sera zake
na zile za Serikali zake.
Ndugu Wajumbe;
Wanachama
ndiyo nguvu kuu ya uhai na ushindi wa CCM. Lazima Chama chetu kiwe na
Jeshi kubwa la wanachama walio tayari kukijenga, kukisemea na
kukipigania. Kuwa na Wanachama wengi ambao ni waumini wa kweli wa Chama
chetu ina maana ya kuwa na kura nyingi za msingi za kuanzia katika
uchaguzi wa dola. Pia wanachama ni nyenzo muhimu ya CCM kupata kuungwa
mkono na wananchi hasa pale ambapo wanachama wataifanya ipasavyo kazi ya
Chama ndani ya umma. Kila mwanachama akifanya kwa mafanikio kazi ya
kushawishi wananchi kupigia kura wagombea wagombea wa CCM tutapata kura
nyingi za uhakika.
Tuwe na Viongozi Wazuri
Ndugu Wajumbe;
Kazi ya kuhakikisha kuwa Chama cha Mapinduzi kina viongozi wazuri ni ya
kudumu na wala siyo ya msimu wa kuchuja majina ya wagombea. Lazima
Chama chetu kiwe na viongozi ambao ni waumini wa dhati wa itikadi yetu
na wanaozijua vyema sera za Chama cha Mapinduzi na Serikali zake. Wao
ndio wanaotarajiwa kuonesha njia kwa kuelimisha wanachama na wananchi.
Viongozi wa CCM lazima wawe hodari wa kufafanua sera na masuala
mbalimbali yahusuyo Chama chetu na Serikali zake. Hawataweza kufanya
hivyo kama wao wenyewe ni maamuma. Kiongozi mzuri wa Chama cha
Mapinduzi ni yule ambaye ni jasiri kukitetea Chama cha Mapinduzi na kama
hapana budi yuko tayari kujitolea muhanga. Kuwa na kiongozi ambaye
haguswi wala kusikitishwa na hali mbaya ndani ya Chama au hujuma dhidi
ya Chama ni sawa na kutokuwa na kiongozi. Bora asiwepo. Na kuwa na
kiongozi ambaye yeye mwenyewe anafanya vitendo viovu dhidi ya CCM na
Serikali zake ni kuwa na nyoka ndani ya nyumba. Ni jambo hatari
lisilokubalika na halistahili kuvumilika. Tukiwajua tuwaseme,
tuwashughulikie, wachague wanapotaka kwenda.
Ndugu Wajumbe;
Kiongozi
mzuri wa CCM lazima awe muaminifu na muadilifu na lazima wanachama na
jamii imuone hivyo. Chama chetu kinashindania kushinda akili na mioyo
ya Watanzania na hiyo ndiyo kazi tunayomtarajia kiongozi wetu afanye
katika jamii. Hii ndiyo hasa kazi ya Chama ndani ya umma. Lakini, ili
kiongozi wetu aweze kuifanya kwa mafanikio taswira yake mbele ya jamii
ni kitu muhimu. Awe na taswira nzuri mbele ya wananchi. Kama jamii
inamuona kuwa si mtu muadilifu itakuwa taabu sana kwake kufanikisha
jukumu la msingi la Chama chetu. Hivyo ndugu zangu, lazima tuhakikishe
kuwa viongozi wetu wanakuwa waadilifu ili wasigeuke kuwa balaa na hasara
kwa Chama.
Ndugu Wajumbe;
Baada ya kukamilisha mchakato wa uchaguzi ngazi ya taifa, tutatengeneza
na kutekeleza programu maalum ya kutoa mafunzo kwa viongozi wa Chama
kuanzia ngazi ya Tawi hadi Taifa. Hali kadhalika, tutaendeleza na
kukamilisha kazi ya ukarabati na upanuzi wa Chuo cha Ihemi ili kiwe
kitovu cha kutoa mafunzo ya siasa kwa makada na viongozi wa Chama na
Jumuiya zake kama ilivyokuwa inafanywa katika Chuo cha CCM cha Kivukoni
na vyuo vyake vya kanda.
Ndugu Wajumbe;
Bahati
nzuri vyama vya ukombozi vya nchi za Mashariki, Kati na Kusini mwa
Afrika vimekubaliana kuwa Chuo cha Ihemi kiwe Chuo cha Mafunzo ya siasa
kwa makada wa vyama vyao pia. Ni heshima kubwa kwa CCM, lakini pia
inakipa Chama chetu wajibu mkubwa wa kuhakikisha kuwa Chuo hicho
kinawekwa katika viwango vya kimataifa. Tuko tayari na tutajipanga
ipasavyo kutimiza wajibu wetu huo wa kihistoria.
Vikao Vifanyike Ipasavyo
Ndugu Wajumbe;
Ni
kazi endelevu kwetu sote, wanachama na viongozi, kuhakikisha kuwa vikao
vinafanyika kwa wakati na kwamba mikutano inaendeshwa vizuri na ina
agenda zenye maslahi ya kujenga Chama na kuendesha nchi. Pia, ni muhimu
kuhakikisha kuwa kinachoamuliwa kinatekelezwa ipasavyo. Naamini kwamba
mafunzo tutakayotoa kwa viongozi na watendaji wa Chama kuhusu wajibu
wao na jinsi ya kuutekeleza yatasaidia sana kuimarisha CCM.
Watendaji Mahiri
Ndugu Wajumbe;
Kwa
Chama chetu kuwa na watendaji wazuri ni jambo lisilokuwa na mjadala.
Lazima tuwe na watendaji ambao ni makada wazuri na watu mahiri kwa kazi
zao. Wawe ni watu ambao wana uelewa mzuri wa sera za Chama na kwamba
wanaweza kuzifafanua, kuzieneza na kuzitetea. Pia, wawe ni watu
wanaojua vyema kazi yao ya utendaji, kwa mujibu wa shughuli zao
wanazozifanya. Ni vyema kwa kazi za kitaalamu tukapata watu wataalamu
wa kazi hizo. Ni muhimu sana tukayazingatia haya kwani utendaji mzuri
katika Chama ni nguvu muhimu sana ya kukifanya Chama chetu kuwa imara.
Chama chetu kiwe na mipango thabiti ya kuwaendeleza watumishi wake na
kama hapana budi kuwadhamini wakasome. Tufanye hivyo.
Bila
ya shaka mtakumbuka kuwa tarehe 3 Novemba, 2007, pale Kizota, niliahidi
kuwa tutaboresha maslahi ya watumishi wa Chama. Tumetimiza ahadi
hiyo. Leo nasema kuwa tutajitahidi kuendelea kuboresha maslahi ya
watumishi wetu kadri uwezo utakavyoruhusu.
Tujitegemee
Ndugu Wajumbe;
Lazima
Chama chetu kiwe na uwezo wake chenyewe wa kujisimamia na kujiendesha.
Kiwe na fedha za kutosha na vitendea kazi. Hivi sasa hatuko hivyo.
Hatuna budi kuongeza maarifa na juhudi za kukiwezesha Chama cha
Mapinduzi kujitegemea kifedha bila ya kujali kama kuna ruzuku au
hakuna. Jambo hili sasa liwe ni la kufa na kupona kwetu kuhakikisha
linakuwa. Iwe agenda kuu ya Chama katika ngazi zote. Kila mmoja
afikirie nini cha kufanya na kifanywe. Jambo la kuzingatia ni kufanya
shughuli halali. Fursa zipo tuzitumie. Tusikubali kushindwa kwenye
azma kwani hiyo itakuwa maangamizi wa CCM. Lazima tushinde.
Ndugu Wajumbe;
Mtakumbuka
pia kwamba niliahidi kuimarisha usafiri ndani ya Chama. Ahadi hiyo
tumeitimiza. Kila Mkoa na kila Wilaya imepata gari mpya tena gari nzuri
na imara. Gari hizi tukizitunza vizuri zitatuwezesha katika uchaguzi
ujao bila ya taabu. Kwa Mikoa na Wilaya mpya mipango ya kuwapatia
magari iko mbioni. Kila Jumuiya tuliipatia magari yasiyopungua matatu.
Jumuiya za Chama
Ni
wajibu wa kudumu wa Chama chetu kuhakikisha kuwa Jumuiya zake
zinaimarika na kutimiza ipasavyo wajibu wake. Jumuiya ndiyo mkono mrefu
wa Chama cha Mapinduzi kuufikia umma mpana wa Watanzania hasa wale
ambao si wanachama. Jukumu letu ni kuhakikisha kuwa watu hao wanakuwa
wanachama au wapenzi na marafiki wa CCM. Kwa hiyo, kuwepo kwa Jumuiya
ni fursa nzuri kwa Chama cha Mapinduzi kuungwa mkono na watu wengi ili
wakati wa uchaguzi tuweze kupigiwa kura na kupata ushindi. Jumuiya
lazima zihakikishe kuwa zinatimiza ipasavyo wajibu wake ili wasiipotezee
CCM fursa hii adhimu.
Ndugu Wajumbe;
Kwa muhtasari, hayo ndiyo baadhi ya mambo ya msingi ya mradi wa
kuimarisha Chama. Mtakubaliana nami kuwa haya yote ndiyo kazi na wajibu
wa kila mmoja kufanya. Ni kazi endelevu isiyokuwa na ukomo. Tupo kwa
ajili hiyo na rai yangu kwenu ni kuhakikisha kuwa kila mwanachama na
kila kiongozi anatimiza ipasavyo wajibu wake.
Mageuzi Ndani ya Chama
Ndugu Wajumbe;
Kwa dhamira ya kuendelea kukiimarisha zaidi, Chama cha Mapinduzi,
katika mkutano wake wa tarehe 11-12 April, 2011, Halmashauri Kuu ya
Taifa iliamua kuanzisha mchakato na kufanya mageuzi ndani ya Chama.
Lengo kuu la uamuzi huo ni kukiwezesha Chama chetu kuwa na taswira
inayovutia katika mitazamo na hisia za wanachama wake na wananchi.
Kimsingi
NEC inataka tukiwezeshe Chama cha Mapinduzi kiendelee kupendwa na
kuaminiwa na wananchi wote wa Tanzania. Tunataka wanawake na wanaume,
wadogo na wakubwa, maskini na matajiri, wanyonge na wenye nguvu waone
kuwa CCM ndiyo kimbilio lao.
Ndugu Wajumbe;
Kwa ajili hiyo mageuzi ya ndani ya Chama yamejengeka juu ya misingi ifuatayo:-
1. Kukiwezesha Chama cha Mapinduzi kuwa na makada na viongozi mahiri, waadilifu na waaminifu kwa Chama chao;
2. Kukiwezesha Chama kuwa na sera zinazojali maslahi ya wengi na kusukuma mbele kwa kasi maendeleo ya taifa letu;
3. Kukiwezesha Chama kuwa na muundo na mfumo wa uendeshaji ulio nyumbulifu na unaokifanya kuwa karibu na wanachama na wananchi;
4. Kukiwezesha Chama kujitegemea kimapato na kiuchumi ili kiweze kuendesha shughuli zake kwa uhakika, uhuru na heshima;
5. Kukiwezesha Chama kuwa na watu hodari wa kazi na Makada wazuri ambao wanalipwa vizuri na kuwezeshwa kutekeleza majukumu yao;
6. Kukiwezesha Chama kuwasiliana na umma kwa urahisi na kupambana na propaganda chafu za vyama vya siasa; na
7. Kukiwezesha Chama cha Mapinduzi kupambana na maovu ndani ya Chama na katika jamii likiwemo tatizo la rushwa na mengineyo.
Ndugu Wajumbe;
Katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa iliamuliwa kuwa kutokana na
umuhimu wa hoja na haja ya kufanya mageuzi ndani ya Chama utekelezaji wa
mageuzi uanze mara moja. Aidha, pawepo na progamu ya utekelezaji
unayoainisha nini kinafanyika lini na mhusika ni nani! Bila ya shaka
mtakumbuka kuwa katika kikao kile, tuliunda upya Kamati Kuu na kuteua
Sekretarieti mpya. Vile vile iliamuliwa kuwa tufanye marekebisho katika
muundo wa Chama na moja ya matokeo yake ni Wajumbe wa Halmashauri Kuu
ya Taifa kuchaguliwa kutoka wilayani. Nafasi za NEC za mikoa zikafutwa
na zile za taifa zikapunguzwa. Aidha, limeundwa Baraza la Taifa la
Ushauri ambalo wajumbe wake ni viongozi wakuu wa Chama wastaafu.
Wanapata fursa ya kukaa na kutoa ushauri kwa Chama na viongozi wake.
Ndugu Wajumbe;
Tuliamua, pia, kuunganisha chaguzi za Chama na Jumuiya zifanyike mwaka
mmoja. Shabaha ya uamuzi huo ni kutaka kujipa muda wa kutosha wa
kujenga Chama na Jumuiya zake na kujiandaa kwa chaguzi za dola. Uamuzi
huo umeokoa takriban mwaka mzima ambao tulikuwa tunautumia kwa
uchaguzi. Vile vile Halmashauri Kuu ya Taifa iliamua kwamba mgao wa
fedha unatokana na mapato Chama zinazopelekwa kwenye Matawi na Mashina
uongezwe. Lengo ni kuziwezesha ngazi hizi muhimu za Chama kufanya kazi
vizuri zaidi.
Ndugu Wajumbe;
Suala la nidhamu na maadili ya viongozi na wanachama lilisisitizwa sana
kwa sababu ya umuhimu wake kwa taswira ya Chama chetu mbele ya jamii na
wanachama wake. Pia, kutokana na ukweli kwamba ni kilio cha wanachama
na wananchi cha kutaka tuiondowe taswira mbaya dhidi ya Chama iliyopo
katika jamii kuwa ni Chama kisichokerwa na rushwa. Hicho ni kilio cha
dhati kwa watu wenye nia njema na CCM: Chama chao, wanachokipenda na
kukiamini. Chama ambacho bado hakina badala yake wa kuiongoza vyema
nchi yetu na watu wake.
Halmashauri Kuu ya Taifa iliamua mambo mawili yafanyike. La kwanza,
mfumo mzima wa kushughulikia masuala ya usalama na maadili katika Chama
utazamwe upya na uimarishwe. Pili, Chama kichukue hatua na lazima
kionekane kinachukua hatua dhidi ya viongozi na wanachama wasiokuwa
waadilifu na waaminifu wanaofanya sura ya Chama ichafuke mbele ya
jamii. NEC iliagiza wenyewe wajipime na kuamua na wasipofanya hivyo
vikao husika katika Chama vichukue hatua.
Ndugu Wajumbe;
Hayo ni baadhi tu ya mambo muhimu yaliyoamuliwa yafanyike katika
kufanya Mageuzi Ndani ya Chama. Utekelezaji wake umeanza. Yapo
yaliyokamilika na yapo yanayoendelea kutekelezwa. Yapo mambo mengi
ambayo ni endelevu kama vile mapambano dhidi ya rushwa. Hatuna budi
kuendelea kulikemea na kusimama kidete kupambana na tatizo hili mpaka
likomeshwe. Ni kwa maslahi na heshima ya Chama chetu kuendesha
mapambano haya bila ya woga mpaka tushinde. Tukishindwa itakuwa hatari
kwa uhai wa Chama chetu.
Umoja ni Ushindi
Ndugu Wajumbe;
Mara ya mwisho tulipokutana tarehe 11 Julai, 2010, tulikuwa tunajipanga
kwenda kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010. Mliniteua mimi na Dkt.
Mohamed Ghalib Billal kupeperusha bendera ya CCM kwa nafasi ya Rais na
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia tulipitisha
Ilani ya Uchaguzi ya 2010-2015. Siku moja kabla ya Mkutano Mkuu,
Halmashari Kuu ya Taifa ilikuwa imemteua Dkt. Ali Mohamed Shein
kupeperusha bendera yetu kwa nafasi ya Rais wa Zanzibar.
Bahati
nzuri tumepata ushindi kwa nafasi zote hizo za juu za uongozi wa taifa
letu. Pia tulifanikiwa kupata Wabunge na Wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi wengi zaidi kuliko vyama vya upinzani. Kwa sababu hiyo,
tumeunda Serikali zote mbili za nchi yetu na utekelezaji wa Ilani ya
Uchaguzi unaendelea vizuri.
Ndugu Wajumbe;
Kwa upande wa Zanzibar, tuna Serikali ya Umoja wa Kitaifa na mambo
yanakwenda vizuri. Tuzidi kuunga mkono na kuwatakia heri Rais wa
Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Kwanza wa Rais, Mheshimiwa
Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd.
Tunawapongeza sana kwa mafanikio yaliyopatikana. Zanzibar ina amani na
umoja unaozidi kuimarika. Tunatakiwa tuendelee kuiunga mkono Serikali
ya Umoja wa Kitaifa ili ifanikiwe zaidi.
Ndugu Wajumbe;
Uchaguzi uliopita kwa upande wa Tanzania Bara ulikuwa na changamoto
nyingi ambazo hatukuzizoea wala kujiandaa nazo. Zinaelezea matokeo
tuliyoyapata jambo ambalo linatulazimu kuwa makini zaidi katika uchaguzi
ujao. Tusikubali kushtukizwa tena. Lakini, jambo moja lililo dhahiri
ni kwamba umoja na mshikamano miongoni mwa wana-CCM ndiyo uliotuwezesha
kukabili changamoto hizo na kupata ushindi tulioupata. Bila ya hivyo,
mbinu hasi zilizotumika zingetufanya tushindwe.
Napenda
ukweli huu uwepo katika vichwa na mioyo ya wana-CCM na sisi viongozi
wao tuliochaguliwa hivi majuzi na watakaochaguliwa katika Mkutano huu.
Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere alisema: Umoja ni Nguvu, ni kweli kabisa na sisi ni mashahidi. Nami napenda kuongeza kwa kusema kuwa Umoja ni Ushindi.
Ndugu Wajumbe;
Nawaomba wakati wote wa mkutano na baada ya mkutano tukumbuke na
kuzingatia Umoja. Tuishikilie kamba ya Umoja isituponyoke. Tuimbe
Umoja kimoyo moyo na tubainishe wazi wazi kwa kauli na matendo yetu
kuwa: Umoja ni Nguvu Utengano ni Udhaifu! Umoja ni Ushindi! Umoja na Ushindi!. Napenda
kuona kuwa tunatoka hapa tukiwa kitu kimoja, tukiwa watu tunaopendana
na tulioshikamana. Nataka tuondoke katika Mkutano sote tukivuta kamba
upande mmoja badala ya kuvutana. Nataka tuazimie kukabiliana na kauli,
matendo au watu wanaopandikiza chuki na kuhatarisha umoja ndani ya Chama
chetu na miongoni mwetu. Nataka kaulimbiu ya ujumbe wa Mkutano huu
uwe Umoja ni Ushindi! Umoja na Ushindi! Tukiendelea kuwa watu
tunaovutana na kuhasimiana hatutaweza kukijenga Chama chetu wala
kuwatafutia ushindi wagombea wa Chama chetu. Tutakuwa sawa na ule msemo
wa Kiswahili usemao: “vita vya panzi furaha ya kunguru” Tusijigeuze panzi na wala tusikifikishe Chama chetu kiwe hivyo.
Ndugu Wajumbe;
Mtakubaliana nami kuwa harakati za kutafuta uongozi ndani ya Chama au
uteuzi wa kugombea katika chaguzi za dola imekuwa ndiyo chanzo kikuu
kinacholeta mifarakano na kuvuruga umoja ndani ya Chama chetu. Hili
ndugu zangu siyo sawa hata kidogo. Kugombea uongozi ni haki ya msingi
ya mwanachama na raia wa Tanzania. Kwa nini mtu achukiwe au aonekane
adui kwa kuamua kuitumia haki yake hiyo? Kwa nini afanyiwe vitimbi,
vitendo viovu au njama za kuhujumiwa? Nani mwenye haki zaidi ya
mwanachama ama raia mwenzake? Ni ubabe na jeuri ya pesa isiyokuwa na
msingi. Ni ubinafsi na uchu wa madaraka uliopitiliza mipaka. Watu wa
namna hiyo ni hatari sana kwani wanaweza hata kuua au kukivuruga Chama
chetu kizuri kama tamaa zao zisipokidhiwa.
Ndugu Wajumbe;
Napenda kutumia nafasi hii kuwasihi wale wote wanaochukiana kwa sababu
ya kugombea watakafakari upya misimamo yao. Wafanyayo siyo sahihi,
wanaathiri nguvu na uhai wa Chama chetu. Naomba Kamati za Siasa za
ngazi zote ziwatambue watu hao na kuwaita kuwapatanisha. Naomba
wahusika watoe ushirikiano wao. Hata wale wanaohisi kuwa hawakutendewa
haki katika uchaguzi, walidhulimiwa au hata kushindwa kwa sababu ya
vitendo vya rushwa, wakumbuke kuwa Chama chetu kina utaratibu wa
kushughulikia malalamiko yao. Wautumie utaratibu huo badala ya kufanya
vitendo vinavyokigawa na kukivuruga Chama chetu. Kulalamika katika
vyombo vya habari, kufanya ghasia au kuchochea migawanyiko hakutaleta
ufumbuzi.
Ndugu Wajumbe;
Niruhusuni nitumie nafasi hii kuwasihi wale wote wenye tamaa ya
kugombea uteuzi ndani ya Chama wasituulie Chama chetu. Kuwa na tamaa ya
kugombea Urais, Ubunge na Udiwani si kosa ni haki ya mwanachama na ni
haki ya raia wa nchi hii. Jambo ambalo halikubaliki na gumu kulivumilia
ni kufanya vitendo vya kuwagawa wanachama na Chama chetu.
Kuwalazimisha au kuwashinikiza kujiunga na kundi fulani siyo sawa.
Kumchukia mtu kwa sababu naye anagombea au amekataa kukuunga mkono au
kumuunga mkono umpendae ni jambo baya. Unaifanya demokrasia iwe haina
maana au kichekesho. Na, lililo baya kupita kiasi ni kutumia fedha
kushawishi, kuwarubuni au kuwanunua watu kukuunga mkono au kumuunga
mkono mgombea wako au kujiunga na makundi. Hili ni jambo haramu na ni
utovu wa maadili usiokubalika ambao lazima tuukatae, tuukemee na tuupige
vita kwa nguvu zetu zote. Naomba wote tushirikiane katika mapambano
haya kwa heshima ya Chama chetu.
Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi
Ndugu Wajumbe;
Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2010 unakwenda vizuri kwa
Serikali zetu zote mbili. Taarifa zitakazotolewa na Waziri Mku,
Mheshimiwa Mizengo Pinda, kwa upande wa Serikali ya Muungano na Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Balozi Seif Ali Idd kwa upande
wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, zitathibitisha ukweli huu.
Niruhusuni nichukue muda wenu kidogo nizungumzie baadhi ya mambo
yahusuyo shughuli za Serikali.
Nchi Iko Salama
Ndugu Wajumbe;
Napenda kuanza kwa kuwahakikishia kuwa Tanzania iko salama pamoja na
kuwepo matukio ya hapa na pale. Mipaka yetu iko salama. Hakuna tishio
lo lote la kiusalama la kutufanya tuhamanike. Hata mpaka wetu na Malawi
uko salama pamoja na kuwepo kwa maneno maneno yahusuyo nchi zetu mbili
kutofautiana wapi ulipo mpaka halali. Hakuna jambo lo lote linalofanywa
upande wa wenzetu ambalo linatufanya tuwe na mashaka ya usalama wa nchi
yetu kuwa hatarini. Kwa sababu hiyo hatujaiona haja ya kusogeza
Majeshi yetu mpakani na anayesema tumefanya hivyo ni muongo. Apuuzwe na
kushushuliwa.
Ndugu Wajumbe;
Tumeendelea
na juhudi za kuimarisha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kwa
kuwajengea uwezo, zana na vifaa vya kisasa vya kivita. Lengo letu ni
kukuza nguvu ya kimapigano ya Jeshi letu na kuimarisha utayari wake
kivita. Hali kadhalika, tumeendelea kuboresha maslahi ya wanajeshi na
mazingira yao ya kufanyia kazi na ya kuishi. Kwa upande wa usalama wa
raia, yaani maisha na mali zao, matukio ya uhalifu yanaendelea
kupungua. Hali hii inaashiria kuwa Jeshi la Polisi linafanya kazi
nzuri. Kama tufanyavyo kwa JWTZ, tutaendeleza juhudi za kuimarisha
Jeshi la Polisi kwa watu, zana na vifaa vya kisasa vya kufanyia kazi.
Tutaendelea kuboresha maslahi na mazingira ya kufanyia kazi na ya kuishi
ya Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama.
Ndugu Wajumbe;
Pamoja na kutokuwepo kwa tishio lililo dhahiri la shambulio la kigaidi,
wakati wote vyombo vyetu vya ulinzi na usalama viko katika hali ya
tahadhari kuepuka kushtukizwa. Kama mnavyokumbuka mwaka 1998 Ubalozi wa
Marekani hapa nchini ulishambuliwa na ndugu zetu 11 walipoteza maisha.
Hivyo basi, kuchukua tahadhari ni jambo la busara kufanya. Aidha, tuko
katika hali ya tahadhari dhidi ya uharamia wa kuteka meli katika Bahari
Kuu ya Hindi. Takriban mwaka mzima umepita bila ya matukio ya kutekwa
nyara meli katika bahari yetu . Hata hivyo hatuachi kuchukua tahadhari.
Ndugu Wajumbe;
Matukio
ya hivi karibuni ya vurugu zenye mwelekeo wa kidini yanasikitisha na
kusononesha. Ni mambo ambayo hayafanani na sifa ya nchi yetu ya
kuheshimiana na kuvumiliana pamoja na kuwepo tofauti zetu za dini,
kabila rangi au maeneo tutokako. Vitendo hivyo havikubaliki na Serikali
haitawavumilia au kuwaonea muhali wale wote wanaohusika na kuchochea
vurugu hizo. Tumechukua hatua na tutaendelea kuchukua hatua bila ya
ajizi. Ombi langu na wito wangu kwa viongozi na wafuasi wa dini nchini
kuhubiri dini zao huku wakitambua na kuzingatia umuhimu wa kuheshimu
imani za wengine na kuvumiliana. Tusipofanya hivyo nchi yetu tutaingiza
kwenye matatizo yasiyostahili kuwepo.
Ndugu Wajumbe;
Inatia moyo kuona kuwa watu wenye nia njema na nchi yao ni wengi. Kwa
sababu hiyo pamoja na jitihada za baadhi ya watu wasiyoitakia mema nchi
yetu hawajafanikiwa kuwagawa na kuwafarakanisha Watanzania. Nawaomba
Watanzania wenzangu tuwe na moyo huo huo na sisi katika Serikali
tutaendelea kumchukulia hatua mtu ye yote anayetaka kutuvurugia amani na
utulivu wa nchi yetu na watu wake.
Ndugu Wajumbe;
Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali haitamuonea mtu ye yote
asiyehusika. Tutaendelea kuidumisha sifa yetu ya kuendeleza utawala
bora, kuheshimu haki za binadamu na kuzingatia utawala wa sheria.
Kadhalika tutaendelea kuheshimu mgawano wa madaraka miongoni mwa
mihimili mikuu ya dola. Nafurahi kwamba mpaka sasa mambo yanakwenda
vizuri.
Muungano Imara
Ndugu Wajumbe;
Muungano wetu ni imara pamoja na kuwepo vitendo vyenye lengo la
kuudhoofisha vinavyofanywa na baadhi ya viongozi wa siasa na wa dini
hasa kule Zanzibar. Jambo linalosikitisha ni watu hao kutumia njia za
vitisho na ghasia ili kuwalazimisha watu kuwaunga mkono. Njia hizo
hazikubaliki na wala hazitavumiliwa.
Inastaajabisha
mambo hayo kufanyika hivi sasa wakati kuna Tume ya Katiba. Kama mtu
ana maoni yo yote kuhusu Muungano ayafikishe tu, yatapokelewa na
kupimwa. Vile vile Kamati ya Pamoja ya Serikali zote mbili
inayowakutanisha Waziri Mkuu na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
chini ya Uenyekiti wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano imekuwa
inafanya kazi nzuri kutatua kero za Muungano. Kama mtu analo jambo
analotaka lipatiwe jawabu awasilishe kwa wahusika litashughulikiwa.
Hali ya Uchumi
Ndugu Wajumbe;
Katika
Mkutano Mkuu Maalum wa Julai, 2010 hapa Kizota, nilielezea mafanikio
tuliyoyapata na changamoto tulizokumbana nazo katika kukuza uchumi wa
nchi yetu na kupunguza umasikini. Nilieleza pia nia yetu ya kuendelea
kupambana na changamoto zilizokuwa mbele yetu pamoja na ugumu unaotokana
na hali ya kuyumba kwa uchumi wa dunia ambamo na sisi pia tumo. Kwa
ajili hiyo mwaka 2011 tulizindua Mpango wa Maendeleo wa Miaka
Mitano(2011/12 – 2015/16).
Mpango
huu ni wa kwanza kati ya mitatu katika safari yetu ya kutekeleza Dira
ya Maendeleo ya mwaka 2025. Kwa mujibu wa Dira yetu hiyo, tunatarajia
ifikapo mwaka 2025 nchi yetu itaondoka katika kundi la nchi maskini sana
duniani na kuwa nchi ya uchumi wa kati. Yaani tunataka pato la wastani
la Watanzania litoke kwenye dola za Kimarekani 545 za sasa hadi kufikia dola za Kimarekani 3,000.
Lengo hilo ni kubwa linalohitaji mipango thabiti na uwekezaji makini wa
Serikali na sekta binafsi. Pia inahitaji kuwepo kwa nidhamu ya dhati
ya viongozi na wananchi wa Tanzania.
Ndugu Wajumbe;
Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo umekwishaanza. Lengo la jumla katika Mpango wa kwanza ni Kufungulia fursa kwa ukuaji wa uchumi; wa pili ni Ujenzi wa mazingira ya maendeleo ya viwanda; na wa tatu ni Kuimarisha ubunifu na ushindani kimataifa.
Tayari miradi ya kimkakati imekwishaainishwa na inapewa kipaumbele
katika bajeti ya Serikali na ubia baina ya sekta binafsi na sekta ya
umma. Katika kila hatua suala la kukuza ajira limepewa umuhimu mkubwa
kwani lengo letu ni kuwa na ukuaji wa uchumi unaojumuisha maisha ya
watu. Vijana ni walengwa wakubwa.
Mwelekeo
wa uchumi wetu ni mzuri. Kasi ya ukuaji wa uchumi iliyokuwa asilimia
6.4 mwaka wa jana inatarajiwa kufikia asilimia 7 mwaka huu. Mauzo yetu
ya nje yanazidi kukua na kuongezeka. Kwa mfano mwaka 2005 ilikuwa dola
za Kimarekani milioni 2,945.5 na sasa nimilioni 7,461.2. Akiba yetu ya fedha ya kigeni nayo ni nzuri. Hivi sasa ni dola za Kimarekanibilioni 4.1 inatuwezesha kuagiza bidhaa kutoka nje kwa miezi 3.8.
Ndugu Wajumbe;
Changamoto
kubwa katika uchumi ni mfumuko wa bei. Ni kweli umepungua kutoka
asilimia 19.8 Desemba, 2011 hadi asilimia 13.5 Septemba, 2012, hata
hivyo kupungua huko ni kidogo mno. Tunaendelea kuchukua hatua za
kudhibiti na kupunguza zaidi mfumuko wa bei. Kwa vile moja ya sababu ni
kupanda kwa bei za mafuta. Tumeipa dhamana EWURA kusimamia kwa karibu
uagizaji na upangaji wa bei ya mafuta.
Kwa kuwa bei za vyakula hasa mchele na sukari navyo huchangia kupanda
kwa mfumuko wa bei na kuongeza gharama ya maisha mamlaka husika
zimeagizwa kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wanawezeshwa kuagiza bidhaa
hizo kwa wingi kutoka kwa nje kwa kuwapatia nafuu ya baadhi ya kodi.
Pamoja na hayo jawabu la kudumu lipo katika kuendeleza mageuzi ya kilimo
ili nchi yetu ijitosheleze kwa chakula na kupata ziada kubwa ya kuuza
nje. Hayo ndiyo malengo na hatua zinazochukuliwa katika ASDP, Kilimo
Kwanza na SAGCOT. Ndiyo maana tutaendelea kutoa ruzuku ya pembejeo kwa
wakulima, kuimarisha masoko na miundombinu vijijini.
Mapato na Matumizi ya Serikali
Ndugu Wajumbe,
Tunazidi
kupata mafanikio ya kutia moyo kwa upande wa ukusanyaji wa mapato ya
Serikali. Makusanyo ya mapato ya kodi Mwezi Agosti 2012, kwa mfano,
yalifikia shilingi bilioni554.8 ikilinganishwa na
makusanyo ya shilingi bilioni 147 mwezi Desemba 2005. Mafanikio haya
yametokana na juhudi za dhati za Serikali katika kusimamia mabadiliko ya
sera na kuimarisha mifumo na taasisi za ukusanyaji wa mapato ya kodi na
mengineyo.
Kwa sababu ya kuongezeka huko kwa mapato, bajeti ya Serikali nayo imeongezeka kutokashilingi trilioni 4.13 mwaka 2005/06 hadi shilingi trilioni 15.12 mwaka huu. Jambo linaloleta faraja ni kuwa mchango wa Serikali kutokana na bajeti hiyo nao umeongezeka kutoka shilingi trilioni 2.1 mwaka 2005 hadi trilioni 8.8 mwaka huu. Utegemezi wa wahisani nao unaendelea kupungua kutoka asilimia 44 mwaka 2005/6 hadi 21.
Ndugu Wajumbe;
Sambamba
na kuongeza mapato, nidhamu, udhibiti wa matumizi ya fedha na mali za
umma vinazidi kuimarika. Hii ni kutokana na kuimarika kwa mifumo na
kada ya uhasibu katika Serikali Kuu na Serikali za Mitaa. Pia ni
matokeo ya kazi nzuri inayoendelea kufanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu
wa Hesabu za Serikali na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma. Hati
Chafu katika idara za Serikali zinaendelea kupungua katika taarifa ya
ukaguzi kila mwaka. Hivi sasa tunaelekeza nguvu zetu katika kuhakiki
thamani ya fedha zilizotumika na kazi iliyofanyika au huduma
iliyotolewa.
Uwekezaji
Ndugu Wajumbe,
Serikali
imechukua hatua kadhaa kuboresha mazingira ya uwekezaji na ya kufanya
biashara hapa nchini. Lengo letu ni kuvutia wawekezaji wa ndani na nje
kuongeza vitega uchumi nchini na kupanua biashara ndani ya nchi na kati
ya nchi yetu na nchi nyingine duniani. Tunafanya hayo kwa kutambua
ukweli kwamba uchumi unakua na kuongezeka pale ambapo uwekezaji
unaongezeka.
Takwimu
zinaonyesha kwamba uwekezaji umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka
katika sekta ya utalii, viwanda, kilimo, madini, fedha, ujenzi na sasa
kwenye utafutaji wa gesi na mafuta. Tumepata mafanikio makubwa
katika utafutaji wa gesi na nchi yetu itakuwa moja ya mzalishaji mkubwa
wa gesi. Mwaka 2011, kwa mfano, kulikuwa na jumla ya miradi 826yenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 7,177 itakayozalisha ajira ya watu 79,000. Haya ni mafanikio madogo lakini tunaweza kufanya vizuri zaidi.
Tutaendelea kutumia
fursa ya kijiografia ya nchi yetu kuvutia uwekezaji na kuifanya
Tanzania kuwa lango kuu la biashara na usafirishaji kwa nchi za Afrika
ya Mashariki na Kati. Ili kufanikisha hayo, tutaendelea kuboresha
miundombinu ya barabara, reli, bandari, viwanja vya ndege na teknohama.
Miundombinu
Ndugu wajumbe;
Moja ya vipaumbele vya juu vya Serikali ya CCM ninayoiongoza ni
kuboresha miundombinu ya usafiri wa ardhini, majini na angani nchini.
Tumethibitisha hayo kwa mgao wa fedha za bajeti ya Serikali ambapo
miundombinu ni ya pili baada ya elimu. Mwaka huu nishilingi trilioni 2.4, ambayo ni asilimia 16 ya bajeti ya Serikali ukilinganisha na elimu yenyetrilioni 3.6 ambayo ni sawa na asilimia 24, na afya yenye shilingi trilioni 1.5 sawa na asilimia 10ya
bajeti ya Serikali. Tunafanya hivyo kwa kutambua mchango muhimu wa
sekta ya usafiri kwa maendeleo ya nchi yetu na watu wake. Usafiri
unapokuwa bora na wa uhakika, gharama za usafirishaji zinapungua,
shughuli za uzalishaji viwandani na kilimo zinaimarika. Ni kichocheo
kikubwa cha kuibuka kwa fursa mbalimbali za uchumi na kuongeza kasi ya
maendeleo na kukuza kipato cha Watanzania waliopo mijini na vijijini.
Ndugu Wajumbe;
Tunafanya uwekezaji mkubwa katika ujenzi wa barabara kuliko wakati
mwingine wo wote katika historia ya nchi yetu. Hivi sasa barabara
zenye urefu wa kilometa 11,154 zinajengwa kwa kiwango cha lami
katika sehemu mbalimbali nchini. Tulijipa lengo la kuunganisha mikoa
yote kwa barabara za lami na barabara zote kuu ziwe za lami.
Nafurahi
kusema kuwa utekelezaji wake unakwenda vizuri. Tumeanza kufanikiwa
kuifikia ile mikoa ambayo kwa muda mrefu ilikuwa haifikiki kwa urahisi
kwa kukosa barabara za lami. Katika hotuba yangu ya tarehe 25 Juni,
2006 niliwaambia Wajumbe wa Mikoa ya Ruvuma, Rukwa, Mtwara, Kigoma na
Tabora kuwa kilio chao tumekisikia. Niliahidi kuwa ujenzi wa barabara
katika Mikoa hiyo tutaipa kipaumbele. Tumetimiza ahadi hiyo na kazi
inaendelea kwa kasi na hata wenyewe ni mashahidi. Karibu tunafikia
ndoto yetu ya kwamba hakuna mkoa utakaoachwa nyuma.
Ndugu Wajumbe;
Inafurahisha zaidi kuona kuwa zaidi ya asilimia 60 ya
gharama za ujenzi wa barabara tunazojenga nchini ni fedha zetu wenyewe.
Aidha, uwezo wa Mfuko wa Barabara (Road Fund) nao umeongezeka sana
kutoka shilingi bilioni 58 mwaka 2005 hadi shillingi bilioni 430.
Hali hiyo imeongeza uwezo wetu wa kujenga na kukarabati barabara
mbalimbali nchini. Kwa ajili hiyo tumeongeza bajeti ya barabara kwenye
Halmashauri zote nchini.
Ndugu Wajumbe;
Pamoja
na barabara, tunaendelea kuimarisha viwanja vya ndege, bandari na
usafiri wa reli. Changamoto mbalimbali zinajitokeza katika
utekelezaji wa lengo letu na kubwa zaidi ikiwa ni ile ya gharama za
ujenzi na ukarabati wa miundombinu kuwa kubwa mno ikilinganishwa na
uwezo wetu. Tunaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuzikabili changamoto
hizo hatua kwa hatua na tunazipunguza.
Elimu
Ndugu wajumbe;
Tumefanikiwa
kupanua sana fursa za kuwapatia elimu vijana wetu katika ngazi zote.
Kuna watoto wengi katika elimu ya awali, na kwa elimu ya msingi asilimia 97 ya watoto wenye umri wa kwenda shule wamejiandikisha. Kwa kiwango hicho, tuko mahali pazuri kufikia asilimia 100ifikapo
mwaka 2015 kama ilvyoagiwa katika Malengo ya Milenia ya Umoja wa
Mataifa. Kuhusu elimu ya Sekondari, wananchi na wadau wengine wameitikia
wito wa Serikali wa kila Kata kuwa na shule ya sekondari. Kwa sababu
hiyo idadi ya shule 3,165 zimejengwa kati ya 2005 na hivi sasa na idadi ya wanafunzi katika shule za sekondari imeongezeka kutoka 524,325 mwaka 2005 hadi 1,884,272 mwaka huu.
Tumepanua sana mafunzo ya ufundi na elimu ya juu. Hivi sasa nchi yetu ina vyuo vikuu27 na wanafunzi waliopo vyuoni humo ni zaidi ya 166,484 ikilinganishwa na 40,719 wa
mwaka 2005. Ili kutoa fursa sawa kwa wanafunzi wote tumeongeza sana
uwezo wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ili iwape wanafunzi wengi
mikopo ya elimu. Bajeti ya Bodi hiyo imeongezeka kutoka shilingi
bilioni 56.1 mwaka 2005 hadi shilingi bilioni 306.0 mwaka huu. Wanafunzi wanaopata mikopo wapo 93,176 ukilinganisha na 16,345 mwaka 2005. Tutaendelea kuongeza fedha ili tuwafikie wanafunzi wengi kadri inavyowezekana.
Ndugu Wajumbe;
Upanuzi
mkubwa wa elimu katika ngazi zote nchini umezua changamoto mbalimbali
kuhusu ubora wa elimu. Tunazitambua changamoto hizo kuwa ni pamoja na
zile za upungufu wa walimu, hususan wa sayansi; upungufu wa vifaa vya
maabara, vitabu na nyumba za walimu hasa kwenye maeneo ya vijijini.
Tumejipanga vyema kuzitafutia ufumbuzi na tumeanza kufanya hivyo.
Tumeongeza vyuo vinavyotoa mafunzo ya ualimu ili kuongeza idadi ya
waalimu. Bajeti ya elimu ni kubwa kuliko zote ili kusaidia kutatua
tatizo la upungufu wa vitabu, maabara, vifaa vya kufundishia na nyumba
za walimu na mahitaji mengineyo. Hivi karibuni nilipokuwa Mkoani
Singida nimewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya zote nchini kuhakikisha
kuwa shule zote za sekondari katika maeneo yao zinakuwa na maabara ya
sayansi katika miaka miwili ijayo.
Afya
Ndugu wajumbe;
Suala la afya ya Watanzania tunalipa umuhimu mkubwa sana. Tumeongeza bajeti ya afya kutoka shilingi bilioni 271 mwaka 2005 hadi shilingi trilioni 1.5 mwaka
huu. Nyongeza hii ndiyo iliyotuwezesha kutekeleza Sera mpya ya Afya
(2007) na Mpango wa Miaka Kumi wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM) wa
kuitekeleza vyema Sera hiyo. Lengo kuu la sera na MMAM ni kuwapatia
Watanzania huduma ya afya iliyo bora katika umbali usiozidi kilometa
tano. Vile vile, ni kuimarisha huduma zinazotolewa katika hospitali za
Wilaya, Mikoa, Kanda na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Katika
mpango huu pia tumeazimia kukabili tatizo la upungufu wa madaktari,
wauguzi na wataalamu wengi. Tunaendelea kupanua mafunzo ya wataalamu
hao katika vyuo vyetu hapa nchini na hata nje ya nchi. Tumejenga na
tutaendelea kujenga vyuo vipya, wakati huo huo tukipanua vilivyopo.
Tumeendelea kujenga uwezo wa kupambana na maradhi makubwa yanayoua watu
wengi. Tumeelekeza nguvu zetu kwenye maradhi yanayoambukiza kama vile
malaria, UKIMWI na kifua kikuu na yale yasiyoambukiza kama vile
saratani, moyo, shinikizo la damu na vifo vya kina mama wajawazito na
watoto chini ya umri wa miaka mitano.
Ndugu Wajumbe;
Kwa maradhi yote mafanikio ya dhahiri yanaendelea kupatikana. Maambukizi ya virusi vya UKIMWI yanapungua kutoka asilimia 8 hadi asilimia 5.7, vifo kutokana na malaria vimepungua kwa asilimia 40 kwa
Tanzania Bara na kwa Zanzibar tunakaribia kutangaza kufutika kwa
maradhi hayo. Tumepanua uwezo wa kutibu maradhi ya moyo ikiwa ni pamoja
na kufanya upasuaji wa moyo. Tumepanua uwezo wa kuchunguza na kutibu
maradhi ya kansa. Tunaendelea kujenga uwezo wa ndani kwa maradhi
tunayopeleka wagonjwa wengi nje na mafanikio yanaaza kuonekana. Safari
ni hatua, naamini tutafika kwani mwelekeo wetu ni mzuri.
Umeme na Maji
Ndugu wajumbe;
Tunaendelea
kupanua uwezo wetu wa kuzalisha na kusambaza umeme nchini. Tumeanza
safari ya uhakika ya kupunguza kutegemea mno umeme wa nguvu ya maji.
Tunapanua umeme utokanao na vyanzo vingine hasa gesi asilia na makaa ya
mawe. Mipango ya kutumia upepo na mionzi ya jua nayo iko mbioni.
Pamoja na hayo tunayo mikakati ya kupunguza umeme unaozalishwa kwa
kutumia mafuta kwa kubadili mitambo hiyo iweze kutumia gesi asilia.
Hivi
majuzi tu nilizindua ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es
Salaam. Litakapokamilika nchi yetu itakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 3,000 na
kuung’oa mzizi wa fitina wa mgao na upungufu wa umeme nchini.
Tumeendelea kuwekeza katika usambazaji wa umeme nchini jambo ambalo
limetuwezesha kuwapatia umeme kwa asilimia 18.4 Watanzania kutoka asilimia 10 mwaka 2005. Kwa kasi hii naamini tutafikia lengo la asilimia 30 ifikapo 2015.
Kwa
upande wa maji, jitihada za kuwapatia wananchi maji safi na salama
zinaendelea vizuri. Eneo hili lina changamoto kuu mbili. Kwanza ni ule
ukweli kwamba kuna baadhi ya maeneo ya nchi yetu hayana vyanzo vya maji
karibu au hayapati mvua za kutosha au yana ukame. Katika maeneo ya aina
hii upatikanaji wa maji huwa wa shida sana na hivyo kutulazimisha
kujenga miradi ya maji ya bomba kutoka masafa marefu. Changamoto yetu
ya pili ni ule uwezo mdogo wa kifedha kwa miradi mingi inayohitaji pesa
nyingi. Mwaka 2006 tulianzisha Programu ya Maendeleo ya Sekta ya
Maji.
Kufuatia utekelezaji ulio makini wa programu ya sekta ya maji,asilimia 60 ya watu wa vijijini na asilimia 86 ya watu wa mijini wanaopata maji safi na salama. Ni matumaini yangu kuwa tutafikia lengo letu la asilimia 65 la upatikanaji maji kwa vijijini naasilimia 90 kwa
mijini ifikapo 2015. Bahati nzuri tunayo miradi ya maji inayoendelea
kutekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini na itapokamilika tutafikia
lengo letu au hata kulivuka.
Pongezi kwa Kuchaguliwa
Ndugu Wajumbe;
Katika Mkutano huu, Ndugu Amani Abeid Karume, Makamu Mwenyekiti wa
Zanzibar na Ndugu Pius Msekwa, Makamu wa Mwenyekiti wa CCM kwa upande wa
Tanzania Bara watastaafu. Ndiyo maana NEC imeamua kuwapendekeza kwenu
Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi na Ndugu Philip Mangula kuchukua nafasi zao. Napenda kuchukua
nafasi hii kwashukuru kwa dhati Rais Amani Abeid Karume na Mzee Msekwa
kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya kunisaidia kuongoza Chama chetu.
Wamekifanyia
Chama chetu mambo mengi mazuri ambayo hatuna budi kuwapongeza na
kuwashukuru. Waliendelea kuwa walimu wangu na washauri wangu kwa mambo
mengi ya Chama na nchi. Nawashukuru sana. Sote tuwatakie afya njema na
maisha marefu. Na tumuombe Mzee Msekwa asichoke kuandika vitabu ili
hazina yake kubwa ya uzoefu na maarifa iwanufaishe wengi kwa miaka mingi
ijayo.
Kwa
viongozi wa Mikoa, Wilaya na Jumuiya pamoja na Wajumbe, nirudie
kuwapongeza nyote kwa kuchaguliwa kwenu. Poleni kwa magumu ya uchaguzi
mliyokumbana nayo. Sasa uchaguzi umeisha, fanyeni kazi ya kujenga
Chama. Tibuni majeraha ya uchaguzi na hasa fanyeni kila muwezalo kuziba
nyufa za uchaguzi na migawanyiko miongoni mwa wanachama na viongozi.
Kumbukeni wosia wa Baba wa Taifa “Umoja ni Nguvu” Kumbukeni kaulimbiu ya Mkutano wetu huu ya Umoja ni Ushindi! Umoja na Ushindi! Kajengeni umoja katika maeneo yenu ya uongozi kwa maslahi ya Chama chetu na nchi yetu.
Hitimisho
Ndugu Wana-CCM;
Kwa kuhitimisha naomba nirudie kusema kuwa tumepata mafanikio ya kutia
moyo katika ujenzi wa Chama na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM
ya mwaka 2010 – 2015. Bado kazi kubwa iko mbele yetu kwa mambo yote
hayo mawili. Tunaitambua na tunayo mipango thabiti ya kutekeleza
majukumu yetu. Nina imani tutafanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kufikia
malengo yetu. Tukiendelea kushirikiana tutafika. Umoja ni Ushindi! Umoja na Ushindi!
Baada ya hotuba yangu naomba sasa nitamke kuwa Mkutano Mkuu wa Nane wa CCM umefunguliwa rasmi.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Kidumu Chama cha Mapinduzi
Asanteni sana kwa Kunisikiliza
0 comments:
Post a Comment