Nafasi Ya Matangazo

May 07, 2026

Serikali imeendelea kuweka mikakati madhubuti ya kukuza ubunifu, utafiti na matumizi salama ya teknolojia ya kisasa ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.

Hatua hiyo inalenga kuongeza uwezo wa wananchi, taasisi za elimu pamoja na sekta mbalimbali kutumia teknolojia kwa tija na usalama zaidi.

Hayo yamebainishwa leo Mei 7,2026 bungeni Dodoma na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Katika juhudi za kukuza ubunifu, Serikali itaendeleza Mfuko wa Kibiashara wa Ubunifu  kwa lengo la kusaidia mawazo ya wabunifu na tafiti zenye manufaa kuingia kwenye matumizi ya kibiashara. Kupitia mpango huo, vyuo vitano vya Maendeleo ya Wananchi vitawezeshwa kuanzisha vituo vya ubunifu vitakavyotoa nafasi kwa vijana na wabunifu kukuza teknolojia, ujasiriamali na ajira.

“Serikali imejipanga kuimarisha uthibiti na utafiti wa kimkakati katika matumizi ya teknolojia ya nyuklia ili kuhakikisha usalama wa wananchi pamoja na mazingira. Mkakati huo unalenga kuongeza matumizi salama ya teknolojia hiyo katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii ikiwemo afya, kilimo na viwanda.”amesema Prof.Mkenda.

Katika mwaka ujao wa utekelezaji, Serikali itaendelea kudhibiti matumizi ya mionzi nchini kwa kufanya ukaguzi katika vituo 900 vyenye vyanzo vya mionzi. Ukaguzi huo unalenga kuhakikisha usalama wa wagonjwa, wafanyakazi, jamii pamoja na mazingira dhidi ya athari zinazoweza kusababishwa na matumizi yasiyo salama ya mionzi.

Vilevile, Serikali itapima na kudhibiti viwango vya mionzi kwa wafanyakazi 2,110 wanaofanya kazi kwenye mazingira yenye vyanzo vya mionzi ili kuhakikisha afya zao zinalindwa na viwango vya usalama vinafuatwa wakati wote.

Hatua hizi zinaonesha dhamira ya Serikali ya kuendelea kuwekeza katika sayansi, teknolojia na ubunifu kama nyenzo muhimu ya kuharakisha maendeleo ya taifa na kuboresha maisha ya wananchi. SOURCE : Mzalendo Blog
Posted by MROKI On Thursday, May 07, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo