RAIS Jakaya Kikwete (pichani) kesho, Oktoba 17, 2011, anatarajiwa kuwasili wilayani Mpanda mkoani Rukwa kuzindua mkutano mkubwa wa uwekezaji wa Kanda ya Uwekezaji ya Ziwa Tanganyika (Lake Tanganyika Investors’ Forum).
Mkutano huo wa siku moja ulioitishwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda unalenga kuinua Kanda ya Uwekezaji ya Ziwa Tanganyika ambayo inaihusisha mikoa ya Rukwa, Kigoma na mkoa mpya wa Katavi ambayo yote mitatu imejaaliwa maliasili nyingi zikiwemo madini, vivutio vya utalii, ardhi nzuri ya kilimo na maeneo ya uvuvi.
Waziri Mkuu Pinda anaondoka jijini Dar es Salaam leo, Jumapili, Oktoba 16, 2011, kwenda Mpanda mkoani Rukwa kushiriki mkutano huo wa uwekezaji.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, mara baada ya kuwasili Rais Kikwete atapokelewa na Waziri Mkuu na kisha kuelekea Ikulu ndogo ambako atasomewa taarifa ya mkoa huo.
Baadaye ataelekea ukumbi wa mkutano na kutembelea mabanda ya maonesho kabla ya kuufungua rasmi mkutano huo. Rais Kikwete ambaye ni mgeni rasmi katika mkutano huo, anatarajiwa pia kuzindua tovuti rasmi ya ukanda wa Ziwa Tanganyika na kutazama filamu maalum iliyoandaliwa kwa ajili ya washiriki wa mkutano huo.
Mada tatu zinazoelezea fursa za uwekezaji, uzoefu walionao watendaji wa mikoa hiyo mitatu na jinsi ya kupata fedha za uwekezaji zitawasilishwa na kujadiliwa na washiriki wa mkutano huo wapatao 300.
Akizungumza kwa njia ya simu juu ya maandalizi ya mkutano huo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa, Bw. Salum Chima amesema kila kitu kiko tayari na kwamba tangu jana (Oktoba 15, 2011) wameanza maonesho ya fursa za uwekezaji katika mikoa hiyo mitatu. Maonesho hayo yatakamilika kesho kutwa (Jumanne, Oktoba 18, 2011).
Amesema mabalozi 34 wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini wamethibitisha kushiriki mkutano huo. Aliwataja wengine kuwa ni makampuni ya simu, mabenki, Wakuu wa Mikoa saba na makampuni mawili ya uchimbaji mafuta.
Mkutano huo ni wa kwanza wa aina yake wenye lengo la kutangaza fursa za uwekezaji katika mikoa hiyo na nchi kwa ujumla. Waalikwa ni wawekezaji wa ndani na nje wenye nia ya kuwekeza.
Kwa muda mrefu, mikoa hiyo ilikuwa ikikabiliwa na vikwazo vya kuvutia uwekezaji kama vile ukosefu wa miundombinu ya uhakika ya barabara, reli, bandari, viwanja vya ndege, umeme na maji.
0 comments:
Post a Comment