SURUA na rubella ni magonjwa
hatari yanayoenezwa haraka kwa njia ya hewa, kutoka kwa mtu mwenye vimelea vya
ugonjwa huo kwenda kwa mwingine.
Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa
dalili za magonjwa haya mawili zinafanana, hivyo ni vigumu kutofautisha. Wataalamu
hao wanasema dalili kuu ni homa na vipele vidogovidogo.
Chanjo ya surua-rubella hutoa
kinga kamili dhidi ya magonjwa haya. Dozi ya kwanza hutolewa kwa mtoto
anapofikia umri wa miezi 9 na dozi ya pili akiwa na mwaka mmoja na nusu (miezi
18).
Serikali kupitia Wizara ya Afya
na Ustawi wa Jamii, imekutana na wadau wake wa masuala ya chanjo jijini Dar es
Salaam jana, kuzungumzia mkakati wa kampeni za chanjo ulio na lengo la
kuwafikia walengwa wengi zaidi ili kuongeza idadi ya watu wenye kinga dhidi ya
magonjwa ya surua na rubella.
Akizungumza katika mkutano huo wa
wadau wa chanjo, Meneja Mpango wa Chanjo wa Taifa, Dk Dafrossa Lyimo, alisema
kampeni hii itajumuisha watoto wenye umri wa miezi tisa hadi chini ya miaka 15.
Dk Lyimo alitoa mwito kwa wadau
wote kushiriki kikamilifu katika kampeni hii nchini kote, kwa kujitokeza na
kuwapeleka watoto wetu katika chanjo kwa tarehe ambazo zimepangwa.
Kampeni hiyo imepangwa kufanyika kuanzia
Oktoba 18 hadi 24 mwaka huu katika vituo mbalimbali vya afya nchini ambavyo
hutoa huduma ya chanjo.
Mimi kama mzazi kwanza napenda
kuwasihi sana wazazi wenzangu tuwapeleke watoto wetu kupata chanjo hii maana
mara kwa mara tumekuwa tukiwapa tiba watoto wetu ya surua kumbe kinachowasibu
si surua ni rubella na matokeo yake ni madhara makubwa.
Ugonjwa wa rubella kwa watoto
huja na dalili za vipele vidogo vidogo, homa, macho kuwa mekundu, uchovu wa
mwili, vidonda kooni na uvimbe wa matezi na mafua.
Wataalamu wanasema madhara ya
ugonjwa huu ukimpata mama mjamzito, unaweza kusababisha kuharibika kwa mimba,
kuzaa mtoto njiti, au mfu. Pia mtoto akizaliwa anaweza kupata madhara kama
mtoto wa jicho, matatizo ya moyo, kutokusikia vizuri, mtindio wa ubongo,
kuvimba kwa ini na bandama na mengineyo kama ukuaji.
Surua yenyewe husababisha watoto
kuzaliwa na upofu, nimonia, utapiamlo, pia kifo kinaweza kutokea endapo mgonjwa
hatapata matibabu mapema.
Kama mwandishi, pia natumia fursa
hii kutumia kalamu yangu kuuelimisha umma juu ya utofauti wa magonjwa haya
mawili ambayo baadhi yetu katika jamii tunazotoka tumekuwa tukitumia mitishamba
kama kuwaogesha watoto walio na homa kali maji ya mchunga au mwarobaini.
Rubella mara nyingi huwapata
watoto wadogo na huenezwa kwa njia ya hewa, lakini watu wazima pia wanaweza kupata.
Shime wazazi na walezi hebu
tujitokeze na tusaidiane kwa pamoja kueneza elimu hii juu ya hiyo chanjo
inayokuja hapo baadae mwezi huu.
Ni wakati muafaka sasa wa
kutokomeza kabisa magonjwa haya katika jamii zetu na hili litawezekana tu pindi
tutakapowapeleka watoto wetu katika chanjo hii.
Katika mkutano huo wa wadau ikaelezwa
kuwa hata ile chanjo ya vitamin A pamoja na minyoo nazo zitatolewa pamoja na
chanjo hii.
Tunahimizwa na wataalamu wa
chanjo na afya kwa ujumla kuwa wazazi tuwapeleke watoto wetu kupata dozi mbili
za chanjo hii ya surua-rubella akitimiza umri wa miezi tisa na miezi 18.
Aidha, inaelezwa kuwa pasije
pakatokea mtu awaye yote akapotosha kuwa chanjo hii ina madhara. Chanjo ya Surua-rubella
ni salama na imethibitishwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Shirika la
Afya Duniani (WHO).
Lakini kubwa zaidi ambalo wengi
huweza kuhofia kujitokeza kupata chanjo hii wakidhani ina malipo, la hasha
chanjo hii haina malipo na itatolewa bure hivyo kila mwananchi aliye na mtoto
wa umri huo ajitokeze kumpeleka mtoto wake.
*Porojo hii ya Anko Kidevu pia imetoka katika gazeti la Habarileo Toleo la Oktoba 7,2014 .
0 comments:
Post a Comment