Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia Kikao cha 80 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
kinachofanyika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa Jijini New York nchini Marekani.
*************
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema Tanzania inalaani
kuibuka upya kwa ukiukwaji wa sheria za kimataifa na kupelekea matumizi ya
nguvu kama njia ya kutatua migogoro hali inayopelekea ukatili uliokithiri kwa binadamu
hususani watoto, wanawake, wazee pamoja na wagonjwa katika maeneo ya migogoro.
Makamu wa Rais amesema hayo
wakati akihutubia Kikao cha 80 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
kinachofanyika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa Jijini New York nchini Marekani.
Amesema uwepo wa mitazamo ya kibeberu, ikiwa ni pamoja na ile ya
kuichukulia Afrika kuwa sehemu ya uchukuaji rasilimali na uporaji wa ardhi,
pamoja na uwepo wa makampuni ya kimataifa kuendelea kufanikiwa kutokana na
unyonyaji wa mali asili za Afrika, huku wakisababisha au kuunga mkono migogoro
inapaswa kumalizika sasa.
Makamu wa Rais amesema Tanzania inauchukulia msimamo
wa upande mmoja na matumizi mabaya ya nguvu za kijeshi, pamoja na kushindwa kwa
jumuiya ya kimataifa na mataifa yenye nguvu duniani katika kukomesha umwagaji
damu na vita vya hatari vinavyoendelea katika maeneo mengi duniani, kuwa ni
jambo lisilokubalika.
Pia ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kutambua kuwa
ongezeko la matumizi ya fedha katika masuala ya kijeshi ikiwemo utafiti na
utengenezaji wa silaha ni jambo la kusikitisha na ni kinyume cha maadili.
Amesema hali hiyo inazuia jitihada za kutafuta amani duniani, na inachukua
kiasi kikubwa cha rasilimali ambazo zingeweza kutumika kuendeleza maendeleo
endelevu na ustawi kwa wanadamu wote.
Makamu wa Rais amesema dunia inapaswa kuendelea
kutafuta amani bila kuchoka kwani ndio sharti la maendeleo ya kijamii na
kiuchumi. Amepongeza juhudi za Katibu
Mkuu wa Umoja wa Mataifa, viongozi wa dunia, na mashirika ambayo yanashiriki
kikamilifu katika upatanishi na utatuzi wa migogoro katika nchi na maeneo kama
vile Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Sudan, Urusi, Ukraine, na
Mashariki ya Kati.
Ametoa wito wa
ushirikishwaji kamili wa wanawake katika kutafuta amani hususani katika kipindi hiki inaposherehekewa miaka 30 tangu
azimio la Beijing na maendeleo
yaliyopatikana katika kukuza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake.
Amesema Rais wa kwanza mwanamke wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan ameonyesha njia katika kueleza sera na
vitendo vinavyoimarisha nafasi ya mwanamke katika sekta zote za jamii. Amesema
kikanda na kimataifa, amekuwa mtetezi wa amani, haki, usalama na matumizi ya
nishati safi.
Amesema Tanzania kama mwanachama wa Baraza la Amani na
Usalama la Umoja wa Afrika, pia nafasi iliyotumikia kama Mwenyekiti wa Asasi ya
Siasa Ulinzi na Usalama Jumuiya ya SADC ilichangia kikamilifu katika mipango ya
amani na kuunga mkono hatua za kuzuia na kutatua migogoro.
Tanzania imetangaza kugombea kiti kisicho cha kudumu
katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa muhula wa 2029-2030, ili
kuthibitisha dhamira iliyonayo ya amani na usalama duniani.
Halikadhalika, Makamu wa Rais amesema, Tanzania inasisitiza msimamo wa Afrika wa kurekebisha uwakilishi mdogo wa bara hilo katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na kutoa wito wa kupitishwa kwa angalau viti viwili vya kudumu vya Afrika vyenye nguvu ya kura ya turufu.
Kwa lengo namba 6, upatikanaji wa maji safi na
salama uliongezeka katika maeneo ya vijijini na mijini kutoka asilimia 32 na 55
mwaka 2000 hadi asilimia 79.9 na 94 mwaka 2024. Kwa nishati safi ya bei nafuu
ambayo ni lengo namba 7, Tanzania imefanikiwa kuunganisha nishati ya umeme kwa
vijiji 8,587 mwaka (2000) hadi 12,318 mwaka 2024 ambapo ni vijiji 15 pekee
vilivyobaki bila umeme.
Makamu wa Rais amehimiza jumuiya ya kimataifa
kuimarisha mwitikio wa pamoja wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Ametoa
wito wa kutumia vyema fursa ya Mkutano wa wa COP30 nchini Brazil kuhakikisha
ahadi zinatekelezwa ikiwemo uchangiaji wa Mfuko wa Hasara na Maafa kutokana na
athari za mabadiliko ya tabianchi (Loss and Demage Fund) pamoja na kuongezwa
kwa ufadhili wa masharti nafuu wa muda mrefu, uhamishaji wa teknolojia, na
masharti ya kibiashara yanayozingatia haki ili kufanikisha ukusanyaji wa mapato
ya ndani kwa mataifa na kutafuta ushirikiano wa manufaa kwa pande zote katika
matumizi ya rasilimali.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwasili
ndani ya Jengo la Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa Jijini New York nchini
Marekani kwaajili ya kuhutubia Kikao cha 80 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Tarehe 25 Septemba 2025.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwasili
ndani ya Jengo la Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa Jijini New York nchini
Marekani kwaajili ya kuhutubia Kikao cha 80 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Tarehe 25 Septemba 2025.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa na
Mwenza wake Mama Mbonimpaye Mpango, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki Balozi Thabit Kombo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Zanzibar
Kazi na Uwekezaji Mhe. Shariff Ali Shariff katika picha ya pamoja na Ujumbe wa
Mabalozi wa Tanzania mara baada ya kuhutubia Kikao cha 80 cha Baraza Kuu la
Umoja wa Mataifa kinachofanyika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa Jijini New York
nchini Marekani.












0 comments:
Post a Comment