Nafasi Ya Matangazo

January 07, 2026

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA. Amos Makalla akipokea ua kutoka kwa mfanyakazi wa hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) Mourine Kivuyo alipotembelea hospitali hiyo leo kwaajili ya kuona  kambi maalum ya upimaji na matibabu ya magonjwa mbalimbali inayofanyika ALMC  ambayo inasimamiwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA. Amos Makalla akimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alipotembelea Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) kwaajili ya kuzindua kitengo cha wagonjwa wa dharura (EMD) ambacho kimekarabatiwa pamoja na kuona kambi maalum ya upimaji na matibabu ya magonjwa mbalimbali inayofanyika katika hospitali hiyo ambayo inasimamiwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Salehe Mwinchete akimueleza Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA. Amos Makalla jinsi wanavyopima utendaji kazi wa moyo kwa kutumia mashine ya ECHO alipofika katika Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center (ALMC) kwaajili ya kuzindua kitengo cha wagonjwa wa dharura (EMD) ambacho kimekarabatiwa pamoja na kutembelea kambi maalum ya upimaji na matibabu ya magonjwa mbalimbali inayofanyika katika hospitali hiyo ambayo inasimamiwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA. Amos Makalla akikata utepe kwaajili ya kuzindua kitengo cha wagonjwa wa dharura (EMD) ambacho kimefanyiwa ukarabati na kuwekewa mashine za kisasa kwa thamani ya shilingi milioni 200 kilichopo katika Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) ambayo inasimamiwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (ALMC).
*************
Na Mwandishi Maalumu - Arusha
Kwa mara ya kwanza kwa kiwango kikubwa  wananchi wa Mkoa wa Arusha na mikoa jirani wamenufaika  na huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo bila kulazimika kusafiri hadi Dar es Salaam, hali iliyotajwa kuwa mkombozi kwa mamia ya familia zinazokabiliwa na gharama kubwa za matibabu.

Hatua hiyo imekuja kufuatia uwezeshaji wa Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia programu maalumu ya tiba mkoba inayofanywa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center (ALMC).

Akiwa katika ziara ya kutembelea kambi hiyo ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali yakiwemo ya moyo Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA. Amos Makalla alisema uwepo wa JKCI mkoani humo ni hatua ya kimkakati itakayobadili kabisa taswira ya huduma za afya katika Kanda ya Kaskazini hasa kwa magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo.

Mhe. Makalla alisema zaidi ya wananchi 1,200 tayari wameshapata huduma za matibabu bila malipo, huku Serikali ikiendelea kujipanga kuwasaidia wananchi wasiokuwa na uwezo wanaohitaji rufaa kwenda kupata matibabu zaidi JKCI jijini Dar es Salaam.

“Huduma hizi si kwa wananchi wa Arusha pekee, bali pia zitawanufaisha watalii na wageni, hususan ikizingatiwa Arusha ni miongoni mwa miji itakayohudumia michuano ya AFCON 2027,” alisema Makalla.

Aidha, alitumia fursa hiyo kuwakumbusha wananchi umuhimu wa kujiunga na mifumo ya bima ya afya ili kupunguza mzigo wa gharama za matibabu pindi changamoto za kiafya zinapojitokeza.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Dkt. Peter Kisenge alisema taasisi hiyo imeendelea kusogeza huduma za moyo karibu na wananchi kwa kufungua vituo sita katika maeneo mbalimbali nchini, huku kituo cha Arusha kikiwa na jukumu la kuhudumia mikoa yote ya Kanda ya Kaskazini.

Dkt. Kisenge alisema kambi ya uchunguzi wa magonjwa mbalimbali yakiwemo ya moyo ilianza Desemba 29, 2025 na inatarajiwa kuhitimishwa Januari 9, 2026, ambapo hadi sasa idadi kubwa ya wananchi wamejitokeza, jambo linaloashiria ukubwa wa tatizo la magonjwa ya moyo katika jamii.

“Mwitikio huu unaonyesha wazi kuwa magonjwa ya moyo yamekuwa tatizo kubwa lakini lisilopewa uzito unaostahili. Tunawasihi wananchi wasisubiri dalili bali wajenge utamaduni wa kupima afya mapema,” alisema.

Aliongeza kuwa wagonjwa waliobainika kuwa na matatizo makubwa walipewa rufaa kwenda Dar es Salaam kwa matibabu ya kibingwa zaidi, huku gharama za awali zikiendelea kugharamiwa na Serikali.

Katika hatua nyingine Dkt. Kisenge aliishukuru Hospitali ya ALMC pamoja na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kwa kushirikiana na JKCI kuanzisha kituo cha huduma za moyo, akisema ushirikiano huo ni mfano wa kuigwa katika kuimarisha huduma za afya nchini.

“Lengo letu ni moja kuhakikisha Watanzania hawapotezi maisha kwa sababu ya magonjwa ya moyo yanayoweza kugunduliwa na kudhibitiwa mapema,” alisema Dkt.Kisenge.

Naye Diwani wa Kata ya Ngarenaro, Abdulaziz Chande maarufu kama Dogo Janja, alisema kufunguliwa kwa kituo hicho kutapunguza kwa kiasi kikubwa mzigo wa gharama na usumbufu kwa familia nyingi zilizokuwa zikilazimika kusafiri mara kwa mara kwenda Dar es Salaam kufuata huduma za matibabu.

“Kwa uzoefu wangu binafsi, familia yangu imekuwa ikipitia changamoto kubwa za kusafirisha mgonjwa wa moyo Dar es Salaam. Kituo hiki Arusha ni faraja si kwangu tu, bali kwa wananchi wengi,” alisema.

Programu hiyo ya uchunguzi na matibabu bila malipo inaendelea katika Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center (ALMC) huku wananchi wakihimizwa kujitokeza kwa siku chache zilizosalia ili kunufaika na huduma hizo muhimu.
Posted by MROKI On Wednesday, January 07, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo