Na OWM–KVAU
Wakulima na wasindikaji wadogo
wa zao la zabibu mkoani Dodoma wamepatiwa mafunzo maalum ya kukuza ujuzi katika
mlolongo wa thamani wa zao hilo, yakiwemo masuala ya uvunaji, uhifadhi,
uongezaji thamani na mbinu za kutafuta masoko ya zabibu na bidhaa zake.
Akizungumza wakati wa ufunguzi
wa mafunzo hayo Oktoba 20, 2025 Hombolo, jijini Dodoma, Afisa Kazi Mkuu Idara
ya Ajira na Ukuzaji Ujuzi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Bi.
Neema Moshi, amesema lengo la mafunzo hayo ni kuongeza ujuzi na maarifa kwa
wakulima na wafanyakazi ili kuendana na mabadiliko ya kisayansi, kiteknolojia
na kiuzalishaji.
“Mafunzo haya yanawezesha
nguvu kazi ya taifa kupata ujuzi na maarifa yanayokidhi mahitaji ya soko la
Ajira, kuboresha tija na kuongeza ubora wa bidhaa pamoja na huduma
wanazozalisha,” amesema.
Awali, akizungumza Mkulima wa
Zabibu kutoka Hombolo, Bi. Rachel Mushi, amesema mafunzo hayo yamemsaidia
kujifunza mbinu bora za uhifadhi na usindikaji wa zabibu jambo litakalomwezesha
kuongeza kipato kupitia uzalishaji wa bidhaa zenye ubora wa juu.
“Awali tulikuwa tunauza zabibu
ghafi pekee, lakini sasa tumejifunza kuzalisha juisi, jamu na mvinyo wa
kienyeji. Hii itatufungulia fursa nyingi zaidi za kipato. Tunashukuru sana
Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kutuletea mafunzo haya muhimu,” amesema Bi. Mushi.
Naye Bw. Daniel Mgonja,
msindikaji mdogo wa zabibu kutoka kijiji cha Nzuguni, amesema kupitia mafunzo
hayo amepata uelewa kuhusu ubora wa vifungashio na namna ya kufikia masoko ya
ndani na nje ya nchi.
Mafunzo hayo ni sehemu ya
utekelezaji wa Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi, inayolenga kuwajengea uwezo
wafanyakazi kutoka sekta mbalimbali, ikianzia na wakulima na wasindikaji wadogo
wa zao la Zabibu. Aidha, yanatolewa kwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Waziri
Mkuu na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), ambapo jumla ya Wakulima
70 wamepatiwa ujuzi.
Posted by MROKI
On Wednesday, October 22, 2025
No comments
0 comments:
Post a Comment