Katika fainali ya Polisi Jamii Cup iliyofanyika katika viwanja vya shule ya Itete, kata ya Mlowo wilayani Mbozi, timu ya Mlowo United iliibuka kidedea baada ya kuichapa Wandewa FC kwa mikwaju ya penati 7-6 na kutwaa kombe la Polisi Jamii Cup, mechi hiyo iliyokuwa ya kusisimua ilimalizika kwa sare ndani ya dakika 90, na kulazimika kwenda hatua ya matuta ambapo Mlowo United walionesha umahiri mkubwa, mbali na kombe walilolinyakuwa la Polisi Jamii Cup, Mlowo United walijinyakulia kitita cha pesa taslimu shilingi milioni moja, 1,000,000/=, huku Wandewa FC wakiondoka na shilingi laki nne na elfu hamsini (450,000/=) kwa nafasi ya pili, huku mshindi wa tatu naye alipata zawadi ya fedha taslimu shilingi laki tatu (300,000/=).
Fainali hizo, zilipambwa na utoaji wa zawadi mbalimbali kwa washindi wa waliofanya vizuri zaidi ikiwemo mchezaji bora, kipa bora, timu bora, pamoja na mashabiki bora wa kiume na wakike, huku mashindano hayo yaliyoandaliwa kwa mafanikio makubwa chini ya uongozi wa Mkuu wa Kituo cha Polisi Mlowo, Mrakibu wa Polisi John Maro, aliyeshukuru ushiriki wa wananchi na kusisitiza umuhimu wa mshikamano kati ya Polisi na jamii katika kulinda amani na usalama wa eneo hilo.
Akizungumza Septemba 07, 2025 na washiriki wa fainali hiyo, Afisa Mnadhimu wa Polisi Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Akama Shabaan, alitumia fursa hiyo kutoa elimu juu ya umuhimu wa michezo kwa vijana, huku akibainisha kuwa michezo sio tu hujenga afya ya mwili na akili, bali pia ni chachu ya kujiepusha na uhalifu, dawa za kulevya, mimba za utotoni, na hutoa fursa za ajira na biashara, pia aliwasihi wananchi hao kudumisha amani na utulivu katika kipindi cha kampeni kuelekea uchaguzi mkuu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Maria Kway, aliwaelimisha wananchi hao kuhusu athari za ukatili wa kijinsia majumbani, huku akisisitiza kuwa ukatili huo husababisha ongezeko la watoto wa mitaani, migogoro ya kifamilia na hata vifo, pia aliwahimiza wazazi kuwapa watoto malezi bora na kukumbusha juu ya zoezi la kulasimisha silaha ambalo linaendelea kwa kipindi cha msamaha lililoanza Septemba 1 hadi Oktoba 30 ili kulinda usalama wa jamii.
Nae, Mkuu wa Polisi Jamii Wilaya ya Mbozi, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Debora Muhekwa, alihamasisha wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe katika masuala ya ulinzi na usalama, akisisitiza kuwa jukumu hilo ni la kila mwananchi, si la Jeshi la Polisi pekee, pia alitoa rai kwa jamii kutoa taarifa za uhalifu mapema kabla ya madhara kutokea.
Nae, Mratibu Msaidizi wa mashindano hayo ambaye pia ni Polisi Kata wa Igamba, Mkaguzi wa Polisi Lusajo Mwaipopo, alitoa wito kwa wananchi kujiepusha na kujichukulia sheria mkononi pindi wanapokumbana na matatizo au uhalifu, alisisitiza kuwa ni kosa la jinai kuadhibu au kuua bila kufuata utaratibu wa kisheria na badala yake wahalifu wafikishwe kituo cha polisi kwa hatua stahiki za kisheria.
Kwa upande wao mashabiki waliokuwepo walionesha furaha na shukrani kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe, huku mmoja wa mashabiki hao waliohudhulia fainali hiyo Emmanuel Mwashitindi, alisema kuwa kupitia mashindano hayo, vijana wengi wamejikita kwenye michezo badala ya uhalifu, na alilishukuru Jeshi la Polisi kwa kuandaa mashindano hayo ambayo yameleta mshikamano, burudani na elimu kwa jamii ya Mlowo.

















0 comments:
Post a Comment