Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson, leo tarehe 6 Aprili, 2025 amefungua rasmi Mkutano Mkuu wa 150 wa IPU na kuendesha Vikao vya Baraza la Uongozi unaofanyika Jijini Tashkent, Uzbekistan.
Katika vikao hivyo, Dkt. Tulia ameendesha ajenda zilizojadiliwa na Kamati ya Uongozi, Maazimio na maamuzi mbalimbali ambayo yamewasilishwa rasmi kwenye Baraza la Uongozi na kisha kutolewa taarifa kwenye kikao cha kwanza cha Mkutano wa 150 kati ya vikao vinne vitakavyokamilisha Mkutano huo.
Mkutano huo umeyaleta pamoja Mabunge wanachama 181, Mabunge ya Kikanda na Kijumuiya yenye hati ya Uangalizi pamoja na taasisi na mashirika ya kimataifa ya Umoja wa Mataifa kuona namna yatakavyoshiriki kufikisha ajenda kuu ya Mkutano huo ya “Kutekeleza Shughuli za Kibunge kwa Maendeleo ya Jamii na Haki kwa wote."
Aidha, Maazimio mawili yanatarajiwa kupitishwa ambayo (i)Jukumu la Mabunge katika kuhakikisha Suluhu ya Serikali mbili kwa Palestina inatekelezwa na (ii)Mikakati ya Kibunge ya kupunguza athari za kudumu za migogoro ikiwa ni pamoja na migogoro ya kivita katika kufikia malengo ya maendeleo endelevu.
Sambamba na hayo, Wajumbe wa Mkutano huo walipata nafasi ya kumchagua Rais wa Mkutano wa 150 ambaye ni Mhe. Tanzila Narbaeva, Spika wa Bunge la Uzbekistan na mwenyeji wa Mkutano wa 150 wa IPU.
0 comments:
Post a Comment