Nafasi Ya Matangazo

October 16, 2026


MBEYA
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amewataka viongozi na watendaji wa Sekta ya Maji kuhakikisha Mradi wa Kimkakati wa Maji kutoka Mto Kiwira, wenye thamani ya Shilingi bilioni 119, unatekelezwa kwa kasi na ufanisi ili kufikia Julai 2027 wananchi wa Mkoa wa Mbeya waondokane na changamoto za upatikanaji wa majisafi.
 
Makamu wa Rais ametoa agizo hilo leo, Oktoba 16, 2026, wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo katika eneo la Forest Mpya, Jijini Mbeya, ambako Serikali inajenga tenki kubwa lenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni tano za maji.
 
Akizungumza na viongozi na wananchi, Mhe. Ndejembi amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kubadilisha maisha ya Watanzania kwa kuhakikisha huduma muhimu za kijamii, ikiwemo majisafi, zinapatikana kwa uhakika.
 
Amesisitiza kuwa Mbeya ni mkoa wa kimkakati katika uchumi wa Taifa, hivyo upatikanaji wa maji ya uhakika ni jambo la msingi katika kuchochea shughuli za uzalishaji, biashara na maendeleo ya wananchi.
 
Aidha, Makamu wa Rais amewataka watendaji wa Serikali kusimamia kikamilifu fedha zinazotolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo, akisisitiza maelekezo ya Rais Samia ya kuhakikisha kila shilingi inayowekezwa inaleta thamani halisi na matokeo yanayoonekana kwa wananchi.
 
Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso, amemhakikishia Makamu wa Rais kuwa Wizara itaendelea kuhakikisha utekelezaji wa mradi huo haukwamishwi, huku akiwataka watendaji na wataalamu kuongeza kasi na kuimarisha usimamizi ili mradi ukamilike kwa ubora na wakati.
 
Kwa mujibu wa taarifa ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mbeya (Mbeya UWSA), mradi huo umefikia asilimia 49 ya utekelezaji, ambapo ujenzi wa banio la maji umefikia asilimia 98, tenki la kuhifadhi maji katika eneo la Forest Mpya asilimia 80, huku ulazaji wa bomba kuu la kusafirisha maji ukifikia asilimia 15.
 
Mradi huo unatarajiwa kuongeza uzalishaji wa maji kwa lita milioni 116 kwa siku, na hivyo kupandisha uwezo wa jumla wa uzalishaji kutoka lita milioni 78 hadi milioni 195 kwa siku, hatua itakayowezesha kuhudumia wananchi wengi zaidi ifikapo mwaka 2045.
 
Kukamilika kwake kunatarajiwa kuongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya majisafi kutoka asilimia 90 hadi asilimia 100, pamoja na kuhakikisha wananchi wanapata maji kwa saa 24 kwa siku, hivyo kuimarisha ustawi wa jamii na kuchochea ukuaji wa uchumi katika Jiji la Mbeya, Mji wa Mbalizi na maeneo jirani.

 






Posted by MROKI On Friday, October 16, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo