Nafasi Ya Matangazo

September 05, 2011

MWANARIADHA Godfrey Chacha  wa Mara jana aliibuka mshindi wa mbio za Rock City Nusu Marathon 2011 upande wa wanaume akiwapiku wenzake zaidi ya 100 kwenye mbio hizo zilizofanyika  jijini Mwanza.

 Chacha alitumia muda wa 61.03.44 na kutwa nafasi hiyo, wakati upande wa wanawake Jackline Juma kutoka Arusha alitwaa ushindi wa kwanza akitumia muda wa 1:15.22 baada ya kuwashinda wenzake  30.

 Kwa upande wa mbio za Kilometa tano wanaume Mohammed Gulle wa Arusha  aliibuka kidedea akiwashinda Dotto Ikangaa, pia kutoka Arusha na Pascal Ramadhan  wa Singida.

 Mgeni rasmi katika mbio hizo, ambazo zilishirikisha wanariadha kutoka mikoa mbalimbalia ya Tanzania na nchi za Kenya , Rwanda Afrika Kusini , Canada na Australia, alikuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Liberatus Balo.

 Akizungumza baada ya kukabidhi zawadi, alisema amefurahishwa na juhudi za sekta binafsi katika kuinua na kuhamasisha michezo nchini na kuomba  kampuni nyingi zaidi zijitokeze kufanya hivyo pia.

 "Michezo inaweza kuwa mojawapo ya vyanzo vya kupata  kipato na kusaidia vita dhidi ya umaskini endapo tu  sekta binafsi itajihusisha zaidi kusaidia kuinua na kupromoti michezo," alisema Balo.

 Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama cha riadha Tanzania (AT), Suleiman Nyambui alisema mbio za Rock City Marathon  zimeonesha mafanikio makubwa kadiri miaka inavyosonga mbele.

 "Ninajivunia mbio hizi na nina hakika mustakabali wake ni  mzuri mno katika siku zijazo," alisema Nyambui.

 Washindi wa mbio za kilometa 21 walijinyakulia medali pamoja na shilingi  500,000 kila mmoja  wakati washindi wa pili waliondoka na shilingi 300,000 kila mmoja  na wale walioshika nafasi ya tatu  walizawadiwa shilingi 200,000   huku washindi wa nafasi  ya nne hadi 12 kila mmoja alitapata shilingi 90,000 wakati  walioshika nafasi za 13 hadi 50  walipata shilingi 30,000 kama kifuta jasho.

 Washindi wa mbio za kilometa tano  na tatu nao pia walizawadiwa medali pamoja na fedha taslimu.

Mbio  za Rock  City zilizoanzishwa mwaka  2009  zikiandaliwa na kampuni ya Capital-Plus International (CPI), inayojishughulisha na masuala mbalimbali ya mawasiliano yenye makao yake jijini Dar es Salaam zilidhaminiwa na kampuni ya simu za mkononi ya  Airtel, Geita Gold Mine, Shirika la ndege Tanzania (ATCL),  Mfuko wa Pensheni wa Shirika ya Umma (PPF), Bank M, MOIL, Mfuko wa Taifa wa  Hifadhi ya  Jamiii (NSSF), New Mwanza Hotel, pamoja na Bodi ya Utalii Tanzania(TTB).  
Posted by MROKI On Monday, September 05, 2011 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo