Wizara ya Madini imetoa siku tatu kwa wachimbaji na wanunuzi wa madini ya jasi kuwasilisha mchanganuo wa gharama za uzalishaji ili kupata suluhisho litakalowanufaisha pande zote katika biashara ya madini hayo.
Agizo hilo limetolewa leo Mei 14, 2026 jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, wakati wa kikao kati ya wachimbaji wa madini ya jasi na wanunuzi zikiwemo kampuni za saruji na wazalishaji wa gypsum kilichofanyika katika ukumbi wa Makao Makuu ya Tume ya Madini.
Dkt. Kiruswa amesema Serikali inahitaji kila upande kuwasilisha kwa kina changamoto zinazoukabili ili kufanya uchambuzi utakaosaidia kufikia muafaka wenye manufaa kwa wachimbaji, wanunuzi na watumiaji wa mwisho.
“Tunataka kila upande uainishe vitu vinavyouumiza upande mmoja na vinavyoubeba upande mwingine ili baada ya uchambuzi huo tupate suluhisho la pamoja,” amesema Dkt. Kiruswa.
Aidha, ameahidi Serikali kuyafanyia kazi malalamiko kuhusu tozo mbalimbali zinazotozwa na baadhi ya halmashauri ambazo zimeelezwa kuwa zinaongeza gharama za uzalishaji na biashara ya madini ya jasi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wachimbaji Wadogo wa Madini ya Jasi Mkoa wa Lindi, Salum Kassim, amesema bei ya madini hayo haijawahi kuongezeka tangu mwaka 2016 licha ya kupanda kwa gharama za uzalishaji ikiwemo mafuta, vipuri vya mitambo na mishahara ya wafanyakazi.
Amesema hali hiyo imeathiri uzalishaji na kufanya wachimbaji wengi kushindwa kupata faida kutokana na biashara hiyo.
Katika mapendekezo yao, wachimbaji wamependekeza bei ya tani moja ya jasi kwa Dar es Salaam na Pwani iongezwe kutoka shilingi 110,000 hadi 150,000, Mkoa wa Mtwara kutoka shilingi 75,000 hadi 95,000, Mkuranga kutoka shilingi 95,000 hadi 130,000 huku eneo la Kiranjeranje bei ikipendekezwa kuongezeka kutoka shilingi 60,000 hadi 75,000 kwa tani.
Kwa mujibu wa Kassim, marekebisho ya bei yatasaidia kufufua uzalishaji wa madini hayo na kuboresha maisha ya wachimbaji ambao kwa sasa wanakabiliwa na changamoto kubwa za uendeshaji.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Manunuzi wa kampuni ya Dangote Cement Limited, Halima Kuchwa, ametoa tahadhari kuwa ongezeko la gharama za malighafi linaweza kuathiri bei ya saruji sokoni na hatimaye kumgusa mtumiaji wa mwisho.
Madini ya jasi ni miongoni mwa malighafi muhimu inayotumika katika uzalishaji wa saruji, gypsum na bidhaa nyingine za ujenzi nchini. Tanzania ina maeneo kadhaa yenye uzalishaji wa jasi ikiwemo Lindi, Mtwara, Pwani na Mkuranga. Kwa miaka ya hivi karibuni, wachimbaji wadogo wamekuwa wakilalamikia kupanda kwa gharama za uzalishaji huku bei ya soko ikibaki ileile kwa muda mrefu, hali inayodaiwa kupunguza tija na kuathiri uzalishaji wa madini hayo.












0 comments:
Post a Comment