Nafasi Ya Matangazo

December 15, 2011

KIWANGO cha ufaulu kwa wanafunzi waliomaliza elimu ya msingi mwaka huu kimeongezeka kwa asilimia 4.76 kulinganisha na mwaka jana, huku ufaulu kwa masomo ya Sayansi, Kiingereza na Hisabati ukiongezeka.

Aidha, asilimia 90.1 ya wanafunzi waliofaulu wamechaguliwa kujiunga na sekondari huku waliofaulu katika mikoa tisa wote wakichaguliwa, wakati baadhi ya mikoa ikiwaacha baadhi ya wananchi ukiwemo Dar es Salaam ambao wanafunzi 7,000 wamekosa nafasi.

Akitangaza matokeo hayo Dar es Salaam jana, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo alisema wanafunzi 567,567 kati ya 983,545 waliofanya mtihani wamefaulu ambayo ni sawa na asilimia 58.28.

Mulugo alisema kati ya hao, wasichana ni 278,377 na wavulana 289,190 pamoja na wanafunzi wenye ulemavu 355 ambao ukilinganisha na mwaka jana, ufaulu umepanda kwa asilimia 4.76 kutoka asilimia 53.52.

Akizungumzia ulinganisho wa ufaulu kimasomo, Mulugo alisema kiwango cha ufaulu kwa somo la Kiingereza kimepanda kwa asilimia 10.23 huku Sayansi kikipanda kwa asilimia 5.28 na Hisabati asilimia 14.66.

Alisema katika masomo ya Kiswahili, kiwango cha ufaulu kimeshuka kwa asilimia 2.44 huku Maarifa ya Jamii ikishuka kwa asilimia 13.16.

“Pamoja na takwimu kuonesha kiwango cha ufaulu kinaongezeka, inasikitisha kuona kiwango cha udanganyifu mwaka huu kimeongezeka ikilinganishwa na mwaka jana na tayari changamoto hii imeanza kufanyiwa kazi,” alisema Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi.

Alisema kutokana na udanganyifu huo, Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) limefuta matokeo yote ya watahiniwa 9,736 ambao ni sawa na asilimia 1.0 kati yao, wavulana wakiwa 4,943 na wasichana 4,793.

Alisema kulikuwa na aina nne za udanganyifu ambapo wanafunzi 94 walikutwa na karatasi zenye majibu, rula na viatu vilivyoandikwa herufi za majibu, wanne waliandikiwa majibu, tisa walikariri darasa la saba na 9,629 walifanana katika maswali waliyokosa.

“Serikali imedhamiria kuwabaini waliohusika katika udanganyifu na kuwachukulia hatua pamoja na kuzichukulia hatua za kinidhamu shule zilizohusika katika udanganyifu,” alisisitiza Naibu Waziri.

Aidha, wanafunzi 515,187 sawa na asilimia 90.1 ya waliofaulu wamechaguliwa kuingia kidato cha kwanza kwa alama za juu za ufaulu kwa wavulana wakiwa 239 na wasichana 233 kati ya 250 huku alama ya chini kuchaguliwa ikiwa 100.

Kati ya wanafunzi hao, wasichana ni 253,402 ambao ni sawa na asilimia 49.1 na wavulana 261,785 sawa na asilimia 50 .9 ya waliochaguliwa idadi ambayo imeongezeka kwa asilimia 12.49 kutoka wanafunzi 456,350 wa mwaka jana.

Alisema ili kuwabaini wadanganyifu waliopita kwa njia mbalimbali, Serikali imeamua kuwa wale watakaojiunga elimu ya sekondari mwakani, watafanya mtihani wa majaribio kupima stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu kabla ya kuanza masomo rasmi.

Alisema mwanafunzi atakayebainika kujiunga na kidato cha kwanza bila ya kumudu stadi hizo, mwalimu wa shule ya msingi alikotoka, mwanafunzi huyo na Msimamizi wa Mtihani wa kumaliza elimu ya msingi watachukuliwa hatua za kinidhamu.

Aidha, Naibu Waziri alisema ajira kwa walimu wa ngazi mbalimbali ziko tayari na zingetangazwa muda wowote ila wanasubiri shule zifunguliwe Januari ili kuongeza nguvu ya walimu katika shule za kata zinazokabiliwa na changamoto hiyo.

Alisema kutokana na uhakika wa hilo, tayari na fedha maalumu kwa walimu watakaoenda kwenye mikoa au vijiji vyenye mazingira magumu ziko tayari.

Naye, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Selestine Gesimba akizungumzia madai ya walimu, alisema madai hayo yataanza kulipwa mwezi huu na kumalizia mwezi ujao.

Gesimba alisema uhakiki wa madai hayo ulimalizika Desemba 2, mwaka huu na kubaini kuwa walimu wanadai jumla ya Sh bilioni 52 ambazo Sh bilioni 30 ni madeni ya mishahara na Sh bilioni 22 ni madeni mengine.

Alisema baada ya kupeleka uhakiki huo kwa Katibu Mkuu Kiongozi, aliagiza kuwa malipo ambayo siyo mshahara yalipwe mwezi huu wa Desemba na yale ya mshahara yalipwe mwezi ujao.

Gesimba alisema Katibu Mkuu Kiongozi alishauri hivyo ili kuwezesha malipo ya mshahara yaingizwe katika malipo ya mwezi na kukatwa malipo yanayokwenda kwenye mifuko ya jamii.
Posted by MROKI On Thursday, December 15, 2011 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo