Nafasi Ya Matangazo

May 07, 2026

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema Serikali itaendelea kusimamia sera, sheria na miongozo inayohusu afya na lishe ili kuhakikisha elimu inayotolewa kwa wananchi inalinda usalama wa afya za Watanzania.
 
Amesema hayo leo Alhamisi, Mei 7, 2026, wakati akijibu swali la Mbunge wa Hai, Mhe. Saashisha Mafuwe, katika kipindi cha Maswali kwa Waziri Mkuu Bungeni jijini Dodoma. Mbunge huyo alitaka kujua mpango wa Serikali wa kuweka utaratibu maalumu wa utoaji elimu ya lishe kwa watu wenye taaluma husika.
 
Akijibu swali hilo, Dkt. Mwigulu alisema Serikali itaendelea kuhakikisha elimu ya afya na lishe inayotolewa kwa wananchi inazingatia taaluma, ushahidi wa kitaalamu na usalama wa afya.
 
“Serikali itaendelea kusimamia miongozo iliyopo ili taarifa au elimu inayotolewa na wenye taaluma ya lishe iwe ya kweli na imethibitishwa kutokuwa na madhara kwa kile kinachoshauriwa,” alisema.
 
Aidha, Waziri Mkuu aliielekeza Wizara ya Afya pamoja na mabaraza yanayosimamia taaluma za afya kuendelea kufanya tathmini kuhusu uratibu wa leseni na vibali kwa watoa elimu ya afya na lishe nchini.
 
Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu alisema Serikali inaendelea kufuatilia athari za migogoro ya kimataifa katika sekta mbalimbali za uchumi, hususan upatikanaji na bei ya mafuta.
 
Amesema hayo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Janeth Mahawanga, aliyetaka kujua hatua zinazochukuliwa na Serikali kukabiliana na athari za migogoro ya kimataifa zinazoathiri upatikanaji wa mafuta nchini.
 
Waziri Mkuu alisema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha bidhaa ya mafuta haipungui nchini na kupunguza athari za kupanda kwa gharama kwa wananchi.
 
“Mheshimiwa Spika, tayari kuna taratibu za namna ya kutekeleza zoezi hilo la ruzuku, ambapo zimekuwepo njia nyingi zinazotumika kwa ajili ya kuhakikisha tunapunguza makali ya madhara yanayotokana na kile kinachoendelea kule Mashariki ya Kati,” alisema.
 
Alisema Serikali pia imeendelea kushirikiana na wadau wa usafirishaji ili kudhibiti ongezeko la gharama za usafiri na usafirishaji.
 
“Tulizungumza na wadau wa usafirishaji na tukakubaliana kupunguza baadhi ya gharama walizokuwa wanazibeba. Kwa mfano, tulisema hakuna ulazima wa kila basi kupita kila stendi kama halina abiria wa kushusha,” alisema.
 
Aidha, alisema Serikali imepunguza baadhi ya taratibu za mizani kwa mabasi na magari ya usafirishaji ili kupunguza gharama za uendeshaji.
 
“Hata yale yanayotakiwa kupima uzito, tumepunguza vituo vya kupita kupima. Watapita kwenye mizani ya kwanza na ya mwisho kabla hawajamaliza safari,” alisema.
 
Alisema hatua hizo ni sehemu ya ruzuku zisizo za moja kwa moja zinazolenga kupunguza gharama ambazo zingebebwa na wananchi.
 
“Hizi ni njia mbalimbali za utoaji wa ruzuku zisizo za moja kwa moja ili kupunguza gharama ambazo zingebebwa na mwananchi,” alisema.
 
Waziri Mkuu alisema Serikali itaendelea kufuatilia mwenendo wa uchumi wa dunia na kuchukua hatua stahiki kuhakikisha huduma muhimu zinapatikana kwa wakati na kwa gharama nafuu kwa wananchi.
Posted by MROKI On Thursday, May 07, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo