Nafasi Ya Matangazo

April 19, 2012

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal (katikati)akikata utepe kuzindua mpango wa Wanachama wa Mfuko wa GEPF,kuchangia na kuweka akiba zao kupitia huduma ya Airtel Money, wakati Makamu alikuwa akifungua Mkutano Mkuu wa Nne wa Mwaka wa Wanachama wa Mfuko wa Akiba ya Wafanyakazi Serikalini, jijini Mwanza leo.
Makamu wa Rasi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed GharibBilal, akisoma hotuba yake wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa nne wa Mwaka wa Wanachama wa Mfuko wa Wafanyakazi Serikalini, ulioanza leo Aprili 19, 2012 kweye Ukumbi wa Hoteli ya Gold Grest, jijini Mwanza.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muunganowa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akimkabidhi zawadi Mwanachama wa Mfuko wa GEPF, Andrew Maziku, aliyefanya vizuri katika kuwekeza akiba katika mfuko huo, wakati Makamu alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu wa nne wa Mwaka wa Wanachama wa Mfuko wa Akiba ya Wafanyakazi Serikalini, katika Ukumbi wa Hoteli ya Gold Grest, jijini Mwanza, leo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiwa katika picha ya pamoja ya kumbukumbu na Viongozi, wafanyakazi na wadau wa Mifuko ya Jamii baada ya kufungua Mkutano Mkuu wa Nne wa Mwaka wa Wanachama wa Mfuko wa Akiba ya Wafanyakazi Serikalini, jijini Mwanzanleo.

Serikali imeitaka Mifuko ya Jamii nchini kuhakikisha inatanua huduma zao kwa kuwafikia wananchi wengi ili waweze kumudu maisha yao hasa kipindi wafikwapo na majanga.

Kauli hiyo imetolewa leo na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal wakati alipokuwa akifungua mkutano wa mwaka wa wanachama wa mfuko wa Akiba ya Wafanyakazi Serikalini (GEPF) mjini Mwanza.

Dk. Bilal alisema pamoja na mchango mkubwa wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii katika uchumi na maendeleo ya taifa kwa ujumla, bado ni sehemu ndogo sana ya Watanzania wanapata kinga dhidi ya majanga kupitia mifuko hiyo. “Takwimu zinaonesha kati ya Watanzania milioni 22.4 wenye uwezo wa kuzalisha kipato, walio katika mifuko yote 6 si zaidi ya asilimia sita,” alidokeza

Mifuko ya jamii iliyopo nchini ni pamoja na Mfuko wa Akiba ya Wafanyakazi Serikalini (GEPF), Mfuko wa Akiba ya Wafanyakazi wa Mashirika ya Umma (PPF), Mfuko wa Akiba ya Watumishi wa Umma (PSPF), Mfuko wa Akiba wa Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (LAPF), Mfuko wa Akiba wa Taifa (NSSF) na Mfuko wa Akiba wa Zanzibar (ZSSF).

Alisema serikali imeanzisha Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa sekta ya hifadhi ya jamii ambayo moja ya majukumu yake ni kupanua wigo wa wanachama wanaojiunga na mifuko hiyo. “Lengo ni kuhakikisha kwamba asilimia kubwa ya Watanzania wanapata kinga dhidi ya majanga yanayoweza kutokea kutokana na kupungukiwa au kupoteza kipato, kutokana na umri mkubwa, maradhi, kufariki au kuumia kazini,” alisema

Aliupongeza Mfuko wa GEPF kwa kazi nzuri wanayoifanya kuhakikisha kwamba kila Mtanzania anapata kinga hiyo kwa kupitia mpango wao wa Hiari wa kujiwekea Akiba ya Uzeeni ambapo katika kipindi cha miaka miwili wameweza kusajili zaidi ya wanachama 10,000 kupitia mpango huo na kujiwekea zaidi ya shilingi milioni 800.

Mapema, akimkaribisha Makamu wa Rais, Naibu Waziri wa Fedha Gregory Teu aliitaka mifuko hiyo ya jamii kubuni mbinu mbalimbali zitakazowawezesha kupanua wigo wa wanachama. Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya GEPF Ladislaus Salema alimweleza Makamu wa Rais kuwa mfuko umeweza kuboresha utendaji wake wa kazi kiasi cha kuweza kutoa mafao ndani ya siku saba.

Katika hafla hiyo Dk. Bilal alikabidhi tuzo kwa wanachama walioonyesha uwezo mkubwa katika kuchangia na kuwasilisha michango katika mfuko huo pamoja na taasisi kwa kuwasilisha michango ya wafanyakazi wake kwa wakati. Aidha alizindua huduma ya Airtel Money ambayo itawawezesha wanachama kutuma michango yao kupitia simu za mkononi.
Posted by MROKI On Thursday, April 19, 2012 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo