Nafasi Ya Matangazo

March 28, 2011

JUMAMOSI ya Machi 26, 2010, unaweza kusema ilikuwa ni ‘Siku mwaka wa msanii 20%’, kutokana na nyota yake kung’ara vilivyo katika hafla ya hitimisho la kuwatuza wanamuziki waliofanya vema mwaka 2010 Tanzania, maarufu kama Kilimanjaro Music Awards.


Msanii huyo alifanikiwa kunyakua tuzo tano pekee yake na kuvunja rekodi kwa wasanii wote ambao waliingia kwenye kinyang’anyiro cha kuwania tuzo hizo zilizofanyika kwa mara ya 12 mwaka huu, tangu zilipoasisiwa.

Katika hafla hiyo ya utoaji wa tuzo, 20% aling’ara kwa kupata tuzo hizo tano, huku ikiwa ni tukio la mara ya kwanza kwa msanii kung’ara kama ilivyotokea kwake katika historia ya tuzo hizo.

Onyesho hilo ambalo lilikuwa likionyeshwa moja kwa moja na kituo cha runinga cha ITV, zilifanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.

Mashabiki wengi walionekana kumshangilia 20% kila jina au wimbo wake ulipokuwa ukitajwa, taswira iliyoonyesha kwamba, anakubalika vilivyo katika jamii kwa ujumla na alistahili kutwaa tuzo hizo.


Tuzo alizonyakua msanii huyo ni; Msanii Bora wa Kiume, ambako katika kundi hilo walikuwamo pia, Barnaba, Ali Kiba, Banana, Belle 9 na Diamond.

Tuzo yake ya pili ni Wimbo Bora wa mwaka, ambako aliibuka kidedea kupitia wimbo wake wa ‘Tamaa Mbaya’, na kuzibwaga nyimbo zifuatazo na watunzi kwenye mabano; ‘Mama Ntilie’ (Gelly wa Rhymes Feat AT &Ray C), ‘Sina Raha’ (Sam wa Ukweli), ‘Mkono Mmoja’ (Tip Top Connection), na wimbo wake mwenyewe, ‘Yanini Malumbano’.


Mashabiki walichanganyikiwa zaidi, pale msanii huyo alipotajwa kunyakua tuzo ya tatu ya Mwimbaji Bora wa Kiume, ambako alikuwa akichuana na Barnaba, Ali Kiba, Belle 9 na Diamond.


Kama haitoshi, 20% pia aling’ara katika Wimbo Bora wa Afro Pop kupitia wimbo wake wa ‘Yanini Malumbano’, na kuzibwaga ‘Mama Ntilie’ ulioimbwa na Gelly wa Rhymes Feat AT &Ray C, ‘Oyoyo’ wa Bob Junior, ‘Tamaa Mbaya’ wa kwake mwenyewe na ‘Mbagala’ ulioimbwa na Diamond.

Baada ya msanii huyo kung’ara vilivyo katika makundi hayo, bendi mpya ya Mapacha Watatu inayoundwa na wasanii Khalid Chuma ‘Chokoraa Tora Bora’, Kalala Hamza ‘Kalala Junior’ na Jose Mara walichukua tuzo ya Wimbo Bora wa Kiswahili wa bendi kwa kibao chao ‘Shika Ushikapo’ na kuwashinda wakongwe The African Stars ‘Twanga Pepeta’ ambao walitupa karata mbili ambazo ni ‘Kauli’ na ‘Mapenzi Hayana Kiapo’, FM Academia na wimbo wao ‘Shida Yangu’ na Akudo Impact kwa kibao chao ‘Pongezi kwa Wanandoa’.


Aidha Tuzo ya Rapa bora ilinyakuliwa na Chokoraa kutoka bendi hiyo ya Mapacha Watatu, huku ikiwa ni kwa mara ya pili kwa msanii huyo, kwani mwaka jana ndiye aliyechukua tuzo hiyo.


Tuzo ya mwimbaji bora wa kike ilikwenda kwa ‘Ndege Mnana’ Lina Sanga ‘Lina’ aliyekuwa akichuana na Judith Wambura ‘Lady Jay Dee’, Mwasiti Almasi ‘Mwasiti’, Khadija Kopa na Sara Kaisi ‘Shaa’.


Kadhalika tuzo nyingine ya tatu aliyopata Lina ni Msanii Mpya Anayechipukia, ambapo wengine waliokuwa wakiwania ni Sajna, Bob Junior, Top C na Sam wa Ukweli.


Kama kawaida yake kushinda, kundi la Jahazi Modern Taarab lilitwaa tuzo ya wimbo bora wa Taarab kupitia wimbo wao unaokwenda kwa jina la ‘My Valentine’.


Tuzo ya wimbo bora wa R & B, imekwenda kwa wimbo wa ‘Nikikupata’ wa Ben Paul, na kuzibwaga ‘We ni Wangu’ wa Belle 9, ‘Hello’ Hussein Machozi FT Maunda Zorro.


Msanii Joh Makini almaarufu kama ‘Mwamba wa Kaskazini’ alichanua kwa kupata tuzo ya wimbo bora wa Hip Hop kwa wimbo wake wa ‘Karibu Tena’, na kuziacha solemba ‘Propaganda’ wa Fid Q, ‘Ukisikia Paah’ JCB Feat Fid Q &Chid Benz, ‘Usije Mjini’ wa AY & Mwana FA na ‘Higher’ wa Nick wa Pili Feat Joh Makini.


Joh Makini, aling’ara tena katika tuzo ya msanii bora wa Hip Hop ambako aliwabwaga Fid Q, Ngwear, Chid Benz na Godzilla.


Tuzo ya Mtayarishaji Bora wa mwaka ilikwenda kwa Lamar aliyewashinda Marco Chali, Man Water, Bob Junior na Pancho Latino, huku Wimbo Bora wa Afrika Mashariki ni ‘Nitafanya’ ulioimbwa na Kidumu na Lady Jaydee.


Nyimbo zingine zilizokuwa zikiwania ni ‘Kare’ wa P-Unit, na ‘Songambele’ wa Alpha.


Katika miondoko ya kunesanesa msanii Hard Mad aling’ara kwa kupitia wimbo wake wa ‘Ujio Mpya’ aliomshirikisha Enika &BNV, na kuzishinda ‘Sauti ya Rasta’ wa Ras Rwanda Magere, ‘Misingi ya Rasta’ wa Warriors From East, ‘Sayuni’ wa Jhiko Man, ‘Reggae Swadakta’ ulioimbwa na Bob Lau Mwalugaja na ‘What U Feel Inside’ wa Hard Mad.


Wimbo ‘Action’ wa CPWAA, aliomshirikisha Dully, Ngwear na Ms Trinity ulichukua tuzo ya Wimbo bora wa Ragga/Dancehall, na kuzishinda ‘Far Away’ wa Big Jah Man feat Richard, ‘My Friend’ wa Benjamin na ‘Kiune Weka Busy’ wa Jet Man.


Katika hali isiyotarajiwa baada ya kutoa wimbo mmoja tu, msanii wa vichekesho Mpoki au unaweza kumwita Mwarabu wa Dubai, amenyakua Wimbo Bora wa Asili wa Tanzania, kupitia wimbo wake wa ‘Shangazi’ na kuzishinda ‘Adela’ ulioimbwa na Mrisho Mpoto, ‘Kariakoo’ wa Mataluma, ‘Ahmada’ wa Offside trick waliomshirikisha Bi. Kidude, na ‘Wa Mbelembele’ wa Ommy G.


Video Bora ya Muziki ilikwenda kwa wimbo wa ‘Action’ wa CPWAA, Dully, Ngwear na Ms Trinity na kuzishinda ‘Mbagala’ ya Diamond, ‘Mkono Mmoja’ ya Chegge & Temba Feat Wahu na ‘Shoga’ wa Shaa.


Tuzo ya Wimbo Bora wa Zouk-Rhumba imekwenda kwa Barnaba na kibao chake ‘Nabembelezwa’ na kuzibwaga ‘Bado Robo Saa’ wa Amini, ‘Bona Nikimbie’ wa Linah, ‘Ulofa’ wa Top C na ‘Sina Raha’ wa Sam wa Ukweli.


Mwanamuziki Mkongwe, Said Mabera kutoka Msondo Ngoma ‘Baba ya Muziki’ ametunukiwa tuzo ya heshima ‘Hall Of Fame’huku Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), wakipata tuzo ya taasisi iliyochangia mafanikio katika kuhifadhi muziki wa Tanzania.

Tuzo hizi ziliratibiwa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), na kudhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia Bia ya Kilimanjaro Premium Lager.

Source Tanzania Daima
Posted by MROKI On Monday, March 28, 2011 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo