Nafasi Ya Matangazo

October 02, 2024

Klabu ya mpira ya Yanga  imeahidi kushirikiana  na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kuchangia matibabu ya moyo kwa watoto wasio na uwezo, kutoa uelewa kwa jamii kuhusu magonjwa ya moyo na kutangaza huduma zinazotolewa na Taasisi hiyo.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Rais wa klabu ya Yanga Eng. Hersi Said wakati akizungumza na viongozi wa JKCI walipomtembelea ofisini kwake kwaajili ya kuona ni namna gani  klabu hiyo itashirikiana na JKCI.

Eng. Hersi alisema katika ushirikiano huo wataanza kwa  kuchangia matibabu ya moyo kwa watoto kwa kushiriki  chakula cha jioni chenye lengo la kuchangisha fedha hizo za matibabu kilichoandaliwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete tarehe 2 Novemba  mwaka huu katika Hoteli ya Johari Rotana iliyopo jijini Dar es Salaam.

“Taasisi hii imekuwa ikitoa huduma kwa jamii tunahitaji kuwa na ushirikiano  nayo kwa muda mrefu kwa asilimia 100,  sisi tutaanza kwa kuchangia matibabu ya moyo kwa watoto wasiokuwa na uwezo kwani tuna ndugu zetu ambao ni wagonjwa wa moyo na sisi pia tunaweza kuumwa hivyo basi ni muhimu kuisaidia jamii yenye uhitaji”.

“Pia tutatangaza huduma za matibabu ya moyo wanazozitoa, tutawapeka wachezaji wetu kupima afya za mioyo yao kwani wanawataalamu waliobobea katika matibabu ya moyo pia wanavifaa vya kisasa vya kupima na kutibu moyo”, alisema Eng. Hersi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema asilimia 70 ya gharama za matibabu ya moyo kwa watoto wanaotibiwa katika taasisi hiyo yanalipwa na Serikali na asilimia 30 iliyobaki inalipwa na JKCI pamoja na wadau mbalimbali.

“Katika Taasisi yetu kuna watoto 1500 wanasubiri kufanyiwa upasuaji wa moyo na asilimia kubwa wanatoka katika familia zenye uchumi mdogo hivyo basi ninawaomba wadau mbalimbali waweze kushirikiana nasi katika  kuchangia matibabu ya  watoto hawa kwani tatizo ni kubwa na tunahitaji kuwasaidia ili wapate huduma”,.

“Ninaishukuru klabu ya  Yanga kwa kukubali kushirikana nasi katika  chakula cha jioni  kwa kuchangia gharama za matibabu ya watoto kwani kuna watoto ambao wanatakiwa kufanyiwa upasuaji wa haraka hii ni ndani ya mwezi mmoja baada ya kuzaliwa na kuna wengine wanaweza kusubiri baada ya muda fulani ndipo wakafanyiwa”, alisema Dkt. Kisenge.

Kwa upande wake mjumbe wa bodi ya wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Abdulmalick Mollel  aliishukuru  klabu ya Yanga kwa kuamua kushirikiana na JKCI katika kuchangia matibabu ya watoto wasio na uwezo na kutoa elimu kwa jamii kuhusu magonjwa ya moyo.

“Magonjwa ya moyo ni moja ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza na yanaweza kuepukika kama wananchi watafuata ushauri wa kitaalamu hii ikiwa ni pamoja na kuwa na uelewa wa jinsi ya kujikinga na magonjwa haya, ninaamini tukishirikiana kwa pamoja watu wengi watakuwa na uelewa wa kutosha wa magonjwa haya na kuepukana nayo”, alisema Mollel.
Posted by MROKI On Wednesday, October 02, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo