Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) mkoa wa Rukwa imetoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kuwa na utaratibu wa kupima ubora wa vifaa wanavyovitumia katika ujenzi kupitia maabara ya Wakala huo ili kuhakikisha wanajenga miundombinu imara, salama na yenye kudumu kwa muda mrefu.
Wito huo umetolewa na Bw. Adamu Samaya, Fundi Sanifu katika Ofisi ya Meneja wa TARURA mkoa wa Rukwa katika Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa 2026 yanayoendelea katika viwanja vya shule ya Msingi Ndua Manispaa ya Sumbawanga.
Bw. Samaya amesema kuwa upimaji wa vifaa vya ujenzi ni hatua muhimu inayopaswa kupewa kipaumbele kabla ya kuanza kwa shughuli za ujenzi kwa kuwa husaidia kubaini iwapo vifaa husika vinakidhi viwango vya ubora vinavyohitajika.
"Ubora wa vifaa hauwezi kuujua kwa kuangalia kwa macho tu, ili kujua ubora wake ni lazima vifanyike vipimo maabara na kupata matokeo yatakayokuwezesha kufanya uamuzi sahihi", amefafanua Bw. Samaya.
Amesema matumizi ya vifaa vilivyopimwa na kuthibitishwa kuwa na ubora unaotakiwa husaidia kupunguza hatari ya uharibifu wa mapema wa miundombinu, kuepusha gharama za matengenezo zinazoweza kuzuilika na kuongeza thamani ya fedha zinazowekezwa katika miradi ya ujenzi.
Akizungumzia mwitikio wa wananchi katika kutumia huduma za maabara hiyo, Bw. Samaya amesema kuwa mwitikio ni mzuri licha ya maabara hiyo kuanza kutoa huduma mwezi Desemba 2025.
Ameongeza kuwa kwa sasa Makandarasi wote waliopata zabuni za kutekeleza miradi ya TARURA wanaitumia maabara hiyo kupima vifaa vyao vya ujenzi hatua inayochangia kuimarisha usimamizi na udhibiti wa ubora wa miradi inayotekelezwa.
Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa 2026 yanaendelea katika viwanja vya shule ya Msingi Ndua Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa ambayo yatafuatiwa na sherehe za Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru zitakazofanyika katika uwanja wa Nelson Mandela tarehe 14 Oktoba 2026 tukio litakaloongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.










0 comments:
Post a Comment