Nafasi Ya Matangazo

December 15, 2011

CHUO Kikuu cha Dar es Salaam, Sehemu ya Mlimani (UDSM), kimewafukuza chuo jumla ya wanafunzi 43 waliokuwa wamesimamishwa masomo wakisubiri kumalizika kwa kesi zilizoko mahakamani pamoja na kuwa viranja wa vurugu zilizotokea chuoni hapo mwanzoni mwa wiki hii.
Aidha, chuo hicho kimewasimamisha wanafunzi tisa kutokana na makosa hayo hayo ambapo wanasubiri uamuzi wa Baraza la Chuo na iwapo watakuwa na hatia, adhabu stahiki itafuatwa.

Kadhalika kimesema kitafanya mawasiliano na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) ili wanafunzi waliofukuzwa, wasipate tena mkopo wa Serikali wala kuruhusiwa kudahiliwa tena katika chuo chochote cha umma.

Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala alitoa uamuzi huo jana Dar es Salaam ambo ni wa Baraza la Chuo Kikuu kuhusu vurugu za wanafunzi ambazo zilisababisha uvunjifu wa amani na ukosefu wa utulivu chuoni hapo.

Baada ya kumaliza kusoma uamuzi huo mbele ya waandishi ya habari, ulibandikwa kwenye kuta za matangazo chuoni hapo na kila mwanafunzi alifika na kusoma.

Kuhusu wanafunzi waliofukuzwa, Profesa Mukandala alisema wako wa mwaka wa kwanza hadi wa tatu, lakini wengi wa waliofukuzwa ni wa mwaka wa pili na wa tatu na ambao wanasoma masomo ya sanaa.

Profesa Mukandala alifafanua kuwa kati ya wanafunzi 51 waliokuwa wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam Novemba mwaka huu wakikabiliwa na makosa ya kufanya mkusanyiko usio halali na kukaidi amri ya Jeshi la Polisi, 43 kati yao ndio waliofukuzwa, watatu sio wanafunzi wa chuo hicho, tisa hawajasikilizwa na Baraza la Chuo hicho na kutolewa mapendekezo.

Aidha, alisema matukio yaliyojiri Jumatatu na Jumanne wiki hii ni mwendelezo wa matukio ya uvunjifu wa amani yaliyoanza mwanzoni mwa Novemba mwaka huu ambapo kila mara vitendo hivyo vilianzishwa na kikundi kidogo cha wanafunzi na hatimaye kupata wafuasi katika kuvuruga shughuli za chuo.

Makamu Mkuu wa Chuo alisema madai ya wanafunzi waliokuwa wakiendesha vurugu hizo, yamekuwa yakibadilika kila kukicha ambapo mwanzo walidai mikopo kwa ajili ya wanafunzi waliochaguliwa katika mwaka huu wa masomo na ambao hawakupata mikopo.

Alisema baadaye dai kubwa likawa ni kuachiwa huru wenzao waliokamatwa na kufunguliwa mashitaka kutokana na kuendesha maandamano kinyume cha sheria na kukaidi amri ya Jeshi la Polisi ya kutawanyika.

Profesa Mukandala alisema katika siku mbili za vurugu madai ya awali yalikuwa kuondolewa kwa adhabu za kinidhamu walizopewa wenzao wachache kwa mujibu wa Kanuni na Sheria za Chuo, lakini baadaye wakageukia suala la kupatiwa fedha za malazi na chakula kuanzia Desemba 10, mwaka huu.

Kuhusu vurugu zilizotokea kwa siku hizo mbili, alisema kikundi hicho kiliingia madarasani na kuwatimua wenzao kwa kutumia fimbo na wakati mwingine kuwamwagia maji wahadhiri waliowakuta wakifundisha, kuziba lango kuu la kuingilia jengo kuu la utawala na kusababisha shughuli ndani ya jengo hilo kusimama.

Alisema mbaya zaidi kikundi hicho kilikwenda kantini na kuendesha vurugu kubwa, ikiwemo kuwamwagia wenzao chakula walichokuwa wanakula, kumwaga mavumbi katika chakula kilichokuwa kikisubiri kugawiwa, kuwapiga wafanyakazi wa kantini, kuharibu majokofu na kushambulia mabasi yapitayo eneo la chuo na hata yale yanayotoa huduma za usafiri kwa wanafunzi wanaoishi katika hosteli ya Mabibo.

Kuhusu uharibifu wa mali, tayari wamefungua jalada Polisi na kwamba kwa vile wanafunzi waliohusika wanafahamika watawajibika katika hilo.
Source Habarileoonline
Posted by MROKI On Thursday, December 15, 2011 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo