LEO ni siku ya Bajeti kwa mwaka wa fedha 2012/13. Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa anatarajiwa kuanza kusoma Bajeti ya Serikali inayosubiriwa kwa hamu na mamilioni ya Wananchi 10.00 jioni.
Hotuba ya Dk Mgimwa itatanguliwa na ile ya Mipango ya Serikali itakayosomwa asubuhi mara baada ya kipindi cha Maswali na Majibu na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira.
Kutwa nzima ya jana, Dk Mgimwa na watendaji wengine wa Wizara ya Fedha walikuwa katika pilikapilika za kukamilisha maandalizi ya bajeti hiyo ya Sh15 trilioni, ambayo inatarajiwa kuwa na vipaumbele saba.
Baada ya kipindi cha maswali na majibu jana, Kamati ya Uongozi ya Wabunge wa CCM, ilikutana chini ya uenyekiti wa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kufanya maandalizi ya kuwapa taarifa ya bajeti hiyo wabunge wakewaliotarajiwa kukutana kuanzia saa 10 jioni.
Kikao hicho ambacho kiliendelea hadi saa tisa alasiri, pia kilihudhuriwa na Dk Mgimwa na Manaibu wake, Janeth Mbene na Saada Mkuya Salum ambao kama alivyo waziri wao, nao wote ni wapya katika wizara hiyo.
Dk Mgimwa alisema jana kwamba maandalizi ya bajeti yalikuwa yamekamilika na tayari Serikali ilikuwa imefikia mwafaka na Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi inayoongozwa na Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge.
“Hoja za wajumbe wa Kamati ya Bunge ni kwamba Serikali iongeze Bajeti ya Maendeleo kutoka asilimia 30 hadi 35 na Bajeti ya matumizi ya kawaida ishuke kutoka asilimia 70 hadi 65, lakini tumejaribu kufanya mapitio ya pamoja imeshindikana,” alisema Dk Mgimwa na kuongeza:
“Hata hivyo, tumekubaliana kwamba kuanzia mwaka ujao wa fedha tuanze kujipanga mapema ili tuweze kufikia lengo hilo na hata ikiwezekana tuvuke hapo.”
Kwa upande wake, Chenge alisema: “Tumewasikiliza na mazingira ndiyo hayo sasa katika hatua hiyo unafanyaje? Lakini hata wao (Serikali) wameanza kuona umuhimu wa hoja yetu kwa hiyo tumeelewana nao kwamba katika bajeti ijayo ambayo nayo haiko mbali, basi wazingatie mapendekezo ya wabunge.”
Hata hivyo, Waziri Kivuli wa Fedha, Zitto Kabwe alisema Bajeti hiyo ya Serikali haitoi matumaini kwa Watanzania kwani itakuwa ni kwa ajili ya kulipa madeni.
“Hii yaweza kuwa Bajeti ya kulipa madeni zaidi kuliko ya kuchochea maendeleo.... yaweza pia kuwa ni Bajeti ya kukopa maana jumla ya Sh 5.1 trilioni (Dola za Marekani 3.19 bilioni), zitachukuliwa kama mikopo kwa Serikali. Mikopo ya kibiashara ambayo ni mikopo ghali sana itachukuliwa kwa wingi zaidi kuliko mwaka wa fedha uliopita.”
Hofu ya kukwama
Awali, kulikuwa na hofu kwamba bajeti hiyo ingekwama kutokana na wabunge kusisitiza kuongezwa kwa fedha maendeleo.
Hata hivyo, wabunge kupitia Kamati ya Fedha ya Uchumi walilegeza msimamo wao kutokana na maombi ya Waziri Mgimwa na Waziri Mkuu, Pinda ambao kwa nyakati tofauti, walinukuliwa katika vikao vya kujadili bajeti hiyo wakiwaomba wabunge wasiwabane kwani watendaji wa wizara hiyo walikuwa ni wapya.
Lakini kuna taarifa kwamba hata sura ya sasa ya bajeti hiyo inatokana na Dk Mgimwa kuifumua katika baadhi ya maeneo baada ya kuingia ofisini kutokana na mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa mapema mwezi uliopita na Rais Jakaya Kikwete na kumweka nje aliyekuwa akiongoza wizara hiyo, Mustafa Mkulo.
Pinda alinukuliwa akizungumza katika kikao cha kutoa mwongozo kwa wabunge wote (briefing) kwamba, Dk Mgimwa aliomba ridhaa ya Rais kufumua bajeti hiyo upya ili iweze kwenda sawa na mtizamo wake kama kiongozi wa wizara, hali iliyosababisha kuchelewa kwa vitabu vya bajeti kwani baadhi viliandaliwa upya.
Hata hivyo, baadhi ya wabunge wakiwamo wa CCM walisema kwa nyakati tofauti kwamba wanaiona Serikali kutokuwa na usikivu kwani mapendekezo yao kila mwaka yamekuwa hayatekelezwi.
“Ni yale yale tu, kweli Dk Mgimwa ni mpya kwenye Wizara lakini hata angekuwa Mkulo hakuna kinachotekelezwa, kila siku wanaahidi halafu hawatekelezi.” alihoji mmoja wa wabunge wa CCM jana.
Hata hivyo, wabunge wa CCM hawawezi kuzuia Bajeti Kuu ya Serikali kutokana na kubanwa na kanuni za chama hicho, lakini huenda hasira zao zikaziangukia bajeti za wizara na kuwaweka mawaziri katika wakati mgumu.
Uchambuzi wa Zitto
Uchambuzi wa Zitto unaweka wazi kwamba vitabu vya Bajeti vinaonyesha mafungu matano ya juu kwenye Bajeti hiyo kuwa ni Deni la Taifa (Sh2.7 trilioni), Wizara ya Ujenzi (Sh1 trilioni), Wizara ya Ulinzi (Sh920 bilioni), Wizara ya Elimu (Sh721 bilioni) na Wizara ya Nishati na Madini (Sh641 bilioni) ambazo jumla yake ni Sh5.982 trilioni.
“Jumla ya mafungu haya ni sawa na asilimia 40 ya Bajeti. Kwa hiyo asilimia 40 ya Bajeti yote imepangwa kwa mafungu matano tu. Fungu lenye kiwango kikubwa zaidi ya Bajeti kuliko vyote ni fungu 22 ambalo ni malipo kwa Deni la Taifa,” unaeleza uchambuzi huo uliofanywa na Zitto na kuongeza:
“Pia sehemu kubwa ya fedha zilizotengwa kwa Ujenzi na Nishati ni madeni kwa makandarasi wanaotekeleza miradi ya miaka ya nyuma. Wabunge wanapaswa kufanya uchambuzi zaidi wa Bajeti ya mwaka huu inayopendekezwa na Serikali.”
“Kuna haja kubwa ya kuharakisha kuanzishwa kwa Ofisi ya Bajeti katika Bunge na Kamati ya Bunge ya Bajeti ili kuweza kufuatilia kwa karibu, kuchunguza na kutoa taarifa kwa wabunge ili kuwezesha kuboresha Bajeti.”
Kilio cha wafanyabiashara
Wafanyabiashara katika Soko Kuu la Kariakoo, Dar es Salaam wametaka bajeti hiyo iwe ya kumaliza tatizo la mfumuko wa bei ya vyakula.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, mmoja wa wafanyabiashara hao, Elizabeth Edward alisema bajeti mara nyingi imekuwa haiwalengi watu wa hali ya chini, bali wenye uwezo.
Edward alitaka Bunge litumie kipindi hiki kupunguza mfumuko wa bei ya chakula ili wananchi waweze kuona unafuu wa maisha.
“Hivi sasa mchele mzuri unauzwa kuanzia Sh2,200 hadi Sh2,500 lakini, mimi siwezi kununua mchele wa bei kubwa. Nitanunua mchele wa Sh1,800 hadi 1,660 ambao ni mbaya una mchanga,” alisema Mama Lishe huyo na kuongeza:
“Mafuta ya kula tunauziwa lita moja Sh3,000, sukari Sh2,400 hivyo kutokana na vyakula kupanda, chai tunauza Sh200 na vitafunwa kuanzia Sh200 hivyo, watu wengi hawanunui, mtu anaona bora ale muhogo wa Sh100 na maji tu.”
Mfanyabiashara wa Soko la Mabibo, Issa Abdallah alisema bajeti hiyo haimwangalii mfanyabiashara wa chini... “Tunataka Bunge liilegeze bajeti ili kuondoa mfumuko wa vyakula hapa nchini.”
“Kama wabunge wangekuwa na umoja, nina imani huu mfumuko wa bei ya vyakula usingekuwapo hivyo, wabunge wote wanatakiwa wagomee bajeti ambayo itamkandamiza mwananchi wa hali ya chini.”
Mtaalamu wa uchumi kutoka Chuo Kikuu Mzumbe, Dk Prosper Ngowi alisema kutokana na hali ya uchumi wa nchi kukabiliwa na changamoto ya mfumuko wa bei na umaskini wa watu wake, inahitajika bajeti inayoweza kutoa majibu kwenye matatizo ya msingi.
Dk Ngowi aliyataja matatizo hayo kuwa ni pamoja na umeme, miundombinu ya umwagiliaji na ile ya usafirishaji kama barabara na reli.
Hata hivyo, alisema dalili zinaonyesha kuwa hilo haliwezi kufanikiwa, kwani katika Sh15 trilioni zinazotarajiwa kuwasilishwa kama Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2012/13, Sh5 trilioni pekee ndizo zinatarajiwa kutumika kwa shughuli za maendeleo.
“Kuna tetesi kuwa kati ya hizo Sh5.25trilioni zitakwenda kulipa madeni na zitakazobaki ndizo za maendeleo, hali hii inaonyesha kabisa kuwa hakuna matumaini,” alisema Dk Ngowi.
Alisema swali jingine la kujiuliza ni wapi Sh15 trilioni za bajeti zitakakopatikana akisema ukusanyaji wa kodi wa Serikali hauridhishi na pia nchi wahisani zinazotegemewa nazo pia hali yake ya kiuchumi siyo nzuri.
SOURCE: Mwananchi Online.
0 comments:
Post a Comment