Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom
Tanzania imesema suala la kuwepo kwa kipengele cha Upekee “EXCLUSIVITY” katika mkataba wa
udhamini wa ligi kuu soka Tanzania bara kati ya kampuni hiyo na shirikisho la
soka nchini - TFF ni la muhimu katika kuepuka migongano ya kimasilahi ya
kibiashara miongoni mwa wadhamini.
Mkuu wa Udhamini na Mawasiliano
wa kampuni ya Vodacom Tanzania Bw Kelvin Twissa amesema kampuni ya Vodacom inajali
na kuthamini maendeleo ya vilabu nchini na kwamba itaendelea kufanya hivyo kwa
kutoa fursa zaidi zinazolenga kukuza kiwango cha uwekezaji katika soka kwa masilahi
ya vilabu na taifa kwa ujumla.
Twissa amesema katika kutambua
umuhimu wa kupanua wigo wa uwekezazi katika ligi kuu ya Vodacom na maendeleo ya
vilabu kwa ujumla, kampuni ya Vodacom Tanzania ilikubali kwa moyo mkunjufu
kuruhusu vilabu kutafuta wadhamini wengine ambao siyo makampuni yanayofanya
baishara sawa na Vodacom.
Twissa alikuwa akizungumza katika
kikao cha pamoja kilichowakutanisha Shirikisho la Soka Tanzania – TFF, Kamati
ya Ligi Kuu na Mdhamini Mkuu kampuni ya Vodacom Tanzania kilichoketi jana jijini Dar es salaam.
“Tunatambua na kuheshimu utayari
wa makampuni mengine ambayo yapo tayari kushirikiana na sisi katika kudhamini Ligi
kuu ya Vodacom nasi tupo tayari kushirikiana nao na hivyo kuleta maendeleo ya mpira wa miguu nchini”Alisema
Twissa
“Vodacom Tanzania inajivunia kuwa
wadhamini wakuu wa ligi hii,tumeamua kuboresha udhamini wetu kwa sababu
tunatambua umuhimu wa michezo kwa Taifa letu, sasa michezo si kwa ajili ya
burudani tu bali imekuwa chanzo cha ajira na kuboresha maisha ya wanaojihusisha
nayo,” Aliongeza Twissa.
“Tunaviomba vilabu vinavyoshiriki ligi kuu, vyombo vya habari na
umma kwa ujumla kutambua kuwa azma ya Vodacom ni kuona mpira wa miguu unasonga
mbele zaidi na ndio maana tumekuwa katika udhamni huu kwa zaidi ya miaka saba
tukipitia vipindi tofauti lakini hatukuwahi kukata tamaa. Hivyo si vyema wakati
huu soka yetu inapokua tukaruhusu hali inayoweza kusababisha changamoto katika
uwekezaji wa soka.” Aliongeza Twisa.
Twissa
amesema kampuni ya Vodacom itaendelea kushirikiana na TFF, Kamati ya Ligi na
wadau wengine wote wa mpira wa miguu nchini katika kukuza uwekezaji kwa
kusaidia vilabu kupata wadhamini watakaosaidia maendeleo ya vilabu hivyo.
0 comments:
Post a Comment