WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewasihi viongozi wa dini nchini waendelee kukemea vikali vitendo vyote ambavyo ni kinyume na maadili ya dini na utamaduni wa Mtanzania.
"Ninawaomba viongozi wetu wa dini tuendelee kuliweka suala la kuimarisha malezi na kidhibiti mmomonyoko wa maadili kuwa ajenda ya kudumu. Lazima tuwe na maadili mema ili Taifa liwe endelevu".
Ametoa rai hiyo leo (Jumapili Machi 9, 2025) alipomwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ibada ya kuwekwa wakfu na kutawazwa kwa Askofu wa Pili wa kanisa la Anglikana Dayosisi ya Kiteto, Askofu Bethuel Mlula iliyofanyika anisa Kuu la Anglikana la Mtakatifu Mikaeli, Kiteto Mkoani Manyara.
Aidha, Waziri Mkuu amesema pamoja na masuala ya kiroho amewaomba viongozi wa dini waendelee kuwahamasisha waumini kuunga mkono ajenda mbalimbali za kitaifa, ikiwemo ya uhifadhi wa mazingira, kampeni ya nishati safi na upandaji miti pamoja na kushiriki katika hatua zote za uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amempongeza Askofu wa kwanza mstaafu wa Kanisa hilo Askofu Isaiah Chambala kwa kazi kubwa aliyoifanya katika kipindi cha uongozi wake, pia ametumia fursa hiyo kumhakikishai ushirikiano wa kutosha kwa mslahi mapana ya Wana-Kiteto na Watanzania kwa ujumla.
“Nitumie nafasi hii kuwahakikishia viongozi wetu wa dini kwamba Serikali ipo pamoja nanyi, tutaendelea kuwa na vikao vya pamoja na sisi tunathamini sana namna ambavyo mmejitoa kuiunga mkono Serikali hii”
Kwa upande wake, Askofu Mlula ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia kwa jitihada kubwa zinazofanyika ili kuwaletea Watanzania maendeleo katika sekta mbalimbali nchini ikiwemo afya na elimu.
Aidha, Askofu Mlula ameipongeza Serikali kwa kusimamia amani umoja na utulivu ambayo iliasisiwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume. “Amani ni tunu ambayo Mwenyezi Mungu ametupatia, tuitumie amani hii kujiletea maendeleo”.
Naye, Askofu wa Tanga na Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania Mhashamu Maimbo Mndolwa ametoa wito kwa wakazi wa Kiteto kwenda kuhakiki majina yao katika daftari la kudumu la wapiga kura ili waweze kushiriki uchaguzi mkuu wa wabunge na madiwani.
0 comments:
Post a Comment