Nafasi Ya Matangazo

February 13, 2025



Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesisitiza dhamira yake ya kuendeleza na kuimarisha ushirikiano wa ndani na kimataifa chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. 

CCM ambacho ni chama tawala nchini kimeeleza kuwa kitasimamia Serikali ili kuendeleza uhusiano mzuri na mataifa na taasisi mbalimbali, ndani na nje ya nchi, kwa lengo la kuleta maendeleo kwa wananchi.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, alipokutana kwa nyakati tofauti na mabalozi wa Korea Kusini, Norway na Uingereza katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba, jijini Dar es Salaam, leo Alhamisi, tarehe 13 Februari 2025.

Katika mazungumzo yake na Balozi wa Korea Kusini nchini Tanzania, Mhe. Ahn Eunju, Balozi Nchimbi alisisitiza umuhimu wa kuimarisha uhusiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Korea Kusini, hasa katika nyanja za maendeleo ya kiuchumi na teknolojia. 

Kwa sasa, Tanzania inanufaika na mkopo nafuu wa Dola bilioni 2.5 kutoka Korea Kusini kwa ajili ya sekta za elimu, afya na miundombinu, huku mojawapo ya miradi mikubwa ikiwa ni ujenzi wa Bandari ya Uvuvi Bagamoyo yenye thamani ya Dola milioni 156.5. Pia, nchi hizo mbili zinaimarisha ushirikiano katika sekta ya madini, hususan utafiti na uchimbaji wa madini mkakati kama nikeli na lithiamu.

Katika mazungumzo yake na Balozi wa Norway nchini Tanzania, Mhe. Tones Tinnes, Balozi Nchimbi alibainisha kuwa Norway ni mshirika mkubwa wa maendeleo wa Tanzania, huku uhusiano wao ukiwa umejengwa katika misingi imara kwa miongo mingi. 

Katika uendelezaji wa ushirikiano huo, Norway inashirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa miradi ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, ikihusisha sekta za kilimo, nishati, maji na afya.

Vilevile, katika mazungumzo yake na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Mhe. Marianne Louise Young, Balozi Nchimbi alisema kuwa uhusiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Uingereza, pamoja na ushirikiano wa karibu na Serikali ya Chama cha Labour, unalenga kuhakikisha wananchi wa pande zote mbili wananufaika na maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Kwa nyakati tofauti, katika mazungumzo yao na Katibu Mkuu wa CCM, mabalozi hao walipongeza maamuzi ya Mkutano Mkuu Maalum wa CCM uliomchagua Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Nchimbi kuwa mgombea mwenza, na Dkt. Hussein Ali Mwinyi kuwa mgombea wa Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM.

Katika kuhitimisha, Balozi Nchimbi imesisitiza kuwa CCM itaendelea kusimamia ushirikiano wa kimataifa kwa kuzingatia misingi ya amani, utulivu na uongozi bora, ili kuhakikisha Tanzania inaendelea kunufaika na ushirikiano wake na mataifa mbalimbali duniani. 
Posted by MROKI On Thursday, February 13, 2025 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo