Nafasi Ya Matangazo

February 22, 2012


* Nusu ya mapato ya Serikali hutokana na zao hilo, imeweka bil 50/-
* Husaidia kuunda magari, ndege, ujenzi wa nyumba, karatasi, noti
* Imewekeza ekari 35,000 Tanga, Kilimanjaro, Pwani, Morogoro
* Bidhaa huuzwa soko la Mashariki ya Kati, Nigeria, Ulaya, India
 
UTAJIRI wa nchi zilizoendelea duniani (G8) umefikiwa kwa kuzingatia uongozi wa nchi hizo kuwekeza kwenye viwanda, na asilimia 90 ya uwekezaji huo hutegemea uzalishaji wa bidhaa zitokanazo na mazao.  Ni asilimia 10 tu ya uzalishaji wa bidhaa katika viwanda hutegemea vitendea kazi ikiwemo mashine za aina zote na vyombo vya usafiri.
Kwa kutambua kuwa viwanda ndiyo chanzo cha ukuzaji uchumi wa nchi, msisitizo kwa viongozi wa ngazi za juu serikalini huelekezwa kwenye kilimo ambapo mkulima atakapozalisha mazao yawe ya chakula aweze kujikimu kwa chakula, lakini pia awe na ziada ambayo ataiuza kwa lengo la kujiongezea kipato.  Yapo mazao ya chakula na ya biashara, na mazao ya biashara hutegemewa kukuza pato la mkulima kwa asilimia kubwa kuliko ilivyo kwa wakulima wa mazao ya chakula. Pia kilimo cha mazao hayo hukuza pato la nchi kwa kuzingatia biashara za kimataifa.

Nchini Tanzania yapo mazao mengi ya biashara, na miongoni mwa hayo ni pamoja na buni, chai, korosho, tumbaku na mkonge.  Wakati baadhi ya wananchi kutokana na hali ya jiografia ya maeneo yao hulazimika kulima aina hiyo ya mazao, baadhi hulima mazao ya chakula ambayo ni mahindi, maharagwe, mchele, viazi, ndizi na mihogo.

Katika makala haya, kubwa linalobainishwa ni jinsi kilimo cha mkonge kilivyotoa ajira kubwa kwa vijana tofauti na ilivyo kwenye uwekezaji wa aina nyingine ya mazao, lakini ukweli wa hilo hauko wazi kwa wengi.  Sifa nyingi zinazobebwa na kilimo cha zao la mkonge ni pamoja na uchumi wa nchi ambapo nusu ya mapato ya Serikali hutokana na zao hilo, lakini pia robo tatu ya ukubwa wa kilimo ni wa zao la mkonge.  Asilimia 80 ya Watanzania wameajiriwa katika kilimo, hivyo kufanikisha sera ya Kilimo Kwanza na mfano wa wazi ni Kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL).

Kampuni hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa katika sekta ya kilimo na kuinua kiwango cha uchumi na maendeleo ya nchi kwa ujumla.  Mwaka 1997, kampuni hiyo iliwekeza ekari 35,000 za mkonge katika mashamba kadhaa mkoani Tanga, Kilimanjaro, Pwani na Morogoro na imeweza kufanikisha biashara ya zao hili.

Kwa uwekezaji huo, zaidi ya wafanyakazi 300 wameajiriwa kwenye mashamba ya mkonge kwa ajili ya kushughulikia zao hilo, idadi ambayo ni kubwa kwa sekta binafsi katika utoaji ajira kwa Watanzania.  Miundombinu kama nyumba za wafanyakazi, kambi za wafanyakazi, matumizi ya barabara, huduma za shule na zahanati vimeanzishwa katika mashamba yote.
Akizungumza na mwandishi wa makala haya, Mkurugenzi Mkuu wa MeTL, Mohamed Dewji maarufu kama Mo, anasema kuwa vitu vingine kama magari na vifaa vya kilimo vimewekwa katika kila shamba, hivyo kampuni imewekeza sh. bilioni 50 katika kilimo hicho.
"Mkonge ni zao pekee ambalo halihitaji maji na linaloweza kuvunwa wakati wowote. Halina mipaka ya ukame... hili ndilo la kulipa kipaumbele kwani litawainua wakulima," anasema Dewji ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mjini (CCM).  "Shughuli za maendeleo ya kilimo zimetoa ajira kwa zaidi ya watu 5,000 wakati wa msimu wa kilimo na tumetoa mbinu za kilimo kupitia kwa wataalamu wetu hivyo kuboresha ufahamu wa wafanyakazi wetu," anasema Mkuu wa Kitengo cha Kilimo wa MeTL, Mamik.

Katika mikoa hiyo, MeTL huzalisha tani 6,000 za mkonge kila mwaka na wanazo ekari 10,000 za mashamba hayo ambapo dhamira kuu ni kulima kati ya tani 10,00 na 15,000 ili kufanikisha kupatikana soko la nje pia.  Mifuko iliyotengenezwa kwa mkonge (magunia) ni bidhaa iliyo bora, inasaidia kuhifadhi vizuri bidhaa zinawekwa ndani yake.

Katika jitihada za kuisadia Serikali, wamesaidia kuinua soko la mkonge kwa kuongeza uzalisahaji kutoka zamu moja ya wafanyakazi hadi tatu kwa siku na kuajiri watu 7,000.

Zao hili linatumika pia kutengenezea kamba katika kiwanda cha 21st Century Holdings Ltd kilichopo Dar es Salaam ambacho kilianzishwa mwaka 2001 ili kuipa nguvu kampuni katika kuendeleza zao la mkonge.  Kiwanda kinazalisha bidhaa mbalimbali zikiwemo kamba, mazulia, magunia na brashi ambapo pia wamekuwa wakiuza katika soko la Mashariki ya Kati, Nigeria, Ulaya na India.

Kitengo cha kilimo cha kampuni hiyo kinalenga kuchangia uchumi wa pato la taifa kupitia kilimo kwa kusisitiza sera ya Kilimo Kwanza ambayo imeanzishwa kwa nia ya kuleta mabadiliko ya kilimo kwa wakulima na taifa lao.  Ni wakati muafaka wa wawekezaji kuona kwa jicho la pembeni mambo ambayo yanaweza kuleta mapinduzi ya maendeleo kupitia kilimo kama walivyotangulia kufanya baadhi ya wawekezaji hususan kwenye eneo la kilimo cha mazao ya chakula, lakini pia bila kusahau kilimo cha mazao ya biashara.

Mkonge unavyotajirishwa.

Mamik anasema kupanda hadi kuvuna mkonge kwa mara ya kwanza huchukua miaka mitatu, lakini katika kipindi hicho, mkulima anaendelea kufaidi mavuno kutokana na mazao mengine kama mahindi na maharagwe ambayo hupandwa sambamba na mkonge.

"Kwa maana hiyo, mkulima anaanza kupata mavuno tangu mwaka wa kwanza anapoanza kulima na anaendelea hivyo kwa miaka mitatu. Baada ya hapo mazao mengine hayawezi tena kuendelea kustawi lakini kuanzia hapo anaanza kuvuna mkonge hivyo kumudu kununua mazao hayo mengine ya chakula."

Kuhusu mapato yanayotokana na mavuno kwa hekta moja, mkuu huyo wa kitengo anasema mkulima anaweza kupata wastani wa sh. 600,000 kwa mwaka, hiyo ikiwa ni baada ya kutoa gharama zote za uendeshaji.  Anafafanua kwamba zao la mkonge ni lile lisilo na msimu maalumu wa kupandwa wala ule w kuvunwa na hatua hizo zikifikia pia hufanyika bila shida wakati katika soko la dunia kukiwa na uhakika wa mauzo yenye tija kwa wakulima.

Vilevile mahitaji ya kutumia mkonge yanaendelea kuongezeka katika suala la uzalishaji bidhaa kama vifaa vya ujenzi, vifaa vya magari, chakula cha mifugo, mbolea na uzalishaji wa nishati huku bei ya mkonge ikiwa imefikia dola 1000 kwa singa za daraja UG.

Matumizi ya mkonge.
Mamik anayataja matumizi ya zao hilo ambayo wengi wetu tunayajua. Haya ni pamoja na kutengenezea kamba, mazulia na magunia. Lakini anakwenda mbali na kutaja mengine ambayo wengi hawayajui. Haya ni pamoja na kusaidia katika uundaji wa magari na ndege, ujenzi wa nyumba, karatasi (noti na vifuko vya majani ya chai).

Lakini mbali ya matumizi hayo, mkonge unatumika pia katika kuzalisha umeme, kutengeneza nishati mbadala ya ethanol, mbolea na chakula cha mifugo.
Posted by MROKI On Wednesday, February 22, 2012 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo