Pichani ni
Naibu Balozi wa Ubalozi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa,
Ramadhan M. Mwinyi, akizungumza wakati wa majadiliano kuhusu ajenda ya
Umalizaji Ukoloni, katika Mkutano wa Kamati ya Nne ya Baraza Kuu la 67
la Umoja wa Mataifa, Kamati hiyo ambayo ni maalum inajihusika na Masuala
ya Siasa na Umalizaji wa Ukoloni
*******
Na Mwandishi Maalum.
Balozi
Ramadhan Muombwa Mwinyi, Naibu Balozi katika Ubalozi wa Kudumu wa
Tanzania katika Umoja wa Mataifa, akizungumza wakati wa mkutano wa
Kamati ya Nne ya Baraza Kuu la 67 la Umoja wa Mataifa. Kamati hiyo ni
Kamati Maalum inayohusika na masuala ya Siasa na umalizaji wa Ukoloni
na kwa wiki nzima imekuwa ikijadili ajenda zinazohusiana na suala zima
la umalizaji wa Ukoloni kama inavyoelekezwa katika Katiba ya Umoja wa
Mataifa na Maazimio mengine mbalimbali.
Hadi sasa
kuna makoloni 16 ambayo bado yapo chini ya Ukoloni na hayajawa huru
kujiamulia mambo yake yenyewe. Baadhi ya Makoloni hayo ni Sahara ya
Magharibi ambayo ni koloni pekee lililobaki Barani Afrika.
Kwa
zaidi ya miaka 57 Sahara ya Magharibi ambayo imejitangaza kujitenga
kutoka Morocco imekuwa katika mgogoro mkubwa na serikali ya Morocco.
Mgogoro ambao umesababisha wananchi wengi kupoteza maisha, wengine
kuishia kuwa wakimbizi huku zikiwamo shutuma za ukiukwaji mkubwa wa haki
za binadamu.
Aidha
Kamati hiyo ilipata fursa ya kuwasilikiliza Wadai (Petitioners)
68 ambao ama walikuwa wakitetea haki ya Sahara Magharibi kujipatia
uhuru wake na fursa ya kujiamulia mambo yao au walikuwa wakiitetea
Morocco dhidi ya Sahara Magharibi.
Akichangia
maoni ya Tanzania katika mkutano huo, Naibu Balozi Ramadhan
Muombwa Mwinyi pamoja na mambo mengine amesisitiza haja na umuhimu wa
Serikali ya Morocco na POLISALIO kuendelea na mazungumuzo ya kutafuta
suluhu ya kudumu na kubwa zaidi ni kwa Morocco kuiachia Sahara
Magharibi ijitawale na kujiamulia mambo yake yenyewe.
Aidha
Tanzania kupitia msemaji wake huyo imeungana na mataifa mengine ambayo
yalizungumzia kwa kina haki na uhuru wa Sahara ya Magharibi huku
ikitoa wito kwa Morocco kujiunga tena na Umoja wa Afrika (AU) kama njia
moja wapo itakayosaidia kuutafutia ufumbuzi mgogoro huo.
Aidha
Tanzania kama ilivyokuwa kwa nchi nyingine imempongeza na kumtia
shime Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon na mshauri wake katika
suala la Sahara ya Magharibi Balozi Christopher Ross, kuendelea na
juhudi zao za kuhakikisha kwamba mazungumao kati ya pande hizo mbili
yanaendelea kufanyika kwa njia ya uwazi, kuaminiana na kwa kuzingatia
Katiba ya Umoja wa Mataifa na maazimio mengine yahusuyo suala la
Sahara ya Magharibi.
Tanzania
pia imezitaka nchi zile ambazo zinaendelea kuyashikilia makoloni
kuonyesha utashi wa kisiasa na kushirikiana na Kamati hiyo maalum ili
kufikia muafaka kuhusu makoloni hayo 16 ambayo bado yanaendelea
kutawaliwa.
Mbali ya
Sahara Magharibi, makoloni mengine ni Falkland Islands/Malvinas koloni
linalogombewa kati ya Uingereza na Argentina, Gibraltar ambalo pia
linagombewa kati ya Uingereza na Spain, New Caledonia, America Samoa,
Anguilla, Bermuda, British Virgin Islands, Cayman Islands, Guam,
Montserrat, Pitcairn, Saint Helena, Turks and Caicos Islands, United
States Virgin Islands, na Tokelau. Baadhi ya makoloni hayo
yanashikiliwa na Marekani.
0 comments:
Post a Comment