Mkurugenzi wa Mawasiliano na Mahusiano wa SBL, Teddy Mapunda kulia, akijadiliana na jambo na Mkurugenzi wake, Richard Wells jana |
KATIKA ukumbi uliopambwa vema- taa zenye mwanga mzuri wa rangi tofauti na mpangilio mzuri wa viti na meza sambamba na majukwaa mawili- moja la burudani na lingine la kutolea tuzo- shughuli ya Utoaji wa Tuzo za Wanamichezo Bora Tanzania kwa mwaka jana, ilifana jana.
Unaweza kusema nini zaidi ya shukrani kwa Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), iliyodhamini tuzo hizo, zinazoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania, TASWA?
Hakika SBL wanastahili pongezi. Tena sana, kwa kudhamini tuzo hizi, ambazo lengo lake ni kutambua na kuthamini mchango wa wanamichezo wa taifa hili, ambao kwa hakika wanastahili heshima ambayo pengine kwa sasa hawaipati kwa kiwango kinachotakiwa.
SBL iliyotumia kiasi cha Sh. Milioni 150 kudhamini tuzo hizo, imekuwa mstari wa mbele katika kusaidia michezo na sekta nyingine mbalimbali za kitaaluma na kijamii kwa ujumla nchini.
Hapana shaka ni sera nzuri, chini ya uongozi bora wa kampuni hiyo, chini ya Mwenyekiti wa Bodi ya SBL, Jaji Mark Bomani, Mkurugenzi wake, Richard Wells, Mkurugenzi wa Masoko, Ephraim Mafuru, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Mahusiano wa kampuni hiyo, Teddy Mapunda.
Lakini pia huwezi kuacha kutoa pongezi kwa wa TASWA, chini ya Mwenyekiti wake Juma Abbas Pinto na Katibu Mkuu wake, Amir Ally Mhando kwa utendaji wao mzuri, uliozifanya tuzo hizo sasa zirejeshe heshima yake.
Katika usiku huo, ndani ya ukumbi wa Diamond Jubilee, katikati ya Jiji la Das es Salaam, mwanasoka chipukizi nchini, Shomary Kapombe aliibuka kinara, baada ya kutwaa tuzo ya Mwanamichezo Bora wa Mwaka na kuzawadiwa kitita cha Sh. Milioni 12.
Awali, Kapombe anayechezea klabu bingwa ya Tanzania, Simba SC, alizawadiwa Sh. Milioni 1 kwa kutwaa tuzo nyingine ya Mwanamichezo Bora Chipukizi Tanzania- ingawa wengine walihoji kwa nini hata tuzo ya Mwanasoka Bora aliyoshinda beki Aggrey Morris wa Azam, FC, asiipate yeye pia?
Wanaweza kuwa wana hoja wenye mtazamo huo- kwani sababu Kapombe kama ni Mwanamichezo Bora Tanzania, basi lazima awe bora kwanza kwenye mchezo anaoucheza.
Lakini hili si suala zito sana, kwa sababu Kamati iliyopewa jukumu la kufanya mchakato huu ilikuwa huru na imefanya kulingana na taratibu ilizojiwekea, chini ya Mwenyekiti wake, Mwandishi wa Habari za michezo mwandamizi Tanzania, Masoud Saanan.
Mkurugenzi wa Masoko wa SBL, Eiphraim Mafuru kulia akikabidhi tuzo |
Mwenyekiti wa TASWA, Juma Pinto kulia |
Pongezi zaidi kwa TASWA kwa kupanua wigo wa tuzo- na sasa hadi Mwanasoka wa Tanzania anayecheza nje anazawadiwa na jana imeshuhudiwa Mbwana Ally Samatta wa Tout Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) akishinda tuzo hiyo.
Yote kwa sababu ya fungu la kutosha kutoka kwa wadhamini, SBL, ambao wamekuwa wepesi mno kupiga jeki shughuli mbalimbali za michezo nchini zinapokwama.
Shoo ya tuzo ilifana. Bendi ya Extra Bongo chini ya uongozi wake Ally Choky Rwambo ilifanya vizuri katika jukwaa lililokuwa upande wa kushoto wa ukumbi. Wane Star naye alifanya vema kwa ngoma zake za asili.
Waongoza shughuli (ma MC) Gadna Habash na Ephraim Kibonde walifanya vema kwa upande wao- sauti zao ni maarufu na zinapendwa sana. Walitumia uzoefu wao kuongoza vema shughuli hiyo, ambayo mgeni wake rasmi alikuwa rais Mstaafu wa awamu ya Pili, Alhaj Ally Hassan Mwinyi.
Mzee Mwinyi ni kiongozi ambaye anapendwa sana na Watanzania kutokana na kile ambacho unaweza kukiita hekima na busara aliyonayo na jana japokuwa alipanda jukwaani kuhutubia wakati ‘muda umeenda sana’ watu walivumilia maelezo yake marefu akitoa nasaha za msingi katika sekta ya michezo.
Alisema mengi Mzee Mwinyi, lakini kikubwa alisistiza maandalizi mazuri kwa timu zetu kabla ya kuingia kwenye mshindano ili kuepuka kufanya vibaya. Mzee Mwinyi, aliyemrithi marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kiti cha urais wa Tanzania mwaka 1985 kabla ya kumuachia Benjamin William Mkapa miaka 10 baadaye, aliwataka wanamichezo walioshinda tuzo hizo, kutobweteka, badala yake kuongeza juhudi ili kusaka mafanikio zaidi.
Ulikuwa usiku mzuri jana ndani ya Diamond Jubilee na asanté sana SBL. Hongera TASWA.
Mzee Mwinyi kulia akimkabidhi tuzo Kapombe kushoto kabisa jana. Wengine ni Makamu Mwenyekiti wa Simba Sc, Geoffrey Nyange 'Kaburu' na Mkurugenzi wa SBL. Richard Wells. SOURCE: BIN ZUBERY BLOG |
0 comments:
Post a Comment