Nafasi Ya Matangazo

January 09, 2026

Afisa Muuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Flora Kasembe akimweleza mkazi wa Arusha huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo zinazotolewa na wataalamu wa taasisi hiyo katika kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya magonjwa mbalimbali yakiwemo ya moyo inayofanyika katika Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) ambayo inasimamiwa na JKCI.
Mtaalamu wa maabara wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Glory Mtui akipima sampuli za damu katika kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya magonjwa mbalimbali yakiwemo ya moyo inayofanyika katika Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) ambayo inasimamiwa na JKCI.
Mtaalamu wa  vipimo vya moyo wa Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) Antony Patrick,  akimpima kipimo cha kuangalia jinsi mfumo wa umeme wa moyo unavyofanya kazi  mkazi wa Arusha aliyefika katika kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya magonjwa mbalimbali yakiwemo ya moyo inayofanyika Hospitali ya ALMC kupata huduma za matibabu.
Daktari wa huduma za dharura wa hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) ambayo inasimamiwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Farida Abdallah akimsikiliza mwananchi aliyefika katika Hospitali hiyo kwaajili ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo zinazotolewa katika kambi maalumu ya matibabu ya magonjwa mbalimbali.
Afisa Muuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hania Bwahama akimpima kipimo cha kuangalia wingi wa sukari kwenye damu mkazi wa Arusha aliyefika katika Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) kwaajili ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali zinazotolewa katika kambi maalumu ya matibabu.
*****************
Na Mwandishi Maalum – Arusha
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) itaimarisha kwa kiasi kikubwa utalii tiba katika Kanda ya Kaskazini na mikoa jirani kufuatia kuingia mkataba wa kusimamia Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) hususan katika huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa watalii wanaotembelea ukanda huo.
Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni katika kambi ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali inayofanywa na wataalamu wa JKCI katika hospitali ya ALMC, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha Dkt. Charles Mkombachepa alisema maboresho hayo yataifanya Arusha kuwa kitovu muhimu cha utalii tiba kutokana na kuimarika kwa huduma za afya zinazokidhi mahitaji ya watalii wa ndani na nje ya nchi.
Dkt. Mkombachepa alisema kuimarishwa kwa huduma za afya ni nguzo muhimu katika kukuza utalii tiba, hasa kwa Mkoa wa Arusha ambao hupokea idadi kubwa ya watalii wanaotembelea vivutio mbalimbali vya utalii.
“Ushirikiano huu utaimarisha kwa kiwango kikubwa huduma za afya katika mkoa wetu, hususan huduma za magonjwa ya moyo ambazo zimekuwa hitaji kubwa kwa wananchi na watalii wanaotembelea Arusha,” alisema.
Alisema kuwa hapo awali, watalii waliokumbwa na changamoto za kiafya walilazimika kusafirishwa kwenda Nairobi au Dar es Salaam kwaajili ya matibabu, hali iliyoongeza gharama na usumbufu.
“Kwa kuwepo kwa huduma hizi hapa Arusha, tunapunguza gharama za matibabu na usafiri, lakini pia tunachochea utalii tiba kwa kuifanya Arusha kuwa kituo muhimu cha huduma za magonjwa ya moyo,” aliongeza Dkt. Mkombachepa.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Arusha Dkt. Maduhu Nindwa ambaye naye alifika katika kambi hiyo ya matibabu kuona huduma zinazotolewa alisema ujio wa madaktari bingwa kutoka JKCI umeongeza ufanisi wa utoaji wa huduma za afya pamoja na kujenga uwezo kwa wataalamu wa mkoa huo.
“Madaktari wetu wanaoshiriki katika kambi hii ya matibabu ya magonjwa mbalimbali yakiwemo ya moyo wanapata fursa ya kujifunza kwa vitendo kutoka kwa wataalamu wabobezi, jambo linaloboresha ubora wa huduma tunazotoa na kuongeza imani kwa wananchi na watalii,” alisema Dkt. Nindwa.
Kwa upande wa wananchi waliopata nafasi ya kupima afya zao katika kambi hiyo walieleza kuridhishwa kwao na huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali yakiwemo ya moyo waliyoipata, wakisema ujio wa JKCI umewapunguzia gharama na usumbufu wa kusafiri umbali mrefu kutafuta matibabu.
“Hii ni mara yangu ya kwanza kupima afya bila ya kuumwa, niliposikia huduma ya upimaji bila malipo inatolewa hapa nikaona nami nitumie nafasi hii kupima afya ya mwili wangu. Nimepokelewa vizuri na ninaendelea kupata huduma bila changamoto,” alisema Suzana Nkini mkazi wa Ngarenanyuki mkoani Arusha.
“Huduma nilizozipata zimenipa matumaini makubwa nimefanyiwa vipimo vya moyo na vipimo vya damu sasa hivi ninasubiri kumuona daktari. Ninawaomba wananchi wenzangu mtakaposikia mahali panatolewa huduma ya kupima afya mjitokeze kupima kwani ni muhimu kujua hali ya afya yako mapema,” alisema Elfas Zakayo mkazi wa Ngerenaro.
Posted by MROKI On Friday, January 09, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo