Kaimu mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Raymond Mushi (kulia) akimkabidhi mwenge wa Uhuru Kaimu mkuu wa mkoa wa Pwani Bi. Halima Kihemba (kushoto)leo katika eneo la Mwandege wilayani Mkuranga. Mwenge wa Uhuru umemaliza mbio zake mkoani Dar es Salaam leo ambapo miradi yenye thamani ya shilingi bilioni 7 imezinduliwa.
********
Na. Adrophina Ndyeikiza na Aron Msigwa – Ofisi ya RC, DSM.
Kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa Kepteni Honest Mwanossa amesifu juhudi mbalimbali zinazochukuliwa na mkoa wa Dar es Salaam katika kuwaletea maendeleo wananchi.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya Mwenge wa Uhuru kati ya mkoa wa Dar es Salaam na Pwani wilayani Mkuranga kiongozi wa mbio hizo amesema kuwa mkoa wa Dar es Salaam licha ya kuwa na changamoto mbalimbali umepiga hatua katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Amesema katika siku 3 za mbio za mwenge wa Uhuru mkoani humo takribani miradi 27 ya maendeleo imezinduliwa na kuwekewa mawe ya msingi na kuongeza kuwa mkoa huo ndio kitovu cha maendeleo ya nchi.
“ Ninawapongeza viongozi wa mkoa wa Dar es salaam kwa mapokezi mazuri ya Mwenge wa Uhuru na pia juhudi mbalimbali za kufanikisha uzinduzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 7”
Aidha kiongozi huyo wa mbio za Mwenge kitaifa ametoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika utunzaji na uimarishaji wa miradi hiyo ya maendeleo ili iendelelee kuwa na manufaa kwa kizazi cha sasa na baadaye.
Awali akizungumza na wananchi wa wilaya ya Mkuranga kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam wakati wa makabidhiano hayo kaimu mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Bw. Raymond Mushi amesema kuwa Mwenge wa Uhuru ukiwa mkoani Dar es salaam umezindua miradi 27 ya maendeleo ikihusisha michango ya nguvu za wananchi kiasi cha shilingi milioni 137, michango ya Halmashauri shilingi bilioni 1.3, fedha kutoka serikali kuu kiasi cha shilingi milioni 69 na fedha za wahisani sh. Bilioni 6.3.
Mwenge wa Uhuru ambao umemaliza mbio zake leo mkoani Dar es Salaam na kuelekea mkoa wa Pwani, umekwisha tembelea takribani mikoa 12 kati ya 30 ambapo kilele chake kitakwenda sambamba na kumbukumbu ya Baba wa Taifa na Wiki ya Vijana kitaifa tarehe 14, Oktoba mkoani Shinyanga.
0 comments:
Post a Comment