Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka wananchi kuchagua wagombea wa CCM kwa kuwa wanaeleza hoja zake za kuondoa umasikini kwa wananchi huku vyama vingine vikitaja majina ya watu katika kampeni zake.
Dkt. Biteko amesema hayo leo Novemba 22,2024 wakati akifungua Kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Wilaya ya Mbogwe zilizofanyika katika Uwanja wa Lulembela mkoani Geita.
“Nataka niwaombe wananchi wote twende tukachague viongozi wa CCM watakaoshughulika na shida zetu, CCM haitaki ushindi wa kubebwa tunataka ushindi halali na sababu ya ushindi halali tunayo kwa kuwa tumetekeleza miradi mingi ya maendeleo kwa wananchi, tulihamasisha kwa wingi watu wetu kujiandikisha na tunaamini mtajitokeza kupiga kura Novemba 27, 2024,” amesema Dkt. Biteko.
Amesema awali katika wilaya hiyo hakukuwa na shule ya sekondari, watoto walikuwa wakifaulu na hakukuwa na shule ya kuwapeleka, aidha kulikuwa na hospitali moja pekee. Kwa jitihada zilizofanywa na CCM sasa wilaya hiyo imekuwa na maendeleo kwa kupata miradi mbalimbali ikiwemo maji, barabara na umeme.
Amewahimiza wananchi kuchagua wagombea wa CCM, ili kuwa na mnyororo wa uongozi kutoka chini hadi juu ili kurahisisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“ Ushindi ni mipango na CCM imejipanga na kuhamasisha wananchi kujiandikisha na kushiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, hivyo wanaCCM tembeeni vifua mbele kwa kuwa Chama chenu kinatambua mahitaji yenu na kiko tayari kuyatekeleza,” amesisitiza Dkt. Biteko.
Mbunge wa Jimbo la Mbogwe, Mhe. Nicodemas Maganga amesema kuwa CCM wataomba kura kistaarabu huku akiwahimiza wananchi kuchagua wagombea wa CCM ifikapo Novemba 27, 2024.
Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Geita, Mhe. Rose Busiga amemshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa miradi mbalimbali katika Mkoa wa Geita.
Ametaja baadhi ya miradi kuwa asilimia 100 ya vijiji vyote mkoani humo vina umeme na tayari Serikali imeendelea kutekeleza miradi ya barabara, hospitali na shule.
Pia, amewahamasisha wananchi wa Bukombe kuchagua wagombea wa CCM katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kumchagua Rais Samia katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2025.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Mbogwe, Mathias Nyororo amesema kuwa katika vitongoji 335 vilivyopo katika wilaya yake vyama vingine vimeweka wagombea katika vitongoji 14 pekee, huku katika vijiji 87 wameweka wagombea 17 pekee.
0 comments:
Post a Comment