Nafasi Ya Matangazo

October 18, 2012

Baadhi ya wanariadha wakishiriki katika mbio za Rock City (Picha kutoka Maktaba)
 
 Na Mwandishi Wetu
NCHI tisa zinatarajiwa kushiriki katika mbio za kilomita 21 za mwaka huu za Rock City Marathon zinazotarajiwa kufanyika Oktoba 28 katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Mratibu wa mbio hizo Bi. Grace Sanga kutoka kampuni ya Capital Plus International (CPI), waandaji wa mbio hizo za kila mwaka alisema kuwa mialiko katika mbio hizo imeongezwa na wanariadha kutoka Afrika Mashariki na nchi nyingine za ulaya wanatarajiwa kushiriki.

Alitaja nchi hizo kuwa ni Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Demokrasia ya Watu wa Kongo (DRC) na nchi nyingine za ulaya kama Australia, India, Canada na Marekani ambapo aliongeza kuwa wanatarajia namba ya washiriki kuongezeka kwa mwaka huu kutokana na maandilizi mazuri.

“Tumejitahidi kutuma mialiko ya kushiriki kwa wadau wote wa riadha katika nchi jirani ili wapate kushiriki mbio za Rock City na tunategemea kupata washiriki wengi zaidi kutoka nje ya nchi tukilinganisha na mwaka uliopita. Hii inaonyesha maandalizi ya mbio kuboreshwa zaidi na hivyo kuongeza ushindani katika mchezo,” alisema Grace.

Mbio hizo za kila mwaka zimegawanyishwa katika makundi matano, ambapo kutakuwa na mbio za kilomita 21 kwa wanawake na wanaume, kilomita tano kwa watu wote, kilomita tatu kwa watu wenye ulemavu, kilomita tatu kwa wazee (miaka 55 na kuendelea) na kilomita mbili kwa watoto umri kati ya miaka saba mpaka kumi.  

Bi. Sanga alisema kuwa mbio hizo zinazoonyesha mafanikio makubwa toka zizinduliwe mwaka 2009, zinalenga kukuza utalii wa ndani kupitia michezo kama kauli mbiu yake inavyosema ‘tukuze utalii wa ndani kupitia michezo’.

“Jiji la Mwanza ni tajiri sana katika vivutio vya utalii na tumelenga kumpitia mbio hizi kuvitangaza vivutio hivyo. Mbio za kilomita 21 zitaanza katika uwanja wa CCM Kirumba na kupita njia tofauti tofauti na kurudi CCM Kirumba”, alisema.

Alitaja wadhamini wa mbio hizo kuwa ni Mfuko wa Hifadhi ya Taifa ya Jamii (NSSF), Airtel Tanzania, Geita Gold Mine, Shirika la Ndege la Air Tanzania, Parastal Pension Fund (PPF), African Barrick Gold, New Africa Hotel, Nyanza Bottles, New Mwanza Hotel, TANAPA na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB).  

Grace aliongeza kuwa washiriki na washabiki wa mbio za Rock City za mwaka huu watapata fursa ya kumshuhudia msanii maarufu wa Tanzania Juma Nature a.k.a Sir Nature na kundi lake la TMK Wanaume wakitumbuiza wakati wa mbio hizo.            

Alisema pia pesa itakayopatikana ikitokana na ada ya usajili toka kwa washiriki moja kwa moja itapelekwa katika mfuko wa msaada kwa watu wenye ulemavu waishio jijini Mwanza.   

Fomu za usajili za mbio hizo zinapatikana katika uwanja wa Nyamagana Jijini Mwanza, Ofisi za Kampuni ya Capital Plus International Ltd zilizopo jengo la ATC ghorofa ya tatu, na pia zinapatikana katika blog ya rockcitymarathon.blogspot.com.

Posted by MROKI On Thursday, October 18, 2012 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo