Nafasi Ya Matangazo

September 05, 2025

Na Mwandishi Wetu, Mwanza
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe Doto Biteko anatarajiwa kufungua rasmi michezo ya 39 ya Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara, Wakala za serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (SHIMIWI) inayofanyika kwenye viwanja mbalimbali jijini Mwanza.

Mwenyekiti wa SHIMIWI, Bw. Daniel Mwalusamba amesema michezo itafunguliwa rasmi tarehe 07 Septemba, kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Michezo hiyo ilianza tarehe 01 Septemba, 2025 kwa hatua ya makundi ya mpira wa netiboli, mpira wa



miguu, kuvuta kamba wanawake na wanaume, na hatua hiyo itamalizika Septemba 5.

Bw. Mwalusamba amesema mwamko ni mkubwa kwa michezo ya mwaka huu ambapo hadi sasa takribani klabu wanachama 65 zinashiriki katika michezo mbalimbali.

Hatahivyo, amesema bado shirikisho linasisitiza kwa klabu ambazo zimesshindwa kushiriki michezo kwa mwaka huu zianze maandalizi kwa ajili ya michezo ya mwakani.

“Kama mnakumbuka mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo watumishi wa umma washiriki mazoezi na michezo ili kuimarisha afya zao, na bado tunaendelea kusisitiza kama kamati ya utendaji kuwa watumishi wa umma wanatakiwa kufanya mazoezi, basi kuangalia wakati wa bajeti kuweka mazingira mazuri ya kuwawezesha kushiriki,” amesema Bw. Mwalusamba.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya michezo hiyo, Bw. Appolo Kayungi amesema michezo ya mwaka huu imekuwa na hamasa kubwa, ambapo timu zinaelewa kanuni.

“Malalamiko ni machache katika usajili, lakini wanaokata rufaa kulalamikia wachezaji wa taasisi fulani, wakieleweshwa basi ile rufaa inakuwa haina maana, maana kanuni zinaruhusu wachezaji watano wataasisi fulani kuchezea taasisi nyingine,” amesema Bw. Kayungi.
Posted by MROKI On Friday, September 05, 2025 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo