Nafasi Ya Matangazo

June 04, 2026

WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali inafanyia kazi mapitio ya sheria inayosimamia uchaguzi wa Naibu Meya na Makamu Wenyeviti wa Halmashauri kwa lengo la kuondoa migogoro na kuongeza ufanisi katika utendaji wa halmashauri nchini.

Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi, Juni 4, 2026 Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la papo kwa papo la Mbunge wa Segerea, Mhe. Agenesta Lambert Kaiza, ambaye alitaka kujua kama Serikali ina mpango wa kurekebisha utaratibu wa uchaguzi wa Naibu Meya na Makamu Wenyeviti wa Halmashauri unaofanyika kila mwaka na kusababisha migawanyiko pamoja na kuathiri utendaji wa halmashauri.

"Ni kweli jambo hili limekuwa chanzo cha migogoro katika baadhi ya halmashauri. Badala ya viongozi kujikita katika kutekeleza majukumu yao, muda mwingi unatumika katika kampeni na uchaguzi wa mara kwa mara. Serikali imeona mantiki ya kuliangalia upya suala hili," amesema Dkt. Mwigulu.

Amesema tayari amemuelekeza Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kulifanyia kazi suala hilo ili kuandaa mapendekezo ya marekebisho ya sheria yatakayowasilishwa Bungeni kwa hatua zaidi.

Aidha, Waziri Mkuu amewataka viongozi wa halmashauri kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maslahi ya wananchi badala ya kujikita katika kampeni za uchaguzi wa ndani ya halmashauri.

"Uchaguzi si kazi. Kazi ni kuwaletea wananchi maendeleo. Tusiwe na nchi inayowaza uchaguzi kila siku badala ya kutatua changamoto za wananchi," amesema.

Katika swali jingine, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa wawekezaji wa ndani na nje huku ikiweka mkazo katika kujenga uwezo wa sekta binafsi inayomilikiwa na Watanzania.

Kauli hiyo ameitoa wakati akijibu swali la papo kwa papo la Mbunge wa Kikwajuni, Mhe. Ally Hassan Omary King, ambaye alitaka kujua mkakati wa Serikali wa kuwawezesha wawekezaji wa ndani bila kuweka vikwazo kwa wawekezaji wa nje, kwa kuzingatia mchango wa uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje katika kukuza uchumi wa Taifa.

"Tunahitaji uwekezaji wa ndani na wa nje. Lengo la Serikali si kuwazuia wawekezaji wa nje, bali kujenga mazingira yatakayowezesha Watanzania kushiriki kikamilifu katika shughuli za uwekezaji na utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo," amesema Dkt. Mwigulu.

Amesema Serikali imeendelea kutoa vivutio mbalimbali kwa wawekezaji wa nje sambamba na kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji wa ndani ili washiriki kikamilifu katika shughuli za uwekezaji na uzalishaji.

Aidha, amesema Serikali imeanzisha dirisha maalum kwa wawekezaji wa ndani na kushusha kiwango cha chini cha mtaji kinachohitajika kwa wawekezaji hao ili kuongeza ushiriki wa Watanzania katika shughuli za uwekezaji.

"Mheshimiwa Rais ameelekeza tusitazame ugeni peke yake, bali tujenge uwezo wa sekta binafsi ya ndani ili Watanzania nao wanufaike na fursa za uwekezaji na utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo," amesema.
Posted by MROKI On Thursday, June 04, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo