Nafasi Ya Matangazo

October 03, 2024


Na Mwandishi Wetu, Morogoro
Vikundi mbalimbali vya ushangiliaji kwenye michezo ya 38 ya Shirikisho la michezo ya Wizara, Idara, Wakala za Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa vimekuwa chachu ya ushindi kwa timu zao wakati wa mechi.

Kawaida wachezaji wa timu husika lakini hawachezi mchezo uliopo uwanjani wamekuwa wakiwatia hamasa wenzao kwa nyimbo zenye kuongeza ari na bidii na hatimaye kupata ushindi au kutoka sare.

Mhamasishaji maarufu, Mwalim Shila Mwanchese, ambaye pia ni kocha wa mpira wa netiboli wa klabu ya michezo ya Wizara ya Elimu  amesema kikundi chao kimekuwa na desturi ya muda mrefu ya kushangilia timu zao za kichezo mbalimbali zinapocheza na hata kama hazipo uwanjani wamekuwa wakishangilia pia timu nyingine kwa lengo la kuleta hamasa.

Mwl. Shila amesema kutokana na walimu kusheheni vipaji wamekuwa wakihamasisha kwa kuimba nyimbo za hamasa na wakati mwingine kuweka nyimbo za wasanii mbalimbali zenye kuleta ari ya ushindi.

“Sisi hatujaanza mwaka huu kikundi chetu kipo muda mrefu sana tuseme sisi ni miongoni mwa wahamasishaji wa kwanza kabisa na tunaimba wote wanaume na wanawake, na hata wakati mwingine watu wanaacha kuangalia mechi wanaungana na sisi kuimba na kucheza, hamasa ni nzuri sana kama sisi timu yetu juzi tu hapa walikuwa nyuma kwa tofauti ya magoli mengi lakini tukaimba hadi wakashinda,” amesema Mwl. Shila.

Hatahivyo amesema kikundi chao kinaimba nyimbo zenye maadili mazuri ya kitanzania na matusi kwao ni mwiko, kwa kuwa ni kioo cha jamii na lengo lao kubwa ni kuwapa moyo wachezaji wacheze kwa bidii.

Naye mwongoza kikundi cha ushangiliaji cha timu ya Ofisi ya Rais Ikulu, Wajihi Mkwipunda amesema timu yake ipo vizuri katika kuhamasisha wachezaji wao na hata kama timu zao mbili za michezo tofauti zinacheza kwenye viwanja mbalimbali wamekuwa wakigawanyika makundi mawili na kila mmoja linahamasisha kwa kuimba na kucheza.

“Hamasa ni nzuri inakubalika na watu wetu wanakubali hamasa yetu ambayo inatusaidia kupata ushindi kwenye mechi nyingi tulizocheza kuanzia kwenye mpira wa miguu, netiboli, riadha na kuvuta kamba, kote huko tumefanya vizuri sana,” amesema Wajihi.

Amesema michezo inawaimarisha afya ya akili wachezaji wanafurahi na kuwaondolea msongo wa mawazo.

Kwa upande wake wa klabu ya Wizara ya Uchukuzi, Lugano Mwakyoko amesema hamasa yao kama lilivyo jila la klabu yao la Uchukuzi ni kuchukua ushindi kwa kila timu wanayocheza nayo.

Naye Amie Lupondo, Katibu Mkuu wa Klabu ya Michezo ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki amesema kuwa wachezaji wanaocheza wanatakiwa kutiwa moyo kwa kushangiliwa ili kuwafanya washinde mechi zao.

Amie akitoa mfano wa timu yake amesema baada ya kufanya vibaya kwa bahati mbaya katika michezo ya kuvutana kwa kamba na netiboli, walihamia kwenye uwanja wa mchezo wa mpira wa miguu kuwashangilia hadi wakapata ushindi, inaonesha wanamichezo wanavyopendana kwa kutiana hamasa.
Posted by MROKI On Thursday, October 03, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo