Nafasi Ya Matangazo

June 20, 2012

 Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Mstaafu Joseph Warioba akizungumza na Waandishi wa Habari katika ukumbi wa Salama, Hoteli ya Bwawani, Zanzibar leo (Jumatano, Juni 20, 2012). Kulia kwake ni Makamu Mwenyekiti Jaji Mkuu Mstaafu Agustino Ramadhani na kushoto ni Katibu wa Tume Rashid Assaa na Naibu Katibu Casmir Kyuki.
 Baadhi ya Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba wakifuatilia maelezo ya Mwenyekiti wa Tume Jaji Mstaafu Joseph Warioba wakati akizungumza na Waandishi wa Habari katika ukumbi wa Salama, Hoteli ya Bwawani, Zanzibar leo (Jumatano, Juni 20, 2012).
Baadhi ya waandishi wa habari wakifuatilia mkutano kati ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Mstaafu Joseph Warioba akizungumza na Waandishi wa Habari katika ukumbi wa Salama, Hoteli ya Bwawani, Zanzibar leo (Jumatano, Juni 20, 2012).

Na Omega Ngole, Zanzibar

Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Mstaafu Joseph Warioba leo (Jumatano, Juni 20, 2012) amefanya mkutano wa pili na wanahabari mjini Zanzibar na kusisitiza umuhimu wa wananchi kutoa maoni kwa uhuru na uwazi kuhusu Katiba mpya.

Akizungumza katika ukumbi wa Salama, Hoteli ya Bwawani, Jaji Warioba amesema ingawa Tume itaanza kukusanya maoni katika mikoa nane hivi karibuni, tayari Tume hiyo imeanza kupata maoni kuhusu masuala mbalimbali likiwemo suala la mamlaka ya wananchi.

Katika wa leo na ule uliofanyika jana (Jumanne, Juni 19, 2012) jijini Dar es Salaam, Jaji Warioba amesisitiza umuhimu wa vyombo wa habari kushiriki kikamilifu katika kuwaelimisha wananchi kuhusu mchakato wa kupata Katiba mpya unaoendelea na kuahidi kuvipa ushirikiano vyombo vya habari.

“Katiba ya sasa inaeleza kwamba wananchi ndio msingi wa mamlaka yote na msukumo mkubwa wa mchakato huu wa kupata Katiba Mpya ni matakwa ya kuwawezesha wananchi kutunga Katiba yao. Lakini kuna watu wanasema mamlaka ya wananchi hayakufafanuliwa,” alisema katika mkutano huo uliohiudhuriwa pia na wajumbe wengine wa Tume na kuongeza:

Jaji Warioba aliongeza kuwa wananchi hao wanasema kuwa mamlaka ya taasisi za dola kama vile Serikali, Bunge, Mahakama, Tume mbali mbali za kikatiba, na hata Vyama vya Siasa, yamefafanuliwa, hali ambayo ni tofauti na mamlaka ya wananchi.

“Tume ingependa kupata maoni ya wananchi kuhusu eneo hili,” alisisitiza Mwenyekiti huyo na kuyataja maeneo mengine ambayo Tume ingependa kupata maoni ya wananchi kuwa ni malengo muhimu na misingi ya mwelekeo wa shughuli za Serikali ambayo alisema yameeelezwa vizuri sana katika Ibara ya 9 ya Katiba.

Aliyataja maeneo hayo kuwa ni kuheshimu na kuthamini utu na haki nyinginezo zote za binadamu; utekelezaji wa shughuli za Serikali kwa njia ambazo zitahakikisha kwamba utajiri wa Taifa unaendelezwa, unahifadhiwa na unatumiwa kwa manufaa ya wananchi wote kwa jumla na pia kuzuia mtu kumnyonya mtu mwingine.

Kwa mujibu wa Jaji Warioba, eneo jingine ni ulinzi wa haki za binadamu na wajibu kwa jamii ana kusema kuwa ingawa Sehemu ya Tatu ya Sura ya Kwanza ya Katiba ina orodha ndefu ya haki na wajibu muhimu kwa raia, baadhi ya wananchi wanasema wanasema haki hizi hazitoshi na wengine wanasema haki za mtu binafsi zinadhulumu haki za jamii.

Wakitoa maoni yao katika mkutano huo, waandishi wa habari, pamoja na kupongeza uamuzi wa Tume kukutana nao, walishauri wananchi wahakikishiwe uhuru wa kutoa maoni ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu bila woga.

“Baada ya kukusikiliza, ninaona utashi wa Tume kufanya kazi kwa uwazi na uhuru. Lakini kwa hali inavyoendelea hususan hapa Zanzibar, nadhani inabidi wananchi wahakikishiwe uhuru wa kutoa maoni,” alipendekeza Jabir Idrissa, Mhariri wa gazeti la Mwanahalisi aliyepo Zanzibar.

Mkutano wa leo (Jumatano, Juni 20, 2012) ni wa pili na umewalenga waandishi wa habari waliopo Zanzibar. Kesho (Alhamisi, Juni 21, 2012) Jaji Warioba ataongea na Wakuu wa Wilaya na Mikoa kutoka Zanzibar. Tume tayari imeshafanya mikutano na Wakuu wa Mikoa na Wilaya wa Tanzania Bara katika semina iliyofanyika mjini Dodoma mwezi uliopita.
Posted by MROKI On Wednesday, June 20, 2012 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo