Tangu mwaka 1964 wakazi wa kata ya Maiella ambao ni kabila la wamasai na wakikuyu katika wilaya ya Naivasha mkoa wa Rift valley nchini Kenya wamekuwa wakigombania ardhi katika shamba la Ng’ati lenye ukubwa wa hekta 16,000 kwa ajili ya malisho, kilimo na maji jambo lililosababisha watu wengi kupoteza maisha.
Hayo yamesemwa hivi karibuni na Mkuu wa wilaya Msaidizi wa Naivasha Timothy Nderitu wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya jinsi ya kuleta amani, upatanishi na kuheshimu haki za binadamu kwa viongozi wa vikundi vya kutunza amani yaliyoandaliwa na chama cha waandishi wa habari wanawake nchini Kenya (AMWIK) ambayo yalifanyika katika hoteli ya Lakeside.
Mkuu wa wilaya huyo msaidizi alisema kuwa makabila hayo wanagombania ardhi ambayo wakikuyu waliinunua kutoka kwa wakoloni mwaka 1963 na kuwakodisha wamasai kwa ajili ya kulisha na kuogesha mifugo lakini hivi sasa kila kabila linadai kuwa ardhi hiyo ni mali yao ndipo walipopeleka kesi mahakama kuu ya Nairobi ambayo ilitoa uamuzi Octoba mwaka jana kuwa wamasai wapewe hekta 4207 na wakikuyu wapewe hekta zilizobaki.
Nderitu alisema, “Kutokana na uamuzi wa mahakama kila kabila lilikubaliana na agizo hilo kwani wananchi hao wamepitia matatizo makubwa ikiwa ni pamoja na kupoteza ndugu pamoja na mali zao. Tayari Serikali imeshapima ardhi hiyo na itaanza kuigawa siku chache zijazo”.
Nderitu pia aliwataka wakati wa kata hiyo kuachana na tabia ya kubaguana kutokana na tofauti zao za makabila ili kuepuka mapigano ya mara kwa mara yanayotokea na kusababisha vifo vya wananchi wasio na hatia.




0 comments:
Post a Comment