Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe (kulia) akizungumza katika kikao na Idara ya Misitu na Nyuki pamoja na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika ukumbi wa Ngorongoro Makao Makuu wa Wizara hiyo Mpingo House Jijini Dar es Salaam leo Januari 5, 2015. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Meja Jenerali Gaudence Milanzi.
Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe akizungumza katika kikao na Idara ya Misitu na Nyuki pamoja na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika ukumbi wa Ngorongoro Makao Makuu wa Wizara hiyo Mpingo House Jijini Dar es Salaam leo.
Kaimu Mkurugenzi Idara ya Misitu na Nyuki Bi. Gladnes Mkamba akiwasilisha taarifa ya Idara yake kwa Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe wa (pili kushoto) katika kikao hicho.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Bw. Juma Mgoo (kulia) akiwasilisha taarifa ya ofisi yake kwa Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe (wa tatu kulia).
Sehemu ya wajumbe wa kikao hicho wakimsikiliza Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe. TAARIFA ZAIDI BOFYA HAPA
Sehemu ya wajumbe katika kikao hicho.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Meja Jenerali Gaudence Milanzi (wa pili kulia) akizungumza katika kikao hicho.
*****************
Waziri wa Maliasili na Utalii
Prof. Jumanne Maghembe amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Mipango na Matumizi
Endelevu ya Rasilimali za Misitu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Bw.
Mohammed Kilongo na Maofisa wa Misitu wa Mikoa nchi nzima kupisha uchunguzi wa
upotevu wa mapato ya Serikali.
Akizungumza leo na Waandishi wa
Habari Makao Makuu ya Wizara hiyo Dar es Salaam, Prof. Maghembe amesema agizo
hilo limekuja kutokana na ubadhilifu unaofanywa na Maofisa wa ukusanyaji wa
maduhuri ya Serikali yanayotokana na rasilimali za misitu katika Mikoa na
Wilaya kwa kutowasilishwa katika mfuko Mkuu wa Serikali.
Ameagiza pia maofisa hao wote
wanaokusanya maduhuri ya Serikali katika Wilaya watumie muda wa siku kumi kuanzia
leo kuhakikisha maduhuri yote yaliyokusanywa yanapelekwa benki ikiwa ni pamoja na
kukabidhi vitabu vya kukusanyia mapato kinyume cha hapo watachukuliwa hatua
kali za kisheria.
“Wale district forestry officers
wote wapeleke vitabu vyao wanavyokusanyia maduhuri ya Serikali kwenye ofisi za
Kanda, Naibu Katibu Mkuu tusaidie kuwasiliana na Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa
Serikali ifanye ukaguzi wa vitabu hivyo ndani ya siku kumi tuhakikishe fedha
zinazotakiwa zinaingia kwenye mfuko wa Serikali, Mtu anakusanya fedha ya Serikali toka mwaka 2004 mpaka leo hajapeleka
benki ananeemesha hali yake ya nyumbani, hili hapana”. Alisisitiza Prof.
Maghembe.
Kwa mujibu wa Waziri Maghembe Bw.
Mohammed Kilongo ambaye Idara yake ndiyo inatoa vitabu kwa ajili ya kukusanya
maduhuri ya Serikali katika Mikoa yote na Wilaya zote nchini analazimika
kusimamishwa kazi kupisha uchunguzi ambapo ukikamilika sheria itachukua mkondo
wake bila uonevu wowote.
Katika hatua nyingine Waziri huyo
wa Maliasili na Utalii amewaagiza pia Wakala wa Huduma za Misitu nchini (TFS)
kutumia muda wa siku saba kurudi katika jengo la Wizara ya Maliasili na Utalii
maarufu kama Mpingo House ambalo walihama mwishoni mwa mwezi Septemba mwaka
jana na kwenda kupanga katika jengo la NSSF Mafao House lililopo Ilala.
“Wakati tunajenga nyumba hii
hapa, tumejenga jengo hili ni kama jengo la misitu ndio maana linaitwa Mpingo
House kwa maana ni jengo la Misitu, ninyi wenyewe mmejenga jengo kubwa hili mmemaliza
mmehama, Naagiza jumatatu Desemba 11 muwe mmesharudi katika jengo hili, ghorofa
ya tatu nikija kukagua niwakute, haiwezekani mueleze matatizo yote mliyonayo
muhame nyumba ya Serikali mkapange jengo hapo jirani” Alisema Prof. Maghembe.
Katika hatua nyingine ya kuboresha
uhifadhi wa Misitu nchini Waziri Maghembe ameiagiza Idara ya Misitu na Nyuki ya
Wizara ya Maliasili kuhakikisha inajiimarisha katika lengo lake kuu la uhifadhi
kwa kushirikiana na wadau wanaohusika kuhakikisha Mamlaka iliyolengwa ya Uhifadhi
Misitu inakamilika.
“Tunataka tutoke kwenye Wakala wa
Huduma za Misitu (Tanzania Forestry Services Agency) twende kwenye Mamlaka ya
Uhifadhi wa Misitu (Tanzania Forestry Services Authority) ili tuweze kufanya
vizuri zaidi kwenye eneo la uhifadhi na uendelezaji wa misitu nchini, Katibu
Mkuu tunaomba pia usaidie kufanikisha hili” Alisema Prof Maghembe.
Aliongeza kuwa wakati wa kuundwa
Mamlaka hiyo ni vizuri pia Idara ya Misitu na Nyuki ya Wizara ya Maliasili ikatenganishwa
na kila moja kuwa Idara kamili kutokana na umuhimu wa kila sekta katika kujenga
uchumi wa nchi kwa kutoa fursa ya kuboresha maeneo hayo na kuongeza pato la
taifa.
Ameitaka pia Idara ya Misitu na
nyuki kupitia Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) kuhakikisha kuwa inaongeza
ukusanyaji wa mapato ya Serikali kwa kuziba mianya yote ya ubadhilifu pamoja na
kuanzisha vyanzo vipya vya mapato na kuboresha vyanzo vilivyopo.
Akizungumzia mchango wa Wakala wa
Huduma za Misitu (TFS) kwenye pato la taifa Mtendaji Mkuu, Bw. Juma Mgoo
amesema katika mwaka huu wa fedha TFS imeweka makisio ya kukusanya Tsh. Bilioni
88 ambapo mpaka hivi sasa wameshakusanya zaidi ya asilimia 20 na makisio hayo.
Waziri Maghembe akizungumzia
kuhusu uvamizi kwenye hifadhi za taifa na mapori ya akiba amewataka wananchi
wote waliovamia maeneo ya hifadhi za taifa kwa ajili ya kuchunga mifugo waondoke
ndani ya siku saba zijazo, na wale walivamia mapori ya akiba kwa shughuli za
kilimo na ufugaji waondoke ndani ya miezi mitatu ijayo.
"Serikali itawaondoa kwa nguvu wasipotekeleza
agizo hili la kuondoka katika maeneo ya hifadhi za taifa na kwenye mapori ya
akiba yaliyohifadhiwa” Alisisitiza Prof. Maghembe.
Akizungumzia kuhusu biashara ya
Mkaa, Prof. Maghembe amewaagiza wataalamu wa Idara ya Misitu kusimamia biashara
ya mkaa kwa kuzingatia taratibu na sheria ikiwa ni pamoja na kuzuia
usafirishaji wa Mkaa nje ya nchi.
Ameongeza kuwa nishati ya Mkaa ni
muhimu lakini Tanzania ina hifadhi kubwa ya makaa ya mawe ambapo ameitaka Idara
ya Misitu kwa kushirikiana na wadau wengine kuona ni namna gani ya kuweza
kutumia mbadala huo kwa kuzalisha makaa hayo ya mawe kwa matumizi ya kawaida ili
kuokoa misitu nchini.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa
Wizara hiyo Meja Jenerali Gaudence Milanzi amesema kuwa maagizo yote yaliyotolewa
na Waziri yatafanyiwa kazi kwakuwa lengo lake ni kuona dhamira ya msingi ya
Serikali ya awamu ya tano inafikiwa ya kubana matumizi, kuongeza mapato ya
Serikali na kuhifadhi maliasili za taifa ikiwemo misitu.
(Na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Maliasili na Utalii - www.wizarayamaliasilinautalii.blogspot.com)
0 comments:
Post a Comment