Kampuni
ya Television ya kulipia ZUKU leo imetangaza kulidhamini tamasha la
ZIFF kwa kulipa tamasha shilingi milioni mia moja kila mwaka kwa miaka
kumi ijayo. Fedha hizo zinakwenda katika kulistawisha tamasha na
kulitangaza katika wigo wa filamu hapa Afrika Mashariki.
******
Mkurugenzi
Mkuu wa Wananchi Group Richard Bell alisema kuwa hii ni hatua kubwa
katika ushirikiano uliopo kati ya ZUKU na ZIFF. “Kwa hakika jinsi
tamasha linavyokuwa ndivyo tutakavyozidi kuliongezea uwezo. Huu ni
mwanzo tu”, aliongezea.
“Na
wala hatutaki kuwazuia wadau wengine kujumuika na ZIFF. Tuonavyo sisi
ni kuwa wadau wengine watatumia nafasi hii kujinufaisha kwa kujitangaza
kupitia ZIFF”.
Akisifu
uwamuzi huu, Mwenyekiti wa Wananchi Group, Ali Mafuruki aliongezea,
“Kama chombo cha habari ZUKU imejitoma katika kukuza sanaa na biashara
zake. Kuungana na ZIFF kunatupa furaha sana tukitilia maanani kuwa ZIFF
imekuwa chombo mahiri na cha kimataifa kinachoendeleza tasnia ya
filamu.”
Akizungumza
toka Geneva, Mwenyekiti wa ZIFF Mahmoud Thabit Kombo, amefurahishwa
sana na imani iliyoonyeshwa na ZUKU kwa udhamini huu. “Unajua ZIFF ni
kiungo na chombo muhimu cha utamaduni wa Mwafrika nasi tunajivunia
kutukuka kwa taasisi hii ya Kizanzibari’, aliongezea.
Mashirikiano
haya ya miaka 10 yataishia mwaka 2022 na Mwenyekiti huyo anaamini kuwa
hadi hapo ZIFF itakuwa imejenga uwezo mkubwa na mahusiano ya kudumu na
taasisi mbalimbali za biashara na za habari.
“Ni
kweli tunafurahia kuona nembo za ZIFF na ZUKU zikishabihiana, lakini
uhusiano wetu sio wa kutangaza nembo tu. ZUKU inataka kushamiri kote
Afrika na uhusiano huu utalenga kuiwezesha ZUKU kutanuka katika tasnia
za habari, filamu na burudani”, aliongezea Mwenyekiti huyo.
Ubia
huu ni kama mwale unaoashiria wawekezaji na wajasiria mali wenye upeo
mkubwa uliopo wa kukuwa kibiashara na kuongeza ajira hasa katika wigo za
utalii na burudani. Kwa kuendeleza biashara za sanaa ZUKU na ZIFF
watawezesha zaidi watengenezaji na waigizaji wa filamu.
ZUKU
ndio mtandao wa televisheni ya kulipia inayokuwa haraka zaidi hapa
Afrika mashariki ikilenga kutoa huduma za burudani za hali ya juu lakini
kwa bei nafuu. Kwa sasa inapatikana Tanzania, Kenya na Uganda na
itapanuka kufikia nchi nyingi za jirani hivi karibuni.
Tamasha la ZIFF litakuwepo huko Zanzibar kati ya tarehe 7 na 15 Julai, 2012
0 comments:
Post a Comment