Kamati ya Kitaifa ya Ufungaji Migodi imeendelea na vikao vyake kwa siku mbili katika Mgodi wa dhahabu wa Shanta uliopo mkoani Singida kwa lengo la kujadili na kupitia Mpango wa Ufungaji wa Mgodi huo ili kuhakikisha unazingatia matakwa ya Sheria ya Madini, Sura 123 na Kanuni za Usalama, Afya na Utunzaji wa Mazingira katika kufunga mgodi huo.
Akiongoza kikao hicho kilichowakutanisha wataalam kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Wizara ya Maji, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Madini, Tume ya Matumizi Endelevu ya Ardhi, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Tume ya Madini pamoja na viongozi wa Wilaya, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Ufungaji Migodi, Dkt. Abubakary Salama amesema migodi mikubwa na ya kati inalazimika kisheria kuandaa mipango ya ufungaji migodi.
Amesema kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Madini Sura ya 123 pamoja na Kanuni ya 206 ya Kanuni za Madini (Usalama, Afya na Utunzaji wa Mazingira) za Mwaka 2010, wamiliki wa migodi wanapaswa kuandaa mpango wa ufungaji mgodi na kuuwasilisha kwa Mkaguzi Mkuu wa Migodi kwa ajili ya mapitio ya kitaalam kabla ya kuidhinishwa na Kamati ya Kitaifa ya Ufungaji Migodi.
Kwa upande wake, Mshauri Mwelekezi kutoka kampuni ya MTL Consulting Company Limited, John Bosco Tindyebwa, amesema kampuni hiyo imefanikiwa kuandaa na kuwasilisha Mpango wa Ufungaji wa Mgodi wa Singida Gold Mine unaomilikiwa na Shanta Mining Company kwa ajili ya mapitio ya kitaalam na uidhinishaji wa Kamati hiyo.
Ameongeza kuwa kampuni ya MTL itaendelea kushirikiana kwa karibu na Tume ya Madini, Shanta Mining Company pamoja na wadau wengine muhimu wa sekta ya madini ili kuhakikisha mpango huo unazingatia viwango vinavyotakiwa, kulinda mazingira na kuacha manufaa endelevu kwa jamii zinazozunguka mgodi huo baada ya shughuli za uchimbaji kukamilika.
Naye Meneja Mkuu wa Mgodi wa dhahabu wa Singida, Juma Kisonda, ameihakikishia Kamati kuwa mgodi huo unaendelea kuzingatia masuala ya usalama, afya na utunzaji wa mazingira, akisisitiza kuwa uongozi wa mgodi utatekeleza maelekezo yote yatakayotolewa na Kamati ya Kitaifa ya Ufungaji Migodi ili kuhakikisha ufungaji wa mgodi unafanyika kwa kuzingatia viwango vinavyokubalika kitaifa na kimataifa.
















0 comments:
Post a Comment