NA MAGRETH KINABO – MAELEZO
KAMATI ya Bunge inayoshughulikia masuala
ya Ukimwi imeishauri serikali kutoa tamko la kuelezea ni hatua gani inaendelea
kuchukua baada ya kusimamisha kazi baadhi ya viongozi wa Bohari Kuu ya Dawa
(MSD) kufuatia kuwepo kwa dawa bandia za kupunguza makali ya Ukimwi( ARV)
katika kikao cha Bunge kitakachoanza mwishoni mwezi huu.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mwenyekiti
wa kamati hiyo, Lediana Mng’ong’o wakati akizungumza na waandishi wa habari
kwenye ofisi ndogo za Bunge jijini Dares Salaam kuhusu kuwepo kwa dawa hizo.
“Sisi tungependa kuishauri serikali
kuendelea kufuatilia na hatua za kisheria pale itakapobaini katika uchunguzi
huo ili tatizo hili lisiendelee kutokea,” alisema Lediana ambaye ni Mbunge wa
Viti Maalum Iringa.
Aliongeza kuwa wanaishauri Mamlaka cha
Chakula na Dawa (TFDA) kuwa na wawakilishi katika kanda mbalimbali ili kuweza
kudhibiti tatizo la kuwepo kwa dawa bandia.
Aidha kamati hiyo imelaani kampuni
ambayo imeingiza dawa feki na imetaka hatua za kisheria zichukuliwe.
Kamati hiyo imewataka watu wanaotumia
dawa hizo kutoziacha , bali waendelee kuzitumia kwa kuwa dawa zote si feki na
pia zipo za kutosha.
0 comments:
Post a Comment