Nafasi Ya Matangazo

December 23, 2025

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, akizungumza na watumishi wa OSHA kwenye ziara ya kikazi katika Ofisi za OSHA Dar es Salaam.
Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, akimkabidhi Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Rahma Kisuo, vifaa kinga (Personal Protective Equipment-PPEs) ambavyo atakuwa anavitumia anapotembelea maeneo yakazi kwa ajili ya ukaguzi wa mifumo ya usalama na afya
Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, akimkabidhi Waziri wa Nchi, Ofisi yaWaziri Mkuu-Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, vifaa kinga (Personal Protective Equipment-PPEs) ambavyo atakuwa anavitumia anapotembelea maeneo yakazi kwa ajili ya ukaguzi wa mifumo ya usalama na afya
Watumishi wa OSHA wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, wakati wa ziara ya kikazi katika Ofisi za OSHA Dar es Salaam.

Na Fredy Mgunda 
Serikali imewataka wamiliki wote wa maeneo ya kazi nchini ambao bado hawajayasajili maeneo yao na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kuhakikisha wanasajili maeneo hayo ndani ya siku 90 kuanzia Januari 2026, hatua inayolenga kuimarisha usalama na afya kwa wafanyakazi nchini.

Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, alipofanya ziara ya kikazi katika Ofisi za OSHA zilizopo Kinondoni, Jijini Dar es Salaam.

Ziara hiyo ni ya kwanza kwa Waziri Sangu tangu alipoteuliwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kushika wadhifa huo, ikiwa na lengo la kujifunza kwa kina namna OSHA pamoja na taasisi nyingine zilizo chini ya wizara hiyo zinavyotekeleza majukumu yao ya kisheria.

Akizungumza na menejimenti na watumishi wa OSHA leo (Desemba 22, 2025), Waziri Sangu amesema taasisi hiyo ina jukumu kubwa la kulinda nguvu kazi ya Taifa dhidi ya ajali, magonjwa ya kazini pamoja na vifo vinavyosababishwa na mazingira hatarishi ya kazi.

Amesema ili OSHA iweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo, ni lazima maeneo yote ya kazi yatambulike rasmi kupitia usajili, jambo litakaloiwezesha taasisi hiyo kufanya ukaguzi wa mara kwa mara na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa waajiri.

“Uzingatiaji wa kanuni bora za usalama na afya mahali pa kazi hauwezekani iwapo maeneo ya kazi hayajasajiliwa. Serikali imeamua kutoa siku 90 kuanzia Januari 2026 ili wamiliki wote wa maeneo ya kazi wahakikishe wanakamilisha zoezi hili,” amesema Waziri Sangu.

Aidha, amewataka watumishi wa OSHA kufanya kazi kwa bidii, kujituma na kuzingatia weledi ili kuwawezesha waajiri kusimika mifumo madhubuti ya usalama na afya mahali pa kazi. Vilevile, amewahimiza waajiri kuzingatia ushauri unaotolewa na wataalamu wa OSHA kwa lengo la kuzuia ajali na magonjwa ya kazini.

Waziri Sangu ameeleza kuwa usajili wa maeneo ya kazi unatekelezwa kwa mujibu wa kifungu cha 16 na 17 cha Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003, inayoiwezesha OSHA kusajili maeneo ya kazi, kuyakagua na kutoa mapendekezo ya kitaalamu juu ya uboreshaji wa mazingira ya kazi.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, amesema taasisi hiyo imefarijika kumpokea Waziri na kupata maelekezo yake, huku akiahidi kuwa watumishi wa OSHA wataendelea kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kwa kuzingatia miongozo ya serikali.

“Kwa niaba ya watumishi wenzangu, nakuhakikishia kuwa tutatekeleza maelekezo yote ya serikali kwa weledi na uadilifu mkubwa, ili kuhakikisha usalama na afya za wafanyakazi zinalindwa na taasisi yetu inaendelea kutimiza wajibu wake,” amesema Bi. Mwenda.

Katika ziara hiyo, Waziri Sangu aliambatana na Naibu Waziri, Rahma Kisuo, pamoja na Kamishna wa Kazi, Bi. Suzan Mkangwa, aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo.

OSHA ni taasisi iliyo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), yenye jukumu la kutoa na kusimamia miongozo ya usalama na afya mahali pa kazi. Kupitia usajili, ukaguzi na ushauri wa kitaalamu, taasisi hiyo inalenga kuboresha mazingira ya kazi na kulinda maisha ya wafanyakazi nchini.
Posted by MROKI On Tuesday, December 23, 2025 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo