Watumishi wapya 37 wa Tume ya Madini wametakiwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma, uwajibikaji na uzalendo katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuimarisha usimamizi wa Sekta ya Madini na kuongeza mchango wake katika Pato la Taifa. Wito huo umetolewa wakati wa ufunguzi wa mafunzo elekezi kwa waajiriwa hao kabla ya kuripoti katika vituo vyao vya kazi mbalimbali nchini.
Akizungumza katika Ofisi za Tume ya Madini Makao Makuu jijini Dodoma, Meneja wa Utawala wa Tume ya Madini, Jacob Mnyenyelwa, kwa niaba ya Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimaliwatu na Utawala, Nsajigwa Kabigi, amesema watumishi hao wanapaswa kuzingatia maadili ya kazi, weledi na uwazi wanapotoa huduma kwa wananchi na wadau wa sekta ya madini.
Amesema wananchi wana matarajio makubwa kutoka katika Sekta ya Madini, hivyo watumishi wapya wanapaswa kuwa mfano bora wa uadilifu, ubunifu na uzalendo ili kuhakikisha rasilimali madini zinasimamiwa kwa manufaa ya Taifa.
Amesisitiza kuwa utendaji wenye maadili utaongeza imani ya wananchi na wawekezaji katika sekta hiyo muhimu ya uchumi.
Mafunzo hayo yamewashirikisha wahandisi, mafundi sanifu pamoja na afisa TEHAMA, yakilenga kuwajengea uwezo kuhusu majukumu yao, misingi ya utumishi wa umma, mawasiliano ya kikazi na taratibu za utendaji ndani ya Tume ya Madini kabla ya kuanza majukumu rasmi.
Tume ya Madini imeendelea kuimarisha rasilimaliwatu kwa kuajiri wataalam wenye ujuzi mbalimbali ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuongeza ufanisi wa usimamizi wa shughuli za utafiti, uchimbaji na biashara ya madini nchini, hatua inayotarajiwa kuchochea ukuaji wa uchumi na maendeleo endelevu ya Taifa.











0 comments:
Post a Comment