Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akisaini Tamko
la kuzindua Toleo la Sheria za Tanzania zilizofanyiwa urekebu la mwaka 2023 kwa
mujibu wa kifungu cha 12 cha Sheria ya urekebu wa sheria, Ikulu Chamwino Mkoani
Dodoma tarehe 23 Aprili, 2025.
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akisaini nakala
3 za Sheria za Tanzania zilizofanyiwa urekebu kwa mujibu wa kifungu cha 17 cha
Sheria ya urekebu wa sheria, Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 23 Aprili,
2025.
***************
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan
ameiagiza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kukamilisha zoezi la kutafsiri Sheria
za Tanzania kwa lugha ya Kiswahili, ikiwemo Toleo la Sheria za Tanzania la Mwaka
2023.
Rais Dkt. Samia ametoa agizo hilo leo wakati wa uzinduzi wa Toleo la
Sheria za Tanzania zilizofanyiwa Urekebu la Mwaka 2023 katika hafla
iliyofanyika Ikulu ya Chamwino.
Aidha, Rais Dkt. Samia ameelekeza uwekwe utaratibu utakaowezesha kupatikana
kwa nakala za Toleo la Sheria zilizofanyiwa Urekebu la Mwaka 2023 ikiwemo
kutumia TEHAMA ili wananchi wazipate kwa urahisi kwenye mitandao kwa minajili
ya kujifunza na kuzijua haki zao.
“Sheria ni kioo
cha ustaarabu wa Taifa, bila sheria zilizowekwa wazi haki haiwezi kupatikana,
bila sheria kuwa wazi uhakika wa ulinzi wa haki ya raia unatoweka na
kusababisha uvunjifu wa amani na shughuli za kiuchumi zinafanyika kwa mashaka,” amesema Rais Dkt. Samia.
Rais Dkt. Samia amebainisha kuwa kutokuwepo kwa Juzuu za Sheria
zilizorekebishwa kwa wakati huchangia kunyima haki za raia, kwa sababu
wanaotumia kutolea maamuzi hawana uelewa wa uwepo wa sheria mpya. Hivyo, kukamilika
kwa Toleo la Sheria zilizofanyiwa Urekebu litarahisisha upatikanaji wa haki kwa
wananchi kwa kuwa Sheria zote kuu 446 zimehuishwa, zinapatikana kwa pamoja na
kwa urahisi na zimepangwa vizuri.
Vilevile,
Rais Dkt. Samia ameeleza kuwa upatikanaji wa Toleo lililozinduliwa utasaidia
kupunguza muda wa Mahakama kufanya utafiti kabla ya kufanya maamuzi, kuongeza uwazi
na kuwajengea wananchi imani kwa Serikali, kupunguza matumizi mabaya ya madaraka
kwa kuziba ombwe la kisheria linalochochea mianya ya rushwa, kuimarisha utawala
wa sheria na kuongeza hadhi ya nchi kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia ameagiza zoezi la Urekebu wa
Sheria lifanyike kila baada ya miaka 10 badala ya sasa ambapo limefanyika baada
ya miaka 20 tangu zoezi kama hilo kufanyika miaka 23 iliyopita mnamo mwaka
2002.
Pamoja na hayo, Rais Dkt. Samia amebainisha kuwa mbali ya kusubiri zoezi
hilo la miaka 10, kila mara Sheria zinaporekebishwa, marekebisho hayo
yajumuishwe kila mwaka na yapatikane kwa urahisi kwa kutumia TEHAMA.
Uzinduzi wa Toleo la Sheria
za Tanzania zilizofanyiwa Urekebu la Mwaka 2023 unadhihirisha dhamira ya dhati ya Serikali kujenga Taifa linalosimamia
utawala wa sheria kwa kuwa na sheria zilizowekwa wazi, zilizo sahihi na
zinazoeleweka.

Matukio
mbalimbali wakati wa uzinduzi wa toleo la Sheria za Tanzania zilizofanyiwa
urekebu la mwaka 2023, Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 23 Aprili, 2025.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akihutubia viongozi pamoja na wageni mbalimbali mara baada ya toleo la Sheria za Tanzania zilizofanyiwa urekebu la mwaka 2023, Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 23 Aprili, 2025.
Matukio mbalimbali wakati wa uzinduzi wa toleo la Sheria za Tanzania zilizofanyiwa urekebu la mwaka 2023, Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 23 Aprili, 2025.
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye
picha ya pamoja na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe.
Profesa Ibrahim Hamis Juma pamoja na Mwakilishi wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba
na Sheria Mhe. Dkt. Joseph Kizito Mhagama mara baada ya kuwakabidhi nakala 3 za
Sheria za Tanzania zilizofanyiwa urekebu kwa mujibu wa kifungu cha 17 cha
Sheria ya urekebu wa sheria kwa ajili ya kumbukumbu, Ikulu Chamwino Mkoani
Dodoma tarehe 23 Aprili, 2025.
0 comments:
Post a Comment